Setilaiti ya mawasiliano iliyotengenezwa na kampuni kubwa ya vyombo vya angani ya Boeing imevunjika kwenye uzingo.

Mwendeshaji satelaiti, Intelsat, amethibitisha “hasara ya jumla” ya iS-33e, ambayo imeathiri wateja katika maeneo ya Ulaya, Afrika na sehemu za eneo la Asia-Pasifiki.

Intelsat pia inasema imechukua hatua kukamilisha “uchunguzi wa kina” wa tukio hilo.

Boeing imekuwa ikikabiliwa na migogoro katika nyanja nyingi, changamoto upande wa ndege za kibiashara na chombo chake cha Starliner.

“Tunashirikiana na mtengenezaji wa satelaiti, Boeing, na mashirika ya serikali kuchanganua data na kufanya uchunguzi,” Intelsat ilisema.

Boeing haikutoa maoni yake moja kwa moja kuhusu tukio hilo, ikirejelea BBC News kwenye taarifa za Intelsat.

Tovuti ya Idara ya Ulinzi ya Marekani ya kufuatilia vyombo vya kwenye anga, SpaceTrack, pia ilithibitisha tukio hilo.

Tahadhari kwenye jukwaa ilisema Jeshi la Anga za Juu la Marekani pia “kwa sasa inafuatilia vipande 20 vinavyohusika” na satelaiti hiyo.

Ikumbukwe kwamba wanaanga wawili wamekwama katika Kituo cha Kimataifa cha Anga za Juu (ISS) baada ya chombo cha Boeing Starliner walichowasili nacho mnamo mwezi Juni kuonekana kutofaa katika safari ya kurudi.