Na Aziza Nangwa,JamhuriMedia,Iringa
SERIKALI imetoa agizo la kwa viongozi wa mamlaka za maji nchini kuvunjwa kwa kuta zilizojengwa mto Ruaha bila vibali na kunufaisha baadhi ya wananchi wachache.
Kauli hiyo imetolewa na kwenye Kongamano la Wahariri na Wadau wa Uhifadhi ,Mazingira na Utunzaji wa Vyanzo vya Maji mkoani Iringa na Makamu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Isdor Mpango.
Mpango amesema kuwa vita ya mazingira ni kubwa hivyo inahitaji ushirikiano kati ya Serikali, waandishi wa habari, wadau wa mazingira,vyama vya siasa, viongozi wa dini, taasisi, kampuni, mashirika pamoja na wananchi ili kuweza kufikia malengo.
Mpango amewataka viongozi wa mamlaka za maji kuchukua hatua za haraka kwa walioziba mto Ruaha Mkuu bila vibali kwani mto huo umekuwa tegemezi kwa mabwawa hivyo kitendo cha kujengwa kwa kuta hizo kunaathiri Watanzania wengi.
“Leo nimedhihirisha kumbe siwezi kupiga vita peke yangu, wala ofisi yangu, wala rais, wala waziri mkuu kwani peke yetu sisi hatuwezi .Mto Ruaha ni injini ya nchi kwa kuwa unapeleka maji kwenye mabwawa ya umeme hivyo Serikali haitakaa kimya kwa wale wanaochangia kusababisha mto huo kukauka.
“Kumbe leo nimeona waandishi ambao ni sawa na askari jasiri, timamu wa kuokoa mazingira na ni askari wazalendo pasipokuwa na shaka.Hili ni jambo letu na sisi tunayo nafasi ya kubadilisha mtazamo na matendo ya Watanzania kulinda na kuhifadhi mazingira ya nchi” amesema.
Mpango alikipongeza Kituo cha cha Wanahabaru Watetezi wa Rasilimali na Taarifa (MECIRA),kwa kusimamia suala la utoaji elimu wa masuala la mazingira nchini.
Amesema kuwa kwa takwimu zilizopo kiwango cha uharibifu kimeongeza kwa asilimia 42 kutoka mwaka 1980 kwenda asilimia 50 hadi mwaka 2012.
“Tangu mwaka 2018 kwa asilimia 63 mazingira yetu tumeshaharibu, inatisha hii ndugu zangu na hii inasababishwa na tabia watu kukata miti hovyo, kuchoma misitu, uvamizi na uhabifu misitu,kuharibu vyanzo vya maji, uvuvi haramu, kutupa takata hovyo.
Ameongeza kuwa kutokana na matendo hayo kumechangia kuwepo kwa mabadiliko ya tabia nchi kwa kuwepo kwa ukame ambapo pia hivi sasa mvua hazitabiriki lakini pia mabadiliko ya tabia nchi yameleta magonjwa ya binadamu, wanyama, magonjwa mimea na baadhi ya mazingira ya sili yanapotea.
“Sisi wote tumechangia kuwepo kwa mabadiliko ya tabia nchi na hili kundi la viongozi ambao nao wamekuwa na maslahi binafsi kwa kuchangia uharibifu wa mazingira.
‘Mimi siamini kwamba wale wanaoswaga ng’ombe ndio wenye ng’ombe 3000 na kuendelea, wala wakulima wetu wale ninao wajua ndio wenye matrekta wanaoziba mito yote na kupeleka maji kwenye mashamba yao.
‘Viongozi wa namna hiyo ndio ninaosema wanywe sumu kwa kuwa wamekuwa na maslahi yao binafsi na kuchangia uharibifu wa mazingira yetu nchini kwa kufanya hivyo itasaidia kunusuru mito yote husuani mito ya mkakati kama Ruaha.Tumesharibu sana mazingira na sasa yalipa kisasi na sasa tumeanza kulipata jeuri yetu,” amesema.
Mpango amesema kuwa hatuwezi kuacha tabia hii kuendelea kwani madhara kwa jamii ni makubwa zaidi ili tuweze kufanikiwa katika zoezi hili ni lazima kushirikiana na kuwa na jitihada za pamoja kutoka Serikalini,taasisi za Serikali, vyama vya siasa, taasisi za dini, sekta binafsi, vyombo vya habari, wadau wote na jamii wote mijini na vijijini.
Ameongeza kuwa Sera ya Mazingira, ilitoa mwongozo kuhusu vyanzo vya maji na mazingira Novemba 16, alizindua kampeni ya kupanda miti Mbeya na kuwataka wakuu wa mikoa kusimamia suala hilo hivyo ni vyema kukawa na jitihada za kila mkoa kupanda miti rafiki wa maji katika mikoa yote nchini ambapo itaweza kusaidia suala la uharibifu wa mazingira.
“Nisisitize kuwa bonde la Ihefu lina utajiri mkubwa sana kwani inalinda na kuhifadhi viumbe hai, ardhi na sura ya nchi na lakini pia uhakika wa kupatikana maji kwa shughuli za jamii na shughuli jamii hivyo ni mhimili katika bwawa la Mtera, Kidatu, Usangu na Rufiji sasa tumeona uhaibifu mkubwa katika bonde la Ruaha hivyo ni lazima kulindwa kwa nguvu zote,” amesema.
“Viongozi walio Serikalini wanaowalinda watu wanaoharibu mazingira kwa kuchepusha maji na kuingiza mifugo maeneo ya hifadhi hawatufai” amesema Dkt. Mpango.
Aidha ametoa wito kwa waandishi wa habari na wahariri kutumia kalamu zao na vyombo vyao kuelimisha jamii kwa kuandika habari za uchunguzi ambazo zina ukweli kuhusiana na uharibifu wa mazingira na si kuficha watu.
“Wahariri na waandishi wa habari muache kuchukua rushwa andikeni ukweli bila kuogopa nawaomba muandae makala maalum na irushwe Watanzania wote waone.Waandishi wahabri ni moja ya nguzo muhimu katika uendeshaji wa taifa lolote na kama nyinyi mkiamua kufanya kampeni jamii iende katika maeneo fulani inakuwa hivyo hivyo.
“Kwa sababu hiyo waandishi waendelee kutumia ushahiwishi wenu kuhusu utunzaji wa mazingira.Kutokana na nguvu kubwa katika kuhamasisha jamii hivyo taasisi zote kushirikiana na waandishi wa habari ili katika kukabiliana uharibifu wa mazingira,’ amesema.
Hata hivyo amtaka katibu mkuu kwenda kujenga hoja katika Wizara ya Fedha ili kuwepo kwa fungu ambalo litasaidia katika kuwaunga mkono hivyo waziri mwenye dhamana asimamie hilo.