Serikali imezugumzia malalamiko ya watumiaji wa bidhaa ya Saruji aina ya Hauxin inayozalishwa na kiwanda cha Maweni Limestone Limited kilichopo Mkoani Tanga kuhusu upungufu wa uzito wa bidhaa hiyo.

Naibu Waziri wa uwekezaji,viwanda na biashara Exaud Kigahe (Mb) ameyabainisha hayo leo jijini Dodoma wakati akieleza mwenendo wa bei za bidhaa muhimu nchini kwa April,2023 ambapo amesema kuwa kwa mujibu wa kifungu namba 41 (a) na (b) cha sheria ya vipimo, sura ya 340 kinatoa katazo kwa mtu yeyote kuuza bidhaa yoyote iliyo chini ya uzito, kipimo au namba kama inavyohitajika kwa mujibu wa sheria.

Naibu Waziri Kigahe amesema sheria hiyo pia inatoa katazo kwa yeyote katika ufanyaji biashara kutoa taarifa za uongo juu ya bidhaa yoyote kuhusu uzito, kipimo, namba, geji au kiwango na endapo makosa hayo yatafayika wote watakuwa wametenda kosa kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wa mweye duka anajukumu la kuhakiki kila bidhaa anayouza kabla ya kumuuzia mlaji wa mwisho na kujiridhisha kuwa bidhaa husika ipo katika hali inayotakiwa kulingana na matakwa ya sheria.

Kigahe amesema sheria hiyo ya vipimo sura ya 340 inatoa adhabu mbili kwa mtu ambaye atakuwa ametenda makosa hayo endapo atakuwa amekiri kosa sheria inampa mamlaka Kamishina wa Wakala wa vipimo kufifisha kosa (compounding of offences) na kumtoza faini ya kiasi kisichopungua shilingi laki moja na kisichozidi milioni ishirini na hiyo ni kwa mujibu wa kifungu cha 46 cha sheria ya vipimo.

Aidha Kigahe amesema sheria hiyo imetoa adhabu ya jumla kwa yeyote ambaye atakuwa ametenda kosa chini ya sheria na ni mkosaji wa mara ya kwanza akitiwa hatiani mahakamani basi atawajibika kulipa faini kiasi kisichopungua laki tatu na kisichozidi milioni hamsini au kifungo kisichozidi miaka miwili au vyote kwa pamoja na endapo ni mara yake ya pili akitiwa hatiani atawajibika kulipa faini isiyopungua kiasi cha shilingi laki tano na isiyozidi milioni mia moja au kifungo kisichopungua miaka mitano au vyote kwa pamoja.

Hata hivo Naibu Waziri huyo amesema baada ya mweye duka kukiri kosa, amechukuliwa hatua za kisheria kwa kufifilishwa kosa kama iliyoelezwa kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kulipa faini na kupewa maelekezo mengine ikiwemo kufanya marekebisho ya mapungufu yaliyojitokeza.

Kigahe ametoa wito kwa wazalishaji wa bidhaa zote za viwandani kuongeze jitihada za uzalishaji wa bidhaa Kwa ubora unaohitajika sokoni na Kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kukabiliana na mfumuko wa bei na bidhaa mbalimbali.