Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kilosa
Jeshi la Polisi wilayani Kilosa limewatia mbaroni watu wawili akiwemo Mwenyekiti wa Kitongoji cha Msowero A, Petro Sanga (Paroko) mwenzake, Awadh Ngajime kwa tuhuma za kuuza eneo la mlima, mali ya kijiji cha Msowero wilayani Kilosa.
Pia, inaendelea kuwatafuta watu wengine 48 ambao wanaosadikiwa kuwa sehemu ya mtandao uliohusika kuuza kinyume na utaratibu jumla ya ekari 1158 za Kijiji zilizopo katika mlima huo.
Hayo yamebainika wakati wa mkutano wa hadhara kusikiliza kero za wanachi katika Kata ya Msowero uliotishwa na Mkuu wa Wilaya ya KIlosa Shaka Hamdu Shaka mwishoni mwa wiki kijjijini hapo.
Shaka amesema kumekuwa na wimbi la uvamizi wa maeneo ya ardhi unaoonekana kukithiri siku hadi siku na baadhi ya maeneo wananchi wamekuwa wakihusika kuyauza kinyume na sheria.
“Tuna kata saba ndani ya wilaya hii zinaongoza kwa migogoro ya ardhi ikiwemo hii ya Msowero, mnaongoza mnavamia maeneo ya serikali, viongozi wapo mnashirikiana nao wengine kisha mnageuka mnasingizia viongozi wa wilaya mkoa na taifa kuwa wanakuja kupora ardhi yenu kumbe ni uongo kabisa.
“Mmeuza mlima kinyume na utaratibu ekari 1,158 zote mmevamia na kuuza hii ni mali ya Serikali ya kijiji kisha mnageuka kushutumu wengine kumbe ninyi wenyewe ndio wahusika, Ocd Huyu mwenyekiti aliyeshiriki kuratibu mauziano na kulipwa 500,000 na huyu aliuza eneo la mlima kwa sh 20,000,000 naondoka nao, pia naagiza watu wengine 48 waliohusika kwenye kuuza wajisalimishe polisi, vinginevyo watafutwe popote walipo na wafikishwa kwenye vyombo vya sheria,” alisema.
Hata hivyo, Shaka alipiga marufuku na kuweka zuwio la kuendeleza shughuli yoyote katika eneo la mlima unaodaiwa kuuzwa huku akisisitiza kuwa walioziwa maeneo hayo wametapeliwa na bado ni mali ya Serikali.
“Viongozi mpo mnayaona kitongoji, kijiji, kata wote mnajua lakini mnalea uovu huu, haiwezekani kila aliyehusika kwenye hili hatabaki salama ili iwe fundisho kwa wengine, naomba wajuilisheni wote walionunua eneo lile wametapeliwa na hatutasita kuchukua hatua kwa yoyote atakaekaidi maelekezo ya serikali.
“Kibaya zaidi baada kufanya uovu mnatafuta watetezi ambao na wao kwa kukosa busara na sababu wanatafuta umarufu wa kisiasa, wanalibeba jambo bila kulifanyia utafiti na kujridhisha kumbe mnawaingiza mkenge.
“Nilishangaa sana viongozi wa chama kimoja cha siasa wakilibeba jambo hili wqkidai wananchi wananyanganywa ardhi wanapigwa na kuindoshwa katika maeneo yao, kumbe mumewalisha matango pori mnaficha uovu wenu na wao kwa kwa vile maarifa yao madogo wakaona ndio ajenda ya kuibeba limebuma sasa warudi kukanusha uongo waliouaninisha umma wa watanzania. Alifafanua Shaka.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Msowero Abdalla Machera alimueleza mkuu wa wilaya kuwa katika siku za karibuni viongozi wa kisiasa wamekuwa wakifika katika maeneo yao huku wakilazimisha wananchi kupigwa picha na kutoa malalamiko ama shutuma za uongo dhidi ya Serikali jambo ambalo amesema sio la kiungwa na kistarabu.
” Mheshimiwa DC unayoyasikia huko ni kutaka kuchafua kata yetu na viongozi wetu ninyi ili wao kutafuta kuungwa mkono kwa mambo ya uongo na uzushi, yaliopo hapa ni baadhi ya wananchi kujihusisha katika matendo maovu sasa wakiona mnataka kuwachukulia hatua wanakimbilia kwa viongozi wa kisiasa ili wapaze sauti wakidhania wanaweza kuzima uovu wao wasichukuliwe hatua kwa makosa yao, haiwezekani, wameuza mlima wetu ekari 1158″ amesema Abdallah Kweche mwenyekiti wa kijiji cha Msowero
Jumla ya wananchi 50 wanadaiwa kuhusika katika kuuza kwa watu mbali mbali kutoka nje ya wilaya kwa ajili ya shuhuli za kilimo na ujenzi wa makazi na wengine kuvamia kuweka makazi na kilimo ambapo imebainika kuna uharibifu mkubwa wa mazingira.