Wanajeshi watatu wa Tanzania wameuawa kwenye shambulio la kombora mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Wanajeshi hao wanahudumu katika kikosi cha kutunza amani cha kijeshi cha Jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika SADC.
Wanajeshi wengine watatu wanasemekana kujeruhiwa.
Taarifa kutoka SADC, haikutoa maelezo kuhusu ni wapi au lini shambulio hilo lilifanyika, au nani aliyelitekeleza .
Februari, mwaka huu wanajeshi wawili wa Afrika Kusini waliuawa kwenye shambulio kama hilo katika jimbo la Kivu Kaskazini.
Katika miezi ya hivi karibuni, maelfu ya watu wamekimbia ghasia zinazoendelea katika maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Wengi wamejificha katika mji mkuu wa eneo hilo wa Goma, ambao wengine wanahofia kuwa M23 wanaweza kuuteka, kama walivyofanya mwaka wa 2012.
Shinikizo limeongezeka kwa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya kuamuru tume kubwa ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa kuondoka nchini humo ifikapo mwisho wa 2024.