Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imesema inatambua mchango wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) hususan katika hifadhi ya mazingira nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira, Dkt. Selemani Jafo amesema hayo jijini Dodoma leo tarehe 28 Juni, 2024 wakati akizungumza na Mwakilishi Mkazi wa WFP Bi. Sarah Gordon-Gibson aliyefika ofisini kwake kumuaga baada ya kumaliza muda wake nchini.
Katika mazungumzo hayo, Waziri Dkt. Jafo amemshukuru kwa ushirikiano wake aliokuwa anauonesha kwa Ofisi ya Makamu wa Rais na Serikali kwa ujumla wakati wa utendaji wake.
Amesema kuwa Ofisi itaendelea kumkumbuka kwa utendaji na mchango wake tangu ateuliwe kuwa mwakilishi mkazi wa shirika hilo kwa vipindi viwili mfululizo hapa nchini.
Ametumia nafasi hiyo kumpongeza Bi. Sarah kwa mchango wa WFP katika ajenda ya kukuza kilimo nchini ya 10/30 kupitia miradi wanayoanzisha ambayo inalenga kuimarisha uchumi kupitia sekta hiyo
Waziri Dkt. Jafo amemuelezea mwakilishi mkazi huyo kuwa ni mchapakazi na ni mtu mwenye kutoa ushirikiano kwa jamii, Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na Serikali kwa ujumla.
“Dada yangu Sarah pamoja na kuwa umemaliza muda wako na unaondoka hapa nchini, nasi tunamkaribisha kwa moyo wote mrithi wako atakayekuja na tuna imani kuwa ataendeleza mazuri yote uliyofanya hasa katika sekta hii ya mazingira,“ amesema Dkt. Jafo.
Halikadhalika, Waziri Jafo amemuomba afikishe salamu kwa viongozi kule makao makuu ya WFP jijini Paris nchini Ufaransa na kwa mwakilishi mkazi atakayechukua nafasi yake.
Kwa upande wake Bi. Sarah ambaye amehamishiwa nchini Chad kikazi ameahidi kuwa shirika hilo litaendeleza uhusiano zaidi na Serikali ya Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo ya mazingira.
Pamoja na hayo pia ameomba apewe ushirikiano kwa mwakilishi mkazi mpya atakayechukua nafasi yake ili kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika usalama wa chakula.
“Nawashukuru pia kwa ushirikiano wenu Ofisi ya Makamu wa Rais kwangu na kwa shirika kwa ujumla, hiyo fursa kwetu kuendelea kuudumisha ushirikiano huo, viongozi watakuja na kuondoa lakini WFP itaendelea kufanya kazi na kila mmoja,“ amesema.
Itakumbukwa kuwa kabla ya kuwa mwakilishi mkazi wa WFP nchini Tanzania, Bi. Sarah amewahi kufanya kazi katika nchi mbalimbali zikiwemo Morocco, Mauritania na Niger.