Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kwa maelezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, serikali imeunda tume ya watu 19 itakayohusika kupitia maghorofa yote Kariakoo ili kutambua ubora wa kila jengo.
Hatua hiyo imetokana na kuanguka kwa jengo Novemba 15, na kusababisha vifo vya watu 15, na wengine kuokolewa kwenye vifusi.
Akizungumza leo Novemba 18, katika tukio la kuiaga miili ya watu waliopoteza maisha viwanja wa Mnazi Mmoja Kariakoo, Dar es Salaam, Majaliwa tume hiyo itasaidia kutambua na kuishauri serikali nini ifanye baada ya uchunguzi huo.
“Soko la Kariakoo ni la kimataifa kwa sasa linategemewa na nchi zote zinazotuzunguka hapa jirani, tunayo sababu ya kuimarisha lakini pia kutambua ubora wa majengo tuliyonayo, ili wajasiriamali waendelee kufanya biashara zao kwa miongozi mipya itakayotolewa na serikali baada ya tume hii kuchunguza na kutoa ushauri kwa serikali,” amesema Majaliwa.
Majaliwa amesema tume hiyo itaongozwa na mwenyekiti wake Brigedia Jenerali Hosea Ndagala Mkuu wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu na katibu wake atakuwa Mhandishi Melecky Mwano kutoka Bodi ya Usajili ya Wakandarasi.