Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametangaza mikakati ya serikali bungeni inayolenga kuimarisha ulinzi na usalama wa makundi ya watu wenye ulemavu na ualbino nchini.
Akitoa tamko la serikali leo Juni 20, ikiwa ni siku chache tangu mtoto mwenye ualbino auawe kikatili huko Muleba mkoani Kagera, Majaliwa amesema mikakati muhimu ya Serikali inahusu kulinda haki za watu hao na itatekelezwa ili kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi yao.
Jeshi la Polisi limesema jana kuwa linawashikilia watu tisa akiwemo Baba mzazi na paroko msaidizi kwa tuhuma za mauaji ya mtoto mwenye ualbino Asimwe Novart (2) wa kijiji cha Bulamula wilaya ya Muleba mkoani Kagera.
Baba mzazi wa mtoto huyo, Novart Venant, mganga wa jadi na mkazi wa Nyakahama, Desideli Evarist, Paroko Msaidizi wa Parokia ya Bugandika, Elipidius Rwegoshora wamekamatwa pamoja na watuhumiwa wengine Danstan Kaiza mkazi wa Bushagara, Faswiru Athuman , Gozibert Alkadi, Rwenyagira Burkadi, Ramadhani Selestine na Nurduni wote wakazi wa Nyakahama, Kamachumu.
Waziri Mkuu ameagiza Jeshi la Polisi kuharakisha uchunguzi na kuwapeleka watuhumiwa wote mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Hatua zinazochukuliwa
Hata hivyo amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali za kisheria na kitaasisi kuhakikisha ulinzi na usalama wa makundi mbalimbali katika jamii, ikiwa ni pamoja na watu wenye ualbino.
“Mikakati hiyo inahusisha ushirikiano na wadau wa maendeleo, mashirika yasiyo ya kiserikali, na jamii kwa ujumla,” amesema Waziri Mkuu.
Alitaja kuwa Sheria ya Kanuni ya Adhabu inatumika kukabiliana na matendo kama vile utekaji, unyanyasaji, au mauaji. Pia, kuna mifumo ya kutoa adhabu kali kwa wahusika wa vitendo hivi.
Kuhusu mikakati, Waziri Mkuu amesema mipango iliyobuniwa na inayotekelezwa ni pamoja na kuanzisha mifumo ya taarifa jumuishi na kamati za ulinzi wa wanawake na watoto.
Majaliwa aliwataka wananchi na viongozi wa kila sehemu ya jamii kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji kwa watu wenye ualbino.
Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa pamoja katika kuhakikisha ulinzi wa haki za binadamu kwa wote.
Vile vile alisema serikali sasa inaandaa Mpango wa Kuzuia Ukatili dhidi ya Watu wenye Ualbino (NAP) kwa kushirikiana na Chama cha Watu wenye Ualbino (TAS) na Wadau; pia inakusudia kuandaa kikao cha Wakuu wa Mikoa wote Tanzania Bara kitakachofanyika Julai 3, 2024 kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya ulinzi wa watu wenye ualbino.
Mpango mwingine ni kuendelea kutoa elimu ya ukatili dhidi ya Watu wenye Ulemavu wakiwemo Watu wenye Ualbino kupitia Maafisa Ustawi wa Jamii, Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Elimu Maalum wa Mikoa yote nchini.
“Serikali itafanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2004 na kuandaliwa kwa Mkakati wake wa Utekelezaji wa Miaka Mitano (National Five Year Implementation Strategy 2024/2025- 2029/2030) na Mkakati wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Miaka Mitano ambayo itazinduliwa mwaka ujao wa fedha 2024/2025,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa bungeni.
Eneo jingine kwa mujibu wa Majaliwa ni kukamilisha na kuzindua Mkakati wa miaka mitatu 2024-2027 wa Upatikanaji wa Teknolojia saidizi kwa Watu wenye Ulemavu wakiwemo watu wenye Ualbino, mkakati huu umepangwa kuzinduliwa mwezi Julai, 2024.
Pia kuandaa na kukamilisha Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Watu wenye Ulemavu 2024/2025 – 2026/2027 na kuendelea na ubainishaji na usajili wa watu wenye ulemavu ngazi za kijiji na mtaa kwa kutumia Mfumo wa Kielektroniki na Kanzidata ya Watu wenye Ulemavu.