Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi katika mwaka wa fedha 2023/24 imetenga Shilingi bilioni 15.77 kwa ajili ya Bajeti ya matumizi ya kawaida ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Fedha hizo, Shilingi bilioni 15.31 ni Bajeti ya Mishahara na Shilingi milioni 464.23 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo huku bajeti ya maendeleo kwa ajili ya mradi wa Rada, Vifaa na Miundombinu ya hali ya hewa katika mwaka 2023/24 ni Shilingi bilioni 13.
Akiwasilisha Bungeni Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Mwaka wa fedha 2023/24 leo tarehe 22/5/2023, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa, amesema kuwa fedha hizo zitatumika kukamilisha malipo ya mwisho ya Rada mbili (2) za hali ya hewa zitakazofungwa Dodoma na Kilimanjaro pamoja na kukamilisha miundombinu yake.
Prof. Mbarawa amesema kuwa pia fedha hizo zitatumika kununuzi wa Rada mbili (2) za uangazi wa hali ya hewa baharini pamoja na ujenzi wa miundombinu yake.
Amesema kuwa TMA imeendelea kutoa, kusimamia, kudhibiti na kuratibu utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini kwa ufanisi mkubwa.
Pia imeendelea kutoa tahadhari kuhusiana na hali mbaya ya hewa, kufanya tafiti za kisayansi za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, kubadilishana taarifa za hali ya hewa katika mtandao wa dunia (Global Telecommunication System – GTS) kulingana na makubaliano ya Kimataifa pamoja na kuiwakilisha nchi katika masuala ya hali ya hewa Kikanda na Kimataifa.
Amebainisha kuwa imeendelea kutoa huduma za utabiri wa hali ya hewa wa kila siku, siku kumi na ule wa muda mrefu pamoja na tahadhari ya matukio ya hali mbaya ya hewa na kusambaza kwa wananchi ili kuhakikisha usalama wa watu na mali zao pamoja na kuchangia katika kuimarisha utendaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii.
“Usahihi wa utabiri wa hali ya hewa unaotolewa na TMA kwa sasa umefikia asilimia 94 ambao ni juu ya asilimia 70 ya kiwango cha usahihi kinachokubalika na Shirika la Hali ya Hewa Duniani” amesema Prof. Mbarawa.
Amesema kuwa usahihi wa utabiri umechangiwa kwa kiasi kikubwa na uboreshaji wa miundombinu na huduma za hali ya hewa ikiwemo ununuzi wa vifaa na mitambo ya kisasa ya hali ya hewa.
Prof. Mbarawa amesema kuwa serikali imeendelea kutekeleza mradi wa kununua na kufunga Rada nne (4) za hali ya hewa. Rada mbili (2) tayari zimeshapokelewa na kazi ya ufungaji wa rada hizo inaendelea katika mikoa ya Mbeya na Kigoma na Rada nyingine mbilI.
“TMA imeendelea kuiwakilisha Tanzania Kikanda na Kimataifa katika masuala ya hali ya hewa. Mamlaka ilishiriki katika mikutano 56 ikiwemo mkutano wa 15 wa watumiaji wa data na huduma zitolewazo na Shirika la EUMETSAT Barani Afrika, uliofanyika Dar es Salaam” amesema Prof. Mbarawa.
Ameeleza kuwa watumishi 18 wa TMA walishiriki katika semina 25 za mafunzo ya hali ya hewa na hivyo kujenga uwezo wa utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini.