Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Habari,Mawasiliano na Technolojia ya Habari imezindua Kampeni ya Tumewasikia Tumewafikia ambayo itakwenda nchi nzima kufahamisha umma kazi kubwa iliyofanywa na inayoendelea kufanywa na serikali ya awamu sita kwenye sekta za maji, afya, miuondombinu na miradi mingine ya maendeleo.
Aidha Kampeni hiyo inawataka wakuu wa mikoa yote 26 na wakurugenzi wa halmashauri zote 184 nchini, kuandaa mikutano na vyombo vya habari ili kutangaza kwa wananchi kazi zinazofanywa na serikali yao.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye, ameeleza hayo wakati akizindua mikutano ya wakuu wa mikoa, wakurugenzi na vyombo vya habari jijini hapa jana alisema pamoja na kazi kubwa inayofanywa na serikali ya awamu ya sita wananchi bado hawana taarifa za kutosha.
Nnauye, amesema anaipongeza Idara ya Habari (Maelezo) kwa kuja na ubunifu huo na kuja kampeni hiyo ambayo wakuu wa mikoa pamoja na wakurugenzi wa halmashauri nchini wataitumia kuandaa mikutano na vyombo vya habari.
“Lengo la kampeni hii ni kuongeza chachu ya mawasiliano kati ya wananchi na Serikali yao kwa kuwa itatoa nafasi ya wakuu wa mikoa pamoja na wakurungezi kueleza mambo ambayo yamefanywa,Serikali inatoa fedha nyingi za utekelezaji wa miradi hivyo wananchi wana haja ya kufahamu kodi zao zinafanya nini, “amesisitiza
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) Mobhare Matinyi, amesema lengo la kuanzishwa kwa kampeni hiyo ni kuwafikisha wananchi ngazi ya chini tarifa kuhusu kazi inayofanywa na serikali yao.
Amesema kupitia program hiyo wananchi watapata fursa ya kueleza kile ambacho serikali yao imefanya na kimewanufaisha kwa namna gani
“Hivi sasa serikali inafanya mambo makubwa sana katika maeneo mbalimbali lakini ukiangalia ukubwa wa kazi unaofanywa na taarifa zinavyosemwa ni mbigu na ardhi,hivyo kampeni hii itasaidia kufikisha taarifa sahihi kwa wananchi kuhusu kile kinachofanywa na serikali yao na kuondoa ‘gap’ lililopo hivi sasa baina ya serikali na wananchi, “amesema