Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo imewaonya baadhi ya Watanzania ambao wamekuwa na tabia ya kuzipokea na kuzishangilia timu ngeni zinapokuja kucheza na timu za Tanzania kuacha tabia hiyo kwani inarudisha nyuma juhudi kubwa za Rais Dk Samia Suluhu katika juhudi za kuendeleza michezo nchini.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Damas Ndumbaro jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa mtandao mpya wa Simba SC uliopewa jina la “Simba Executive Network” ambao una lengo kukusanya fedha kwa ajili ya kuendeleza miundombinu ya klabu hiyo.
Dk Ndumbaro amewaomba Watanzania waziunge mkono timu za Simba na Yanga kwa kuwa ushindi wa timu hizo utaleta heshima kwa nchi, mpira wa Tanzania na timu zinazoshiriki.
“Natamani kuziona timu zote nusu fainali, inaleta heshima kwa nchi, inaleta heshima kwa mpira wetu na vilabu vyetu”-amesisitiza Dk Ndumbaro
Amesema Serikali haifurahishwi na tabia ya baadhi ya Watanzania ambao huwafanya wageni wajisikie nyumbani wanapokuja kucheza hapa nchini huku wakiibeza timu ya Tanzania jambo ambalo halina faida kwa maendeleo ya soka.