Na Daniel Limbe, JammhuriMedia, Chato

SERIKALI imewataka wananchi kutumia demokrasia yao kuwachagua viongozi bora watakao kuwa tayari kutatua changamoto za jamii badala ya kuwaachia watu wengine kufanya maamuzi ambayo hayana tija kwa umma.

Kauli hiyo imetolewa kwa nyakati tofauti na mkuu wa wilaya ya Chato mkoani Geita,Louis Bura,baada ya kutembelea kata ya Bwongera,Muganza,Kigongo na Nyamirembe kwa lengo la kuhamasisha jamii kujitokeza kwa wingi kusikiliza sera za wagombea mbalimbali wa vyama vya siasa hatua itakayowasaidia kufanya maamuzi sahihi.

Mkuu wa wilaya ya Chato,Louis Bura, akizungumza na wananchi

“Nimekuja kuzungumza nanyi ili wale wote mliojiandikisha kwenye daftari la mkazi mkajitokeze kwa wingi kwenye mikutano ya wagombea wa vyama vyote kusikiliza sera zao ili iwasaidie Novemba 27, 2024 kuchagua viongozi bora”

“Serikali inaanza na viongozi wa vitongoji pamoja na vijiji, maana hao ndiyo kimbilio la kwanza la wananchi waliopo huku chini,serikali inatekeleza miradi mingi ya maendeleo na viongozi hao ndiyo wanakuwa mstari wa mbele kuelekeza maeneo ya kuweka miradi hiyo,na hao ndiyo wanaoandika barua zenu za dhamana kwenda polisi na mahakamani, kwa hiyo hao ni viongozi muhimu sana” amesema Bura.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya hiyo, jumla ya wananchi 236,000 walijiandikisha kwenye daftari la mkazi sawa na aslimia 85 ya lengo la kuandikishaji watu 277,000 huku matazamio ya wilaya hiyo ni aslimia 90 ya walioandikishwa watapiga kura.

Awali akizungumza na vyombo vya habari ofsini kwake,Bura amewahakikishia wananchi wote kuwa zoezi la kupiga kura litaendeshwa kwa uwazi mkubwa na kwamba kila mwananchi ajitokeze kuwachagua viongozi wanaofaa kuwatumikia wananchi.

Kushoto ni Katibu tawala(Das) wilaya ya Chato, Thomas Dimme, akiwasalimia wananchi na kulia ni mkuu wa wilaya hiyo.

Amevitaja vyama vilivyojitokeza kuweka wagombea kwenye nafasi mbalimbali za uongozi kuwa ni Chama cha Mapinduzi (CCM), Chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema) pamoja na ACT Wazalendo.

Kadhalika amewasisitiza wagombea wa vyama vyote kufanya kampeni za kistaarabu kwa kunadi sera za vyama vyao badala ya kutumia lugha za kejeli na matusi kwa madai kuwa wananchi wanahitaji kusikia mipango bora ya kutatua changamoto zinazowakabili.

Aidha amesisitiza kuwa Novemba 27 ni siku ya kuchagua viongozi, siyo kufanya kampeni na kwamba hakuna mwananchi yeyote atakaye ruhusiwa kuvaa sare zinazoashiria chama chochote cha siasa na atakaye kiuka maelekezo hayo sheria itachukua mkondo wake.