1: Sioni pa kuanzia, Kueleza taarifa,
Nchi yetu Tanzania, Imekumbwa na maafa,
Taifa zima twalia, Ni msiba wa taifa,
Watu mia na zaidi, Leo tumewapoteza.
2: Raia kwa wanafunzi, Na wazazi kwa watoto,
Wametujaza simanzi, Na mili kuwa mizito,
Mili imeshika ganzi, Ni kwa hili jambo zito,
Jamani watanzania, Tuwaombee wenzetu.
3: Tumeumbiwa upofu, Kifo kwetu bado fumbo,
Ijapo tunayo hofu, Ya kifo tangu kitambo,
Tutembeapo tu wafu, Tulijue hili jambo,
Kifo hakibishi hodi, Popote waweza kufa.
4: Japo ni mengi mawazo, Vichwani yalotufika,
Kutafakari tatizo, Kwa ndugu walotutoka,
Ya nchi maombolezo, Msiba umetufika,
Jama tupige magoti, Kumrudia Muumba.
5: Leo ni wana Ukala, Imetimu yao zamu,
Tuwaombee kwa sala, Ili wafike kuzimu,
Ingawaje hili suala, Linaacha swali gumu,
Je, tatizo ni ubovu, Au chanzo ni uzembe?
6: Maswali najiuliza, Nini chanzo cha ajali?
Nani wa kunileza, Ijue yangu akili?
Tukio linaumiza, Wananchi serikali,
Ndugu wana Bugolora, Mamia tumewazika.
7: Twaomba wawajibishwe, Wote waliohusika,
Kwenye vyombo wafikishwe, Tena iwe kwa haraka,
Uzembe na ukomeshwe, Kabla hatujazika,
Tukio linaumiza, Kupoteza nguvu kazi.
8: Yapungua yangu kasi, Si kama ile ya mwanzo,
Kwa hili wingu jeusi, Vyema tutafute chanzo,
Wananchi na Rais, Ajali itupe funzo,
Haya yaliyotokea, Kesho yasijirudie.
9: Nimefikia tamati, Machungu kuelezea,
Kwenye wa tisa ubeti, Ndipo ninapokomea,
Nizionapo maiti, Kwa uchungu ninalia,
Ya mv Nyerere, Yametuachia kovu.
Mwalimu Tobias Siwingwa (Msakatonge)
0755721609