Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ( DCEA), imeteketeza jumla ya hekari 101 za mashamba ya bangi sawa na kiasi ya kilo 550 za bangi mbichi pamoja na magunia 482 ya aina hiyo ya dawa za kulevya katika eneo la Kisimiri juu kata ya Uwalu, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.
Ukamataji huo umefanyika kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kufanya operesheni nchi nzima ili kuhakikisha dawa za kulevya zinatokomezwa Nchini.
Akizungumza operesheni hiyo, iliyoanza Mei 31, 2023 mkoani humo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo amesema, Mamlaka kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Usalama itaendelea kufanya operesheni za mara kwa mara katika maeneo haya ili kuhakikisha bangi inatokomea kabisa mkoani humo na hatimaye wakulima na wananchi kwa ujumla wanaoishi katika eneo ya kisimiri juu na chini wanaachana na kilimo cha bangi na kujikita katika mazao mengine ya biashara badala ya bangi.
Kamishna Lyimo amesema kuwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) katika kuhakikisha agizo la Mheshimiwa Rais ilinatekelezwa, ameelekeza kufanyika kwa utafiti kujua ni mazao gani mbadala yanaweza kulimwa katika maeneo haya ambayo yamekithili kwa kilimo cha dawa za kulevya, ili wananchi wa maeneo husika waweze kupewa mbinu mbadala za kulima mazao mbalimbali ya chakula na biashara badala ya kuendelea na kilimo cha bangi.
“Tumewasiliana na Wizara ya Kilimo na Afisa kilimo wa kata ya Uwalu hapa kisimiri ambaye ameeleza tayari utafiti huo umefanyika.
Aidha,katika kuhakikisha wananchi wanoishi katika maeneo yaliyokithiri kwa kilimo cha dawa za kulevya hususani bangi na mirungi,wanapata elimu juu ya athari za biashara na matumizi ya dawa hizo,elimu juu ya tatizo hilo itatolewa kupitia shule za msingi na sekondari.
Hii inafanyika kufuatia agizo la Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mheshimiwa Jenista Mhagama (Mb) kuitaka Mamlaka kushirikiana na wadau kutoa elimu katika maeno hayo.
Ambapo tayari maafisa elimu kata wameanza kutoa elimu kwa wanafunzi, ili baadaye wasijihusishe na kilimo cha bangi na mirungi badala yake wajikite kwenye mazao mengine.
Naye Afisa kilimo Kata ya Uwelu, Samwel Parangyo, amesema kuwa, utafiti uliofanywa na wizara ya Kilimo kupitia kituo cha utafiti wa kilimo cha TARI Tenguru, ilionekana mazao kama pareto, karoti na viazi mviringo yanaweza kustawi katika maeneo haya na kuwa mbadala wa zao haramu la bangi ambalo halifai katika jamii yatu. Ameiomba Serikali kuangalia namna ya kuwawezesha wananchi wa maeneo hayo kwa kutoa ruzuku ya mazao hayo.
Kwa upande wa elimu, Afisa elimu wa kata hiyo Gilbert Kavishe amesema kuwa, tutaanza kutoa elimu kwa wanafunzi wetu ili wanapokuwa wakubwa waachane na kilimo cha bangi, tutatumia mikutano ya wazazi na wadau wengine kuhamasisha jamii kuachana na kilimo cha bangi kwani kina madhara makubwa ikiwemo kudhorotesha kiwango cha elimu katika jamii yetu.
Operesheni hii imefanyika ikiwa ni siku moja baada ya Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mheshimiwa Jenista Mhagama (Mb) kutoa taarifa ya hali ya dawa za kulevya nchini kwa mwaka 2022 ambapo katika taarifa hiyo alitaaja mikoa inayojihusisha na kilimo cha Bangi kwa kiasi kikubwa, Mkoa wa Arusha Ukiwa kinara ukifuatiwa na Mikoa na Iringa, Morogoro na Manyara.