Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
SERIKALI imesema itaanza kuwashughulikia watumishi wake wanaoshukiwa kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja na kueleza kuwa tabia hiyo ni kinyume na maadili ya kitanzania na kwamba inavuruga mfumo mzima wa maadili ya utumishi wa Umma.
Hatua hii imekuja kufuatia kuwepo kwa malalamkiko kwamba kuna viashiria hivyo kwenye baadhi ya Taasisi za serikali jambo linalotoa taswira mbaya kwa jamii na kusababisha baadhi ya huduma kushindwa kutolewa ipasavyo.
Hayo yamezungumzwa leo Oktoba 17,2024 jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi,wakati akifungua kikao kazi cha kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na utawala bora baina ya taasisi simamizi za maadili ya utendaji na mamlaka simamizi za maadili ya kitaluma.
Amesema msimamo wa nchi upo bayana kwamba vitendo hivyo havina nafasi na hivyo kuwataka wana jamii kuendelea kushirikiana na Serikali kukemea kwa nguvu zote.
“Lazima tuwe wakweli kwenye hili ,Serikali ilishaweka msimamo wake kuhusu mapenzi ya jinsia moja,suala hili tulikemee kwa sauti moja ili kuwa na jamii inayozungumza lugha moja ya maadili ya kiafrika yenye miiko yake,” ameeleza.
Mbali na jambo hilo ametumia nafasi hiyo kukemea vikali ukiukwaji wa maadili kwa watumishi wa umma ikiwemo mmomonyoko wa maadili na mavazi yasiyofaa kwa watumishi wa umma jambo ambalo limekuwa likichafua taswira ya serikali.
“Ofisi imeanza kupokea tuhuma na malalamiko kuhusu kuwepo kwa viashiria vya mmomonyoko wa Maadili kinyume na mila na desturi za nchi yetu vinavyohusu vitendo vya mapenzi ya jinsia moja kwa baadhi ya watumishi wa umma,vitendo hivyo ni miongoni mwa vitendo vya kijinai kwa mujibu wa sheria za nchi lakini pia ni vitendo vya kinyume na maadili kwa mujibu wa miongozo ya utumishi wa umma, “anasisitiza .
Pia amewataka washiriki wa kutumia kikao kazi hicho kujadili na kubadilishana uzoefu ili kuja na mapendekezo ya namna sahihi ya kudhibiti vitendo hivi na namna sahihi ya kushughulikia masuala hayo yatakapojitokeza katika maeneo ya kazi kwa baadhi ya watumishi wanaohusishwa navyo.
Amesema hali hiyo itasaidia kuepuka kuchafua taswira ya utumishi wa umma kwa ujumla huku akiweka msisitizo kwa Taasisi za dini nchini kusimama kidete kukemea na kuonya vitendo hivyo vya ndoa ya jinsia moja katika jamii ya kitanzania mana wao wana nguvu na Sauti kubwa ya kusikika zaidi.
Naibu Katibu Mkuu huyo ameeleza kuwa,”Hivi sasa zipo nchi zimeacha kuzaliana kutokana na kushamiri kwa vitendo hivyo vya mapenzi ya jinsia moja,sisi hatutaki kufika huko ,na kwa watumishi kila mmoja akemee mavazi yasiofaa kwa kutumia waraka namba 6 wa utumishi wa umma unaozungumzia mavazi kuchukua hatua dhidi ya watumishi wanaochafua taswira ya serikali kwa kuvaa hovyo ndani na nje ya utumishi, “amesema
Kutokana na hayo Kaimu Mkurugenzi Idara ya Usimamizi wa Maadili,Ally Abdul Ngowo,
amesema wanatarajia kupokea taarifa ya utendaji kazi kwa kipindi cha Septemba 2023 hadi Septemba 2024 katika maeneo yao kuhusu suala la maadili na kwamba kupitia kikao kazi hicho watajadili namna ya kuondokana na suala la uvunjifu wa maadili.
Amesema imekuwa ni changamoto kubwa na kwamba wataanza kulifanyia kazi kwa kuwa wameshapokea malalamkiko mengi kuhusu viashiria hivyo na kufafanua kuwa kikao hicho kitatoa maazimiao kwa kuhakikisha wanaanza kuwachukulia hatua za awali kabla ya kuajiri watumishi.
“Kuwepo na taarifa za malalamiko mengi kutoka vyanzo mbalimbali, yatokanayo na vitendo hivyo vinavyoshusha utendaji na maadili ya kitaaluma katika utumishi wa umma, tutachukua hatua za awali kabla ya kuajiri watumishi ili kumaliza tatizo hili, ” amesisitiza.
Pia amesema wataona namna ya kuanza kutoa msaada wa Saikolojia kwa watumishi wenye viashiria hivyo ikiwa watahitaji kutokana na kutambua kuwa baadhi yao wamejiingiza kwenye tabia hiyo kwa kutokupenda na wapo tayari kubadilika .
“Tunapokea malalamiko mengi yakiwahusisha baadhi ya watumishi wetu wa umma kutoka kada mbalimbali kama Wauguzi, Madaktari, Waalimu, Maafisa Utumishi, Maafisa Ardhi, Wahasibu katika Halmashauri, Wataalam waliopo Sekta ya Ugavi wa Umeme, na Maji, pamoja na Wahandisi wanaosimamia miradi ya maendeleo. “ameeleza na kuongeza kuwa;
Msaada wa Saikolojia utaweza kusaidia kujitambua na kuelewa kwamba wanachokifanya si sahihi na kuwa tayari kupokea mabadiliko, ” ameeleza