Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amesema Serikali itaanza Mpango wa Utoaji wa Chanjo na utambuzi wa Mifugo Kitaifa kuanzia Mwezi Januari 2025 ambapo Shilingi Bilioni 28.1 zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza mpango huo.
Amesema lenga ni kudhibiti na kutokomeza magonjwa ya mifugo nchini na kwamba mpango huo utatekelezwa kwa miaka mitano kutoka 2024-2029 na kugharimu Shilingi Bilioni 216 zitakazotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo Shilingi Bilioni 28.1 zitatumika awamu ya kwanza ya uchanjaji na utambuzi wa mifugo kuanzia Mwezi Januari 2025.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa Kampeni ya Chanjo za Mifugo Kitaifa uliofanyika ukumbi wa Jakaya Kikwete leo Desemba 18, 2024 jijini Dodoma, Waziri huyo wa Mifugo na Uvuvi amesema, katika kufanikisha zoezi la chanjo ya mifugo serikali itachangia nusu bei ya gharama za chanjo ili kuwarahisishia wafugaji kuchanja mifugo yao.
“Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kuwa Serikali itachangia nusu ya bei kwa ajili ya chanjo kwa mifugo ambapo kwa upande wa Ng’ombe itachangia Shilingi 500, kwa upande wa mbuzi na kondoo itachangia Shilingi 300 na upande wa kuku itakchangia Shilingi 100 itakuwa sawa na bure” amesema Dkt. Kijaji.
Aidha ametumia nafasi hiyo kuwataka viongozi wa mamlaka ya serikali za mitaa, manispaa na majiji kutoa ushirikiano kwenye kampeni hiyo ya chanjo na kisha kueleza umuhimu wa chanjo za mifugo kwa taifa na wananchi kwa ujumla.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amesema Zoezi hilo la chanjo litahusisha wataalam na wafugaji katika kufanikisha hilo hivyo amewaomba wataalam na wafugaji kutoa ushirikiano wa zoezi hilo .
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Taifa CCWT Mrida Mshota amesema zoezi la chanjo linalokuja kwa awamu hii litawasaidia mafugaji hasa kukabiliana na ugonjwa wa mifugo na kuiomba Wizara kuupa kipaumbele pia ugongwa wa Miguu na midomo (FMD) .
Aidha, ameishukuru serikali kwa kuonyesha dhamira ya dhati ya kuboresha sekta ya mifugo kupitia hatua hizi za chanjo, na kuahidi ushirikiano wa karibu kutoka kwa wafugaji katika utekelezaji wa zoezi hilo.