Na Mwandishi Wetu

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amesema wametoa treni maalumu ya kisasa (SGR) kusafirisha takribani watu 922 wanaotarajiwa kushiriki kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) unaofanyika kesho na kesho kutwa jijini Dodoma.

Hivyo amewashukuru wakiwamo wajumbe 600 wa CCM kutumia SGR kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma unapofanyika mkutano huo. Wajumbe wa CCM kutoka maeneo mbalimbali nchini wanakutana Dodoma kwa Mkutano Mkuu.

Kabla ya mkutano huo, kunatarajiwa kufanyika kikao cha Kamati Kuu na kufuatiwa na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) jijini humo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Stesheni ya Magufuli Dar es Salaam jana, Kadogosa amesema, “Wajumbe wa CCM wako zaidi ya 600, kutoka Lindi, Mtwara, Zanzibar, Dar es Salaam, Pwani tutawachukua Soga, Morogoro…

Lakini pia kuna wageni na wasanii mbalimbali walioalikwa kwenye mkutano huo, tunasafirisha takribani abiria 922, nawashukuru CCM kwani wangeweza kusafiri kwa kutumia mabasi au ndege, lakini wameamua kutumia treni.

Alisema usafiri wa SGR ni moja ya mambo yaliyopo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020 – 2025, hivyo wajumbe hao wa CCM kutumia usafiri huo inawafanya kujivunia chama chao.

“Mpaka sasa tangu tumeanza usafirishaji tume shasafirisha abiria takribani milioni 1.4, ni watu wengi sana, wastani wa watu 7,000 mpaka 10,000 kwa siku lakini haimaanishi changamoto hazipo, zipo na Watanzania wajue hivyo,” ameeleza.