Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia, Mafia
SERIKALI imeagiza mara moja kusitishwa kwa shughuli za wananchi katika eneo la mto Maleta, kwa kuwa ni eneo la Uhifadhi wa bahari na ni chanzo cha maji na mazalia ya samaki pia ni sehemu ambapo mto unamwaga maji baharini.
Akitoa Maagizo mbalimbali ya Baraza la Mawaziri ambalo Mwenyekiti wake ni Rais ,yaliyotokana na mapendekezo ya kamati ya mawaziri nane wa kisekta pamoja na wataalamu waliopita kwenye maeneo ya migogoro ,Mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge aliutaka uongozi wa Wilaya ya Mafia kusimamia utekelezaji wa agizo hilo.
Aidha , Serikali imeagiza Mwekezaji Chole Mjini Conservation and development company Ltd , Kitongoji Cha Mnyange, kisiwa cha Chole ,asiruhisiwe kubadili hati yake ya kumiliki Magofu ya Kale , ifikapo april 2027 hadi hapo atakapofuata utaratibu unaotakiwa kisheria.
Kunenge alifafanua, mchakato wa upatikanaji wa umiliki wake haukufuata utaratibu na kusababisha Serikali kuikoseshea mapato Serikali yanayotokana na malekale hizo.
Alimtaka Kamishna Msaidizi wa ardhi mkoa na Mkurugenzi Mafia kuhakikisha wanasimamia agizo hilo .
“Sehemu ya kisiwa cha Chole katika Kitongoji cha Mnyange kina Magofu ya Kale ambayo yamemilikishwa kwa Mwekezaji huyo,na Serikali imekuwa haipati mapato yanayotokana na matumizi ya malekale hizo, “hatoruhusiwa kurenew hati yake inayokoma april 2027 kwakuwa mchakato wa awali haukufuata utaratibu”anasema Kunenge.
Vilevile, idara ya Malekale iandikiwe barua ili iende kutambua malekale zilizopo Mafia na kuziweka chini ya usimamizi.
Mkuu huyo wa mkoa ,aliutaka uongozi wa wilaya kuhakikisha wawekezaji wanakumbushwa umuhimu wa kufuata sheria za nchi na kuzingatia matumizi endelevu ya raslimali bahari na nchi kavu.
Kunenge alitaja maagizo mengine kuwa ni, Kamishna Msaidizi wa ardhi mkoa wa Pwani , Halmashauri, Wakala wa misitu TFS ,Marine Park na Serikali za vijiji kuweka alama za kudumu katika maeneo ya uhifadhi yaliyoainishwa ili kuepusha uvamizi wa maeneo hayo.
“Marine Park kwa kushirikiana na Uongozi wa wilaya kuimarisha doria maeneo ya uhifadhi wa bahari na nchi kavu kwenye maeneo ambayo kisheria wana wajibu wa kuyasimamia.:”
Kunenge alimuelekeza ,Katibu Tawala mkoa apeleke barua kukumbushia Mamlaka zinazohusika hasa kitengo cha hifadhi ya bahari kuhamishiwa wizara ya maliasili na utalii.
Pamoja na hayo , Kunenge alieleza mgao wa maduhuli upelekwe kwenye vijiji husika katika hifadhi ya bahari na usimamiwe na hifadhi ya bahari ya Mafia badala ya Halmashauri ambayo ina majukumu mengine mengi ya kuyasimamia.
“Dhamira ya Serikali ni kubadilisha maisha ya wananchi wa kisiwa cha Chole na Mafia kupitia uchumi wa bluu na kilimo cha Mwani, Nazi,korosho,miwa ili kujiongezea maendeleo” anasisitiza Kunenge.
Awali Mkuu wa wilaya ya Mafia, Zephania Sumaye alieleza , Changamoto kubwa Mafia ni uharibifu katika hifadhi ya bahari.
Zephania alieleza kwamba , wananchi wamekuwa wakivamia maeneo ya Hifadhi hasa maeneo tengefu kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kilimo,uvuvi,ukataji miti na mkaa.
Eneo la Uhifadhi wa bahari Mafia una ukubwa wa km za mraba 822 ,zilizopo baharini na nchi kavu katika vijiji 12 na vitongoji vitano ambavyo vimezungukwa na hifadhi ya bahari inayojumuisha eneo tengefu.