Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kagera
Serikali imetoa Sh milioni 982 kwa Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) ili kukarabati barabara zilizoharibiwa na mvua za El-Nino zilizoanza kunyesha Septemba 2023 hadi sasa katika baadhi ya maeneo mkoani Kagera.
Akiwasilisha taarifa ya mpango kazi na bajeti ya shughuli za barabara kwa mwaka wa fedha 2024/2024, Meneja wa Tarura mkoani humo Avith Theodory amesema barabara nyingi zimeharibiwa na hivyo kukata mawasiliano kutoka kata moja hadi nyingine.
Amesema wakala huo unahudumia mtandao wa barabara mkoani Kagera kilometa 60,404 kati ya hizo kilometa 4,248 ni za udongo na ndizo zilizoathiliwa na mvua zaidi.
“Fedha iliyoletwa na serikali kukarabati barabara zilizopata athari za mvua ni awamu ya kwanza bado serikali itaendelea kuleta fedha nyingi tayari tumefanya tathimini na kubaini barabara ambazo zimepata athari kubwa na kuleta madhara na tumetangaza tunaamini ndani ya siku 10 barabara hizo zitakuwa zimeanza kufanyiwa ukarabati,”amesema Theodory.
Alitaja baadhi ya barabara ambazo zimeathiriwa zaidi na zinaenda kukarabatiwa haraka kuwa katika Wilaya ya Biharamulo barabara ya Mubaba, Mavota, Wilaya ya Karagwe Nyakagando, Kyota Wilaya ya Missenyi barabara ya Kagera Sugar-Bubale na barabara nyingine nyingi ambazo tayari zimetangazwa kuanza kukarabatiwa .
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatuma Mwasa kupitia kikao hicho aliwataka wakala huo kufanikisha ukarabati wa barabara hizo haraka ili kurudisha mawasiliano ya wananchi na kurahisisha shughuli zao katika swala la kusafirishaji wa mazao kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
TARURA Mkoa wa Kagera wamepitisha kiasi cha Sh bilioni 24 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za barabara kwa mwaka wa fedha 2024/2025