Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
SERIKALI mkoani Pwani, imetoa wiki mbili kukamatwa viongozi 24 ambao ni vinara wa utapeli ikiwemo mabalozi, wenyeviti wa Mitaa, watendaji walioshirikiana kuuza maeneo katika shamba namba 34 ambalo ni mali ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mitamba kata ya Pangani,Kibaha Mjini mkoani Pwani.
Aidha amewaagiza wataalamu wa Halmashauri ya Kibaha Mjini kupima na kuweka alama eneo hilo ndani ya siku 60.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge, alitoa maagizo hayo wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi wa shamba la Mitamba Kibaha ambalo lipo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kusimamiwa na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) .
Akitoa msimamo wa serikali kuhusu maamuzi ya eneo hilo alimuagiza Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani pamoja na Kamanda wa TAKUKURU Pwani kuwahoji watu hao na endapo watabainika kuhusika kuwa sehemu ya kutapeli wananchi sheria ichukue mkondo wake.
‘”Ninayo majina 24 ya viongozi na madalali waliohusika kuwauzia wananchi eneo hilo la shamba namba 34 kinyemela, wahojiwe na sheria ichukue mkondo wake,” Na nyie wananchi wenzangu mliouziwa viwanja katika eneo hili fungueni kesi dhidi ya waliowauzia na serikali itatoa ushirikiano” alifafanua Kunenge.
“Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Kibaha nakupa siku 60 anzeni kutekeleza maagizo kwa kupanga mji , baada ya hapo ambao watakuwa nje ya eneo la makazi watatakiwa kupisha ” aliongeza Kunenge.
Kunenge pia aliwataka wananchi walioendeleza maeneo yao katika kiwanja namba 34 kuondoa maendelezo yao ndani ya siku 14.
Mpimaji Ardhi Halmashauri ya Mji Kibaha, Aron Shushu, alieleza kiwanja hicho kimepimwa upya kwa kuzingatia sheria namba 8 ya mipango miji na mwaka 2021 kilifanyika kikao na wananchi hao kwa ajili ya kutoa katazo la kutovamia shamba hilo.
Awali Mwenyekiti Mtaa wa Lumumba, Gideon Tairo, aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano wakati wataalam watakapofika kupima eneo hilo.
Maagizo mengine ni Mkurugenzi na Wataalamu wa Mji ,kuhakikisha wanafanyia kazi upimaji wa awali ili kuonyesha maeneo ya kiwanja namba 34, maeneo ya Taasisi kazi ambayo inatakiwa kufanyika kabla ya kuwaondosha waliovamia.
Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilipewa shamba la hekta 4,000 na Wizara ilikubali kuipatia Halmashauri ya Mji wa Kibaha kiasi cha hekta 2,963 bila malipo yeyote na Wizara ikabaki na hetka 1,037. Pamoja na kugawa eneo hilo bado kuna watu wamevamia kile kipande kidogo kilichobaki.