*Yaguswa ubunifu tuzo za kihistoria TEHAMA 2025
Na Mwandishi Maalumu, JamhuriMedia, Arusha
JIJI la Arusha limeandika historia ya kuwa mwenyeji wa kwanza wa Tuzo za TEHAMA Tanzania, huku Serikali ikiahidi kufanya kila linalowezekana katika kuikuza sekta ya TEHAMA ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha nchi inakwenda kuujenga kwa kasi uchumi wa kidigitali.
Aidha, imeahidi kuwafikia Watanzania wote, lengo likiwa kuhakikisha hakuna Mtanzania atakayeachwa nyuma katika sekta ya TEHAMA.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa aliyezindua na kutoa tuzo za TEHAMA za mwaka 2025 kwa washindi takribani 50 kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango ambaye alikuwa na majukumu mengine ya kitaifa, akimwakilisha Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Alipongeza kuanzishwa kwa tuzo hizo, akisema zitasaidia kuchochea ubunifu wa masuala ya TEHAMA na kukuza sekta ya Tehama nchini ambayo ni muhimu katika uchumi wa kidijitali.
“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan mara zote amekuwa akitoa maelekezo ya kuhakikisha tunatekeleza Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali wa kitaifa wa miaka kumi (10), hivyo basi, tusingependa kumuacha nyuma hata mdau mmoja, lazima tushirikiane kuhakikisha sekta yetu ya Tehama tunaikuza,” alisema.

Aliiagiza Tume ya TEHAMA kuhakikisha Tuzo hizo zinakuwa endelevu na zinafanyika kila mwaka kwa weledi na viwango vya hali ya juu ili kuvutia wadau zaidi kushiriki.
Tuzo hizo zilizoandaliwa na Tume ya Tehama (ICTC) kwa kushirikiana na kampuni ya SoftVentures, Chama cha Watoa Huduma za Intaneti Tanzania (TISPA), zilitoa fursa kwa washiriki 380 kuwasilisha kazi zao zilizochujwa kitaalamu na kuthibitishwa na Kampuni ya Kimataifa ya Deloitte ambayo imekuwa na jukumu la kutoa ushauri na usimamizi katika mchakato wa tathmini ya tuzo.
Awali, akitambulisha tuzo hizo na kumkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga alisema lengo la Tume yake kutoa tuzo hizo ni kuhamasisha watu kufanya ubunifu mzuri wa masuala ya TEHAMA nchini.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohamed Abdullah alitoa wito kwa Tume ya TEHAMA kuhakikisha mwakani mchakato wa tuzo hizo unakuwa mzuri zaidi na kushirikisha wadau wengi zaidi.
Baadhi ya washindi wa tuzo hizo akiwemo, Nafidh Ally Mola mwanafunzi wa mwaka wa kwanza kozi ya Sayansi ya Kompyuta katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Dar es Salaam na Dorice Malle kutoka Taasisi ya Mama Mia’s Soko walisema tuzo walizopata zitawajengea hamasa zaidi katika kazi zao za ubunifu kwa kuwa zimewapa heshima katika jamii.
Washiriki wa Tuzo za TEHAMA 2022 walichuana katika vipengele vya Ubunifu katika Bidhaa au Huduma za TEHAMA, Matumizi Bora ya TEHAMA, TEHAMA kwa Maendeleo ya Jamii, Kijana Aliyefanikiwa Katika TEHAMA, Wanawake Katika TEHAMA, Usalama wa TEHAMA, Mradi wa TEHAMA wa Sekta ya Umma, TEHAMA Endelevu, Tuzo za TISPA kwa Mtoa Huduma Bora ya Uunganishaji wa Mtandao na kadhalika.







