Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Novemba 27, 2024 Tanzania ilifanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepata ushindi asilimia 99 na zaidi. Nimejaribu kufuatilia nini kimetokea? Nimebaki na maswali mengi. Yapo maeneo unatajiwa unaona harufu ya kuonewa. Yapo maeneo unatajiwa unaoja harufu ya kujihujumu.
Sitanii, nitazungumza kwa uchache hayo ninayoyaita maeneo, ila nitazungumza pia juu ya vurugu zilizotokea maeneo mbalimbali nchini. Nianze na la mbinu za kimkakati. Maeneo mengi CCM kimepita bila kupingwa ingawa walipiga kura za ndiyo na hapana. Nimejiuliza imekuwaje? Mbona wapinzani wakiwa na mikutano inajaa washiriki?
Nimejitahidi kufuatilia kilichoendelea. Nimesikia matukio yanayotajwa kuwa ya mauaji ya kisiasa, Mbeya na Singida. Nimesikia matukio maeneo mengine ya nchi, ambayo watu ama wamepigana au kutukanana.
Hili limenipa shida kuliko yote. Hasa hili la vifo vinavyohusishwa na ufuasi au ushabiki wa kisiasa. Nimejiuliza hivi nchi yetu imefika hapo kweli?
Sitanii, kwamba mtu anaona aingie madarakani au abaki madarakani kwa kuua binadamu mwenzake kweli? Nimejaribu kufuatilia yalikotokea haya matukio. Nimeelezwa chanzo kikubwa ilikuwa ni siasa za chuki, kuzodoana, matusi na kejeli, za hamuwezi, tunaweza, hamfai, tunafaa, ndizo zimeleta maafa haya. Hili limenifahamisha jambo ninalodhani vyombo vya habari vinapaswa kulifanya.
Nimebaini kuwa katika nchi yetu, siasa imechukuliwa kama imani au ajira. Hili ni wazo na mkondo mbaya mno. Siasa za nchi yetu zinapaswa kushindanisha sera. Mfano mzuri nitalitumia taifa la Marekani. Novemba mwaka huu, wamefanya uchaguzi. Vimeshindana vyama vya Republican na Democrat. Katika uchaguzi huo, ukiacha undambwe, wameshindanisha sera.
Democrat waliokuwa chama tawala, walijipambanua kwa kuihakikishia dunia kuwa wao wanataka kuendeleza ushoga, usagaji na vita ya Ukraine dhidi ya Urusi. Chama cha Republican chini ya Rais Mteule Donald Trump, kilijipambanua kwa kupinga ushoga, usagaji, vita na mfumko wa bei.
Trump aliwaambia Wamarekani kuwa iwapo angechaguliwa, basi masilahi ya Marekani yangekuwa ya kwanza kabla ya mataifa mengine.
Wagombea Kamala Harris na Donald Trump kutoka Democrat na Republican, mtawalia, kwa miezi minne walipepetana wakieleza sera zao kwa wapigakura na hatimaye Trump akachaguliwa. Natamani Tanzania tufikie hatua hii. Wagombea wetu waeleze sera. Watueleze tukiwachagua watalifanyia nini taifa letu, si kila siku kutukanana kwa ajili ya jinsia au uwapo katika vyama.
Sitanii, nchi yetu nafahamu imekuwa kwenye mfumo wa vyama vingi kitambo. Ni zaidi ya miaka 30 sasa tukiwa katika mfumo huu, hata hivyo, dozi iliyotolewa chini ya chama kimoja kati ya mwaka 1965 na 1992, ilikuwa kubwa mno. Najua kipo kizazi kinachoamini katika chama kimoja. Hawa wakikuona unazungumza na Freeman Mbowe au Tundu Lissu wa CHADEMA, haraka wanakwekea alama mgongoni na kusema, huyu si mwenzetu.
Kwa upande wa wapinzani, wakikusikia mtu anazungumza na Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi au viongozi wengine wa CCM, haraka wanakutangaza kuwa ni kibaraka wa chama tawala. Kumbe imefika wakati sasa, hatushindanishi sera za vyama kuwatumikia wananchi, badala yake tunashindanisha imani na itikadi kali. Naamini kama tulivyoamua kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi, ni vyema tuukubali.
Dhana ya kuingia kwenye uchaguzi wengine wakifahamu matokeo na wengine wakifanya makosa yasiyotarajiwa kama nitakayoyataja hapa chini, inanipa shida. Hapa nizungumzie jambo la pili. Nafahamu Rais Samia Suluhu Hassan alielekeza wagombea wa upinzani katika serikali za mitaa waliokuwa na makosa madogo madogo warejeshwe kugombea.
Sitanii, wagombea zaidi ya 5,800 walirejeshwa kwenye kinyang’anyiro. Hata hivyo, kuna hoja imenipa shida. Ilikuwa zinagombewa nafasi zipatazo 63,000. Nimeambiwa Chama Kikuu cha Upinzani CHADEMA kilisimamisha wagombea 14,000 na chama tawala CCM kikasimamisha wagombea katika nfasi zote 63,000. Hii ina maana kuwa kabla ya uchaguzi kuanza, CCM waliishajihakikishia ushindi kwa wagombea 59,000.
Swali ni je, wapinzani walisindwaje kupata wagombea angalau asilimia 50? Nitaje kosa moja kati ya mengi yaliyojitokeza. Mfano Jimbo la Bukoba Mjini, wagombea wa CHADEMA, walienguliwa wote kwa kosa la muhuri. Badala ya muhuri kusomeka Chama cha Demokrasia na Maendeleo, muhuri ukawa unasomeka Chama cha Maendeleo na Demokrasia. Hili najiuliza ni hujuma ya ndani kwa ndani au ni uwezo mdogo?
Kwa vyovyote iwavyo, Tanzania ni yetu sote. Tunajifunza kutokana na makosa. Swali kubwa ninalojiuliza, ni iwapo haya yametokea hivi katika uchaguzi wa serikali za mitaa, uchaguzi mkuu itakuwaje? Naamini hapa ndipo vyombo vya habari tuna jukumu la kuingia. Tutoe elimu ya uraia. Vyama vinadi sera kwa wananchi badala ya kushambuliana. Hatujachelewa, TUJISAHIHISHE.
0784 404827