Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Singida

MKUU wa Wilaya ya Singida,Mhandisi Paskas Mragili, amezitaka shule za msingi na sekondari wikayani hapa kujipanga kuingia katika mfumo wa ufundishaji kwa njia ya kidigitali kwa kuwa mpango wa serikali ni kutaka utendaji wote uwe unafanyika kidigitali.

Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili, akimkabidhi Kishikwambi Sr. Josephine Revelion kutoka Shule ya Musange.

Amesema hayo jana baada ya kukabidhi walimu vishikwambi 270 ambavyo vitatumika katika shule 135 za msingi na sekondaji kwa ajili ya kufundisha masuala ya elimu ya uzazi na jinsi ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

“Mpango wa serikali ni kutaka kuhama kabisa katika utendaji wa ‘analog’ kwenda kwenye utendaji wa kidigitali hivyo lazima shule zijipange kuingia katika mfumo huo,” amesema.

Mragili amesema anafahamu zipo shule zitakuwa ndio zinaanza kwa mara ya kwanza matumizi ya kidigitali katika ufundishaji hivyo ziwe mfano bora kwa zingine ili ziweze kuvutika kutumia teknolojia hiyo.

Mragili alisema shule ambazo zimebahatika kupata vishikwambi hivyo ziwe mfano kutumia vifaa hivyo ili kuzivutia zingine kutumia teknolojia hiyo na shule zione umuhimu wa kuongeza vishikwambi zaidi kwani viwili ambavyo vimetolewa kwa kila shule havitoshelezi.

Amesema walimu lazima watambue kuwa mpango huu ulipoanzisha tayari tafiti zilifanyika na kuona kuna tatizo la elimu ya uzazi kwa vijana hivyo wahakikishe wanafundishwa ili waweze kujitambua na kupunguza maambukizi ya VVU.

Mkuu huyo wa Wilaya alisisitiza suala la itunzaji wa vishikwambi hivyo ili visaidie vijana wengine zaidi na kwamba kuvifabya kuwa mali ya shule sio kwamba utunzani uwe wa kulegalega.

Aidha,aliishukru serikali kwa kutoa vishikwambi kwa kutoonyesha ubaguzi ambapo vimetolewa kwa shule za serikali na binafsi kwa suala la elimu ya afya huwezi kubagua kati ya wanafunzi wanaosoma shule binafsi na za serikali.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida,Ester Chaula,amesema vishikwambi hivyo vitatolewa kwa walimu 270 waliopewa mafunzo ya namna ya kuvitumia na vitakuwa mali ya shule.

Amesema halmashauri yake imekuwa miongoni mwa Halmashauri 20 kati ya 184 zilizogawiwa vishikwambi hivyo ambapo shule za msingi 94 na sekondari 41 ndizo wanafunzi wake watafundishwa masomo ya uzazi wa mpango na jinsi ya kujikinga na maambukizi ya VVU.

Amesema Serikali imetoa vishikwambi hivyo ili kuweza kutoa elimu ya uzazi wa mpango na maambukizi ya VVU ili kufikia malengo ya mradi unaojulikana kama Timiza Malengo unaoendeshwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).