Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Same

Kamishna Jenerali Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Aretas Lyimo ametoa onyo kali kwa viongozi wa ngazi ya halmashauri  watakaobanika kutochukua hatua stahiki kuhusiana na kilimo cha mirungi, na kusema kuwa watachukuliwa hatua za kisheria bila kujali nafasi zao.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema hayo jana katika operesheni ya uteketezaji wa mashamba ya mirungi katika Kata ya Tae iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Same katika mkoa wa Kilimanjaro.

Alitoa rai kwa viongozi wa halmashauri kuanzia Afisa Tarafa mpaka Mwenyekiti wa Kitongoji kuwa ni wajibu wao kuhakikisha wanadhibiti uhalifu wa kilimo na matumizi ya mirungi, pamoja na kutoa elimu kuhusu athari ya matumizi yake katika maeneo wanayosimamia kulingana na sheria za nchi.

“Ni wajibu wa kila kiongozi katika halmashauri kuhakikisha anadhibiti matumizi ya mirungi, ikiwa ni pamoja na kukomesha kilimo chake kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu shughuli mbadala wanazoweza kuzifanya ikiwemo kilimo cha mazao mengine yenye tija. Pia, kwenda kwenye vyuo mbalimbali vya ufundi kupata ujuzi utakaowasaidia kwa namna moja au nyingine au kufanya biashara halali zitazokuwa chanzo cha mapato kwa ajili ya kujikimu na maisha wakiachana na biashara ya mirungi.”, Kamishna Jenarali Lyimo amesisitiza.

“Operesheni hii ni endelevu na tunatoa muda wa visiki vyote vilivyokatwa ving’olewe na mashamba yote ya mirungi yateketezwe mara moja, vinginevyo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa viongozi kuanzia tarafani mpaka kwenye vitongoji pamoja na wananchi wote wanaojishughulisha na kilimo haramu cha mirungi.”, Kamishna Jenerali Lyimo ameonya.

Akisisitiza kuwa ni wajibu wa kila mwananchi popote alipo kutojishughilisha na biashara ya mirungi na kutoa taarifa za kudhibiti uhalifu huo kwa mamlaka kwa kutumia namba maalum ambayo aliitoa kwa wananchi hao.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni ameagiza viongozi  wa Kata ya Tae kusimamia zoezi la ung’oaji wa visiki vyote na kutekekeza mashamba yote ambayo hayajafikiwa yateketezwe ndani ya kipindi cha mwezi mmoja. Hukua akiwataka wananchi kutojihusisha tena na kilimo cha mirungi, pamoja na kuwahimiza kujishughulisha na kilimo cha
mazao ya chakula.

Akizungumzia athari za matumizi ya mirungi, Kamishna wa Kinga na Tiba DCEA, Dkt. Peter Mfisi ameeleza kuwa matumizi ya mirungi yanachochea uhalifu ikiwemo ugomvi na mauaji kwa sababu ya kuathiri uwezo wa kufikiri, jambo linalosababisha mtu kuchukua maamuzi yoyote pasipo kutafakari matokeo yake na kusema kuwa baadhi ya maeneo ambayo kilimo cha mirungi
yamekithiri kuna changamoto kubwa wananchi wake kitabia.

Akitoa shukrani kwa mafunzo hayo, miongoni mwa wakazi wa Kata ya Tae ambayo ni miongoni mwa kata 35 za Wilaya ya Same, Happiness Yeremia ameishukuru Serikali kwa kuwapa elimu kuhusu mirungi na dawa za kulevya kwa ujumla kwa kuwa itawasaidia kuachana nazo, lakini pia akiomba uthibiti wa matumizi makubwa ya pombe.

Vilevile, mkazi mwingine wa Kata ya Tae, Elisante Semkondo amesema kuwa asilimia kubwa ya rika la vijana katika kata hiyo wanatumia mirungi kutokana na tabia ya kuiga. Hata hivyo,akisisitiza elimu waliyoipata imetoa hamasa kuchukua hatua ya kudhibiti changamoto hiyo na kuachana kabisa na kilimo cha zao hilo.

Aidha, Kamishna wa Huduma za Sheria DCEA, Veronica Matikila amesema Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya. Na. 15 ya Mwaka 2015 inakataza matumizi yote ya dawa za kulevya ikiwemo kulima au kutumia kwa kila Mtanzania. Hivyo yoyote anayejishughulisha kwa namna yyote na dawa za kulevya anakwenda ni kosa na atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Operesheni hiyo ya kutekeza mirungi katika mkoa wa Kilimanjaro ni hatua ya Serikali katika kuhakikisha inadhibiti na kutokomeza matumizi ya dawa ya kulevya, ambayo yamekuwa na athari katika ustawi wa jamii na maendeleo ya taifa kwa ujumla.