Na Georgina Misama – MAELEZO
Serikali kupitia Wizara ya Afya imetoa dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya Shilingi 216, 715, 516 kwa ajili ya kuhudumia wahanga wa mafuriko waliokusanyika kambi mbalimbali katika maeneo ya Rufiji na Kibiti mkoani Pwani pamoja na Mlimba Mkoa wa Morogoro.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Mobhare Matinyi amesema toka kutokea kwa mafuriko hayo Serikali kupitia Kamati ya Maafa imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kutembelea maeneo yaliyoathirika na kutoa maelekezo ili kuhakikisha wahanga wanapata huduma zote muhimu zikiwemo za afya.
“Katika hatua zilizochukuliwa kwa upande wa afya, serikali imesambaza dawa, vifaa na vifaa tiba, dawa za kusafisha maji kwenye familia na vyanzo vya maji ambapo hadi sasa tayari dawa na vifaa tiba vya thamani ya sh. 216 ,715, 516 vimeshapelekwa, vilevile katika kuimarisha huduma hizo wataalamu wa afya 20 wamepekwa ili kutoa chanjo kwa watoto; na kutoa huduma za msingi za matibabu kwa waathirika kwenye kambi hizo, kutoa huduma za afya akili, msaada wa kisaikolojia na kijamii kwa waathirika,” amesema Bw. Matinyi.
Amesema kwamba baada ya ziara ya viongozi wa Serikali wakiwemo Mawaziri na Makatibu Wakuu kamati ya Maafa ilikaa kikao tarehe 13 Aprili, 2024 ambapo Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameagiza Serikali ichukue hatua zinazostahili ili kukabiliana na hali hii ya mvua kubwa na mafuriko nchini ikiwemo Wakuu wa Wilaya na Mikoa kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ili kusimamia vema uratibu na uchukuaji wa tahadhari na uokoaji pale itakapobidi.
Matinyi amesema, Rais pia ametoa salamu za pole na rambirambi kwa Watanzania wote na wafiwa kufuatia vifo vilivyotokea katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo na Arusha ambako watoto saba waliokuwa wakienda Shule walipoteza maisha kutokana na ajali ya mvua hizi.
Katika hatua nyingine zinazochukuliwa na Serikali mpaka sasa mkoani Pwani na Morogoro ni pamoja na kutafuta na kuokoa watu na mali zao, jumla ya watu 2278 wameshaokolewa; kati ya hao, Morogoro ni watu 78 na Pwani watu 2,200 (Rufiji 1, 135 na Kibiti 1 ,065), kuanzisha kambi za muda kwa waathirika wa maafa ambapo kambi nane (8) zenye jumla ya watu 1529 zimeanzishwa kati ya hizo, kambi saba (7) zenye watu 1394 zipo mkoani Pwani na kambi moja (1) yenye watu 135 ipo Morogoro.
Aidha, Serikali imeendelea kupeleka misaada ya kibinadamu kwa wananchi ambapo chakula tani 40 za mahindi: vifaa vya malazi vikiwemo vyandarua 500; mablanketi 400; mahema 5 (mahema 4 Rufiji na moja (1) Kibiti ambapo kila hema linabeba wastani wa watu 70): pamoja na ndoo 300. Vilevile, tani 43 za unga na maharage tani 25 zipo njiani kuelekea Rufiji lakini pia kupeleka wataalamu kwa ajili ya kufanya tathmini ili kubaini kiwango cha maafa na hatua za kuchukua aidha, kazi hii inafanyika kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali.