Tumesikia habari za Serikali za Mitaa. Wakati nchi yetu ilipokuwa chini ya Mjerumani hakukuwa na Serikali za Mitaa. Kulikuwa na Serikali Kuu tu ambayo ni Serikali moja ya nchi nzima.

Alikuwa Gavana wa pili Mwingereza, Donald Cameroon, aliyeanzisha Tanganyika (Tanzania Bara) Serikali za Mitaa mwaka 1927.

 

Serikali za Mitaa ni mfumo wa utawala ulioundwa  kwa ajili ya maeneo mbalimbali. Madhumuni ya kuwapo Serikali za Mitaa ni kupeleka madaraka kwa wananchi.

 

Katika serikali mbili, Serikali Kuu na Serikali za Mitaa,  serikali iliyo karibu zaidi na wananchi ni Serikali ya Mitaa. Kwa mfano, wakati ngazi ya chini kabisa katika Serikali Kuu ni tarafa, ngazi ya chini kabisa katika Serikali za Mitaa ni mtaa (mijini) na kitongiji (Vjijini).

 

Hii ina maana kwamba Serikali za Mitaa zikifanya kazi vizuri, hurahisisha utendaji wa Serikali Kuu, pia hupunguza kwa kiasi kikubwa malalamiko yanayoelekezwa kwenye Serikali Kuu. Lakini, ukitaka kusema kweli Serikali za Mitaa katika nchi yetu kwa kiasi kikubwa zimeshindwa kufanya kazi. Inayofanya kazi ni Serikali Kuu hadi huku mitaani na vijijini.

 

Wakati Rais Jakaya Kikwete alipofanya ziara mkoani Dar es Salaam mwezi Machi mwaka huu, alifika mahali akauliza: “Hivi madiwani mnapokutana kwenye vikao nyenu mnajadili nini?” Hili lilikuwa swali la msingi kama tujuavyo wabunge ni madiwani wa Serikali za Mitaa (halmashauri) za maeneo yao, lakini unakuta mbunge analalamika nje ya vikao vya halmashauri, jambo ambalo ungetazamia kuwa madiwani wangejadiliana katika vikao vyao.

 

Ni katika mazingira hayo naunga mkono swali la Rais Kikwte lililotaka kujua, madiwani wanapokutana wanajadili nini? Chukua, kwa mfano, Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu, ambaye pia ni Diwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke. Huyu aliwahi kulalamika kuhusu idadi kubwa ya ombaomba iliyopo mitaani. Ikaishia hapo.

 

Ninaamini suala la ongezeko la ombaomba katika mitaa ya Dar es Salaam (hasa katika Manispaa ya Ilala) linamkera kila mtu. Kwanza kwa sababu linadhalilisha Taifa.

 

Pili, kwa sababu hao wanaoomba wana nguvu za kufanya kazi. Lakini badala ya kufanya kazi wanashinda kando ya mahekalu ya ndugu zetu Waasia wakiomba.

 

Tatu, sasa suala la ombaomba linahusisha watoto wadogo ambao hawataki kusoma na wataongeza idadi ya watoto wa mitaani.

 

Wakati umefika kwa madiwani wote wa Manispaa za Dar es Salaam kujadili katika halmashuri zao suala la ombaomba na kulitafutia ufumbuzi. Halmashauri za Manispaa ziwahusishe ombaomba suala hili, wafanyakazi wa Idara ya Ustawi wa Jamii, ambayo tabia yao ni kudumu ofisini badala ya kuyashughulikia masuala haya mitaani.

 

Kana kwamba malalamiko ya Mbunge na Diwani wa Temeke, Mtemvu, hayakutosha, naye Mbunge na Diwani wa Manispaa ya Ilala, Azan Zungu, amekuja na malalamiko yake. Analalamika kwamba adui wa wafanyabiashara ndogo ndogo Dar es Salaam (wamachinga), ni askari wa mgambo ambao huwapora wafanyabiashara hao vitu vyao na kuwaacha katikati ya matatizo.

 

Tabia ya wanamgambo wa Manispaa za Dar es Salaam kupora wafanyabiashara vitu vyao badala ya kuwapeleka mahakamani, ni ya siku nyingi na inakera sana wananchi. Madiwani wanajua hivyo na wanamgambo ni sehemu ya Halmashauri za Manispaa ambazo madiwani ni wajumbe wake. Na hawa madiwani ni wawakilishi na watetezi wa wananchi.

 

Lakini wameshindwa kuwatetea na sasa wamebaki wanalalamika mitaani badala ya kujadili kero hii kwenye Halmashauri. Wanapokutana wanajadili nini kama hawajadili kero za wananchi? Kuna tatizo la dawa za kulevya ambalo Serikali Kuu imeachwa inalihangaikia peke yake wakati wenyeviti wa Serikali za Mitaa, madiwani na maofisa watendaji wa kata wanawajua fika watu wanaojishughulisha na dawa za kulevya katika mitaa yao.

 

Kwanini Serikali Kuu imeshindwa kushirikiana na viongozi wa Serikali za Mitaa katika kukomesha tatizo la dawa za kulevya na matatizo mengine?

 

Vijijini kuna tatizo la kutofanyika mikutano ya serikali za vijiji, kuporwa wananchi ardhi yao, mapambano ya wakulima na wafugaji, uharibifu wa mazingira, nk. Matatizo hayo yote yameachwa yashughulikiwe na Serikali Kuu badala ya kushughulikiwa mara moja na Halmashauri za Wilaya.

 

Hivi madiwani wanapokutana katika vikao vyao wanajadili nini kama wanaacha kujadili matatizo ya maeneo yao?