KATIKA bajeti ya mwaka 2025/2026, serikali imetenga Sh bilioni 5.5 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 54 za walimu nchi nzima.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi, Zainab Katimba alisema nyumba hizo ni mbili kwa moja na zitajengwa katika maeneo yenye uhaba wa nyumba za kuishi.
Katimba alikuwa akijibu swali la Msingi la Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli (CCM) aliyeuliza, “Je, serikali ina mpango upi wa kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu hususani kuwajengea nyumba za kuishi”.
Katimba alisema Sh bilioni 14.82 imepokelewa kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya nyumba za walimu 741 katika mwaka wa fedha 2024/2025.
Alisema katika mwaka 2024/2025, serikali imetoa Sh bilioni 13.79 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu 263 katika shule za msingi nchini.
Naibu Waziri huyo alisema: “Mpango wa serikali ni kuendelea kutenga fedha za kujenga na kufanya ukamilishaji wa maboma yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi kwa kutoa kipaumbele kwenye maeneo yenye uhitaji mkubwa kadiri ya upatikanaji wa fedha”.
Katika swali la nyongeza mbunge huyo alitaka kufahamu katika nyumba hizo 54 zitakazojengwa katika mwaka ujao wa fedha, jimbo la Segerea litapata nyumba ngapi.
Pia, alihoji watumishi wanaodai malimbikizo watalipwa lini.
Akijibu yote hayo, Katimba alisema fedha zitakapoanza kutolewa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hizo, jimbo la Segerea litapata kipaumbele, lipate nyumba hizo.
Kuhusu malimbikizo ya watumishi, Katimba alisema, “Natoa maelekezo kwa wakurugenzi wote wa mamlaka za serikali za mitaa watengeneze mchanganuo na kubaini watumishi wangapi wanadai malimbikizo ya mishahara na isiyo ya mishahara na wapeleke hazina kwa ajili ya malipo”.
“Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma jana (juzi) imetoa hadi muda hadi Mei 31 halmashauri zote wakamilishe orodha ya watumishi wanaodai na zipeleke kwao”.
