Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Mfamasia Mkuu wa Serikali Daud Msasi amewahakikishia Watanzania kwamba dawa zinazozalishwa nchini zimethibitishwa na zina ubora unaostahili.
Msasi ametoa kauli hiyo leo Aprili 6,2023 kwenye semina kwa wahariri wa habari nchini iliyoandaliwa na Bohari ya Dawa (MSD) ambapo baadhi ya wahariri walitaka kufahamu ubora wa dawa zinazozalishwa nchini iwapo zina ubora sawa na zile zinazotoka nje ya Tanzania.
“Dawa zetu ni bora, ila tiba ni pamoja na mtazamo, unakunywa dawa halafu unasema hata nikinywa siponi. Niwahakikishie dawa zetu zina ubora unaostahili na zimethibitishwa.
“Familia yangu tunakunywa dawa za Tanzania na sababu TMDA yuko nyumbani, anaweza kukagua mara kwa mara. Dawa zote tunazokunywa zimethibitishwa na TMDA ambayo kwa ubora Afrika ni ya kwanza, hivyo dawa zetu zinaweza kwenda hata Marekani,” amesema Msasi.
Akijibu swali kuhusu idadi ya viwanda vya dawa na vifaa tiba vilivyopo nchini, Mfamasia Mkuu wa Serikali amesema kwa sasa kuna viwanda 11 vinavyozalisha dawa na 24 vya vifaa tiba, hivyo jumla vipo viwanda 35.
Hata hivyo, amesema Bohari ya Dawa inajitahidi kuhakikisha huduma zake hazisimami kwani hilo likitokea husababisha athari ambazo huonekana baada ya muda.
“Matokeo yanakuja baada ya miezi 12 mzima, sifuri (kukatika kwa mnyororo wa usambazaji) mwaka 2019/2020 matokeo yakaja 2022,” amesema.
Amesema kazi kubwa imeendelea kufanyika na sasa ukienda malalamiko ya ya upungufu au kukosekana kwa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya yamepungua.