Na Daniel Limbe, JamhuriMedia, Chato
SERIKALI mkoani Geita imewataka watumishi wa umma wajiepushe na mikopo ya kinyonyaji kutoka kwenye baadhi ya makampuni binafsi ya ukopeshaji fedha badala yake watumie vyama vyao vya kuweka na kukopa Saccos.
Mrajis msaidizi wa Ushirika Mkoa wa Geita, Doreen Mwanry, amesema baadhi ya watumishi wamekuwa wakikutana na madhira mbalimbali kutoka kwa baadhi ya makampuni ya ukopeshaji ikiwemo kudhalilishwa baada ya kushindwa kurejesha mikopo yao kwa wakati pamoja na kukosa utulivu kazini.
Kwamba njia pekee ya kuepukana na kero hizo ni kujiunga na vyama vya ushirika ili wakopeshane wenyewe kwa utaratibu mzuri wanajiwekea jambo litakalo wasaidia kuwa na utulivu wa nafsi.
Alikuwa akizungumza kwenye mkutano mkuu wa kawaida wa mwaka wa Chama cha kuweka na kukopa cha walimu ( Chato Teachers Saccos) ambapo pamoja na mambo mengine amewasihi kukopa kwa ustaarabu na kurejesha kwa wakati ili kuifanya taasisi yao kujiendesha kwa faida na kutatua changamoto zao za kifedha.
Kutokana na hali hiyo,Katibu tawala wa wilaya ya Chato,Thomas Dime,amewataka viongozi na wanachama kujiepusha na migogoro kwa madai ni moja ya sababu zinazochangia kusambaratika kwa saccos nchini.
Kadhalika ametumia fursa hiyo kumtaka mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo,kulipa deni la zaidi ya milioni 9 anazodaiwa na Saccos hiyo kwa kipindi kisichozidi siku 60 ili kuondoa usumbufu kwa saccos hiyo kufuatilia deni hilo kila mwaka.
Hata hivyo,Kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo,Gaston Misingi,amekiri kuwepo kwa deni hilo na kudai kuwa halmashauri inaendelea na mchakato wa kulipa deni lote na kuwataka wananchama hao kuwa na subira.
Kwa upande wake meneja wa Saccos hiyo Mwl. Pius Katani, amesema pamoja na changamoto za uwepo wa mikopo chechefu taasisi hiyo inakwenda vizuri na kwamba wamefanikiwa kupata hati safi za ukaguzi wa hesabu kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo.
Hata hivyo,mwenyekiti wa Chato Teachers Saccos, Mwl. Petro Rwegasira, amesema malengo ya kuanzishwa kwa Saccos hiyo ni kuwasaidia watumishi wa umma kutatua changamoto zao za kifedha kwa muda mwafaka, kusaidia utulivu wa nafsi,kuongeza ufanisi wa uwajibikaji katika majukumu yao pamoja na kustili aibu ya kudhalilishwa kwenye taasisi zingine za fedha.