Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Dodoma

Serikali yawapa Mawakili Wafawidhi wa Serikali siku kumi nne kuanzia leo kuwasilisha orodha ya kesi zilizopo kwenye taasisi za umma wanazofanyia kazi pamoja na majina na vyeo vya wahusika waliosababisha kesi hizo.

Maelekezo hayo yalitolewa na Waziri wa Katiba na Sheria,Dkt. Damas Ndumbaro wakati akifunga Mkutano wa Mawakili wa Serikali uliofanyika kwa siku tatu mkoani Dodoma.

Waziri Dkt.Ndumbaro aliwataka Mawakili hao kuandaa orodha ya kesi zote za madai zilizo kwenye taasisi zao; chanzo na sababu ya kesi hizo; taarifa hiyo ieleze gharama au hasara ambayo Serikali inaweza ikaingia; na taarifa iseme ni nani amesababisha kesi hiyo kwa jina na cheo chake; na taarifa hizo za kesi ziwasilishwe kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndani ya kipindi cha wiki mbili.

“Niwaelekeze Mawakili muwasilishe taarifa hizo za kesi zilizopo kwa kuwa taasisi nyingine zimekuwa ni vyanzo vya kuzalisha migogoro na mhusika aliyehusika kuzalisha mgogoro huo hausiki tena wala kutoa ushirikiano kwa Mawakili kwa kuwapatia taarifa za kutosha kuendesha majadiliano, mashauri, usuluhushi pamoja na kuiwakilisha Serikali mahakamani,” amesema Waziri Dkt. Ndumbaro.

Pia, amewaeleza Mawakili wote wa Serikali wajiandae kuelimisha umma kuhusu Katiba tuliyonayo na haki za binadamu ili kujenga uelewa kwa wananchi na kupata hoja zao badala ya kupata hoja kutoka kwa wanasiasa pekee hasa tunapoelekea kuwa na katiba mpya ikizingatiwa kuwa haya ni maelekezo ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi, Chama Tawala kinachoongoza Serikali ya Awamu ya Sita iliyopo madarakani chini ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuwajengea uwezo Mawakili wake ili wawe na ujuzi na ueledi katika masuala ya mikataba; uchumi wa bluu; haki za binadamu; na uendeshaji wa mashtaka ili kuweza kuendesha kesi kwa weledi na amewaasa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia uadilifu; maadili; mila, desturi na tamaduni za nchi yetu; misingi ya katiba na sheria za nchi.

Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Jaji Dkt. Eliezer Feleshi amewaasa viongozi wa mpito walioteuliwa kuongoza Chama cha Mawakili wa Serikali kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa kuhakikisha kuwa wanalinda imani ya viongozi wa taasisi zao na imani ya wanachama kwa kuongoza chama hicho kwa kuzingatia malengo ya uanzishwaji wake badala ya kuwa jukwaa la siasa kwa kuwa Serikali inategemea kupata maoni na ushauri wa kitaalam kutoka kwa wanachama kuhusu masuala ya kisheria yanayohusu taifa letu.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo akizungumza na Mawakili wa Serikali (hawapo pichani) wakati wa kufunga mkutano wa Chama cha Mawakili wa Serikali uliofanyika kwa siku mbili jijini Dodoma

Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria,Mary Makondo amesema kuwa Wizara yake imeyapokea maelekezo ya Rais Samia na watayafanyia kazi ili kuratibu utekelezaji wa majukumu ya Mawakili hao ndani ya utumishi wa umma pamoja na kulea Chama cha Mawakili wa Serikali kwa kipindi cha miaka mitatu.

.