Serikali imeshitukia matumizi mabaya ya fedha za makusanyo ya ardhi kiasi cha Sh milioni 71.
Fedha hizo zinazodaiwa kutojulikana zilipo zinatokana na malipo ya viwanja 194 vya wakazi wa mji wa Hungumalwa, Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, Mkoa wa Mwanza.
Raia hao walitoa fedha hizo ili wapimiwe na kupewa hati za maeneo yao ya makazi na biashara.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, ametoa siku 90 kwa halmashauri hiyo, akisema hadi Mei 14, 2019 watu hao wawe wamekwisha kupata haki yao, vinginevyo hatua zitachukuliwa dhidi ya Mkuu wa Idara ya Ardhi na Mkurugenzi.
Uchunguzi wa JAMHURI unabainisha kuwa agizo kama hilo liliwahi kutolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Machi 2018.
Wakati huo waziri mkuu alizuru Kwimba na wananchi walimuonyesha mabango yenye malalamiko kuhusu dhuluma hiyo.
Majaliwa alikumbana na hali hiyo alipowasili mji wa Hungumalwa katika ziara ya kikazi na kuagiza ndani ya miezi mitatu, kuanzia wakati huo, watu hao wapimiwe viwanja vyao.
Lakini sasa, akiwa mjini Ngudu – Kwimba, Naibu Waziri Mabula ameeleza kukerwa na matumizi mabaya ya fedha hizo alizodai zimeliwa.
“Wapeni viwanja vyao. Kama hamtawapa ndani ya miezi mitatu tutahesabu hapa hatuna mtu wa ardhi, mkurugenzi na wewe utakuwa na la kwako.
“Kwa sababu ni mwiko kula hela ya mtu ukaitumia kwa mambo mengine halafu usimpe ardhi yake,” amesem Mabula na kuongeza: “Milioni 71 mmekula, viwanja hamjawapa. Halafu sasa mnataka mimi nianze kutoka wizarani.
“Hatufanyi biashara hiyo. Hatufanyi biashara hiyo,” amesisitiza naibu waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Mwanza.
Amesema suala hilo linaikosesha serikali imani kwa wananchi wake, hivyo hataki lelemama.
“Mna sifa mbaya. Mkurugenzi naagiza hawa wananchi wapeni viwanja vyao,” amesema Naibu Waziri huyo wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Baadhi ya wananchi waliotoa fedha ili wapimiwe maeneo yao wanasema imekuwa vigumu kupata haki yao licha ya kulipa fedha.
Mmoja wa wananchi hao aliyekataa kutajwa gazetini ambaye ni kati ya wanaoshinikiza maeneo yao kupimwa, amesema: “Tumedhulumiwa.”
Diwani wa Kata ya Hungumalwa, Shija Malando, amekiri fedha hizo kukusanywa na uongozi wa halmashauri lakini hazijulikani zilipo.
“Kila mtu alikuwa anatoa fedha kulingana na ukubwa au udogo wa eneo lake. Wale wenye maeneo ya biashara ndio walikuwa wanatoa hela nyingi,” Diwani Malando ameeleza katika mazungumzo yake na gazeti hili.
Malando ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo ya Kwimba, amesema ana wasiwasi na utekelezwaji wa agizo hilo la Waziri Mabula.
“Nakumbuka Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, mwezi Machi mwaka jana alikuja hapa naye akaagiza wananchi wapimiwe maeneo yao.
“Alipokelewa kwa mabango na wananchi hapa Hungumalwa wakidai fedha zao walizotoa wapimiwe viwanja. Lakini wapi.
“Hadi leo hakuna utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu,” amesema Malando.
Amesema vikao vilivyowahi kujadili na kutolea maelekezo suala hilo ni Kamati ya Mipango na Fedha, pamoja na Kamati ya Uchumi na Mazingira.
Kwa mujibu wa Malando, suala hilo liliwahi pia kujadiliwa na kuazimiwa na Baraza la Madiwani, lakini maazimio hayo yanaonekana kupuuzwa.
“Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya, Mhandisi Mtemi Msafiri (yupo Chato kwa sasa) Februari 18, 2018, akiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama na mkurugenzi mwenyewe, alikuja Hungumalwa akaagiza ndani ya miezi miwili wananchi hao wapimiwe viwanja vyao.
“Inavyoonekana hizi fedha wamekula. Sijui kwa nini viongozi wa serikali wanaagiza halafu maagizo yao yanapuuzwa?” amehoji Malando.
Amesema ufike wakati viongozi wanaopewa maagizo wayatekeleze, kwani kuyapuuza ni kinyume cha kanuni za utumishi.
Amesema tangu awe diwani mwaka 2010, amekuwa akipambana kutatua migogoro ya ardhi wilayani Kwimba.
Ofisa Ardhi Wilaya ya Kwimba, Wicklith Benda, alipoulizwa alisema: “Muulize mkurugenzi ndiye msemaji.”
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Pendo Malebeja, amesema tayari wamekwishaanza kulishughulikia suala hilo.
Hata hivyo, mkurugenzi huyo alikataa kujibu maswali mengine zaidi aliyoulizwa na gazeti hili.
“Njoo ofisini tuongee,” Malebeja amesema. Hata hivyo, gazeti hili limemtafuta wiki mbili mfululizo ofisini kwake bila mafanikio, na jitihada za kumtafuta zinaendelea.
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Kwimba, Maijo Faustine, amesema suala hilo wanalifanyia kazi.
“Hili jambo tunalo,” amesema mkuu huyo wa Takukuru Wilaya ya Kwimba.
Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Senyi Simon, amesema Kamati ya Ulinzi na Usalama imeagiza utekelezwaji wa agizo kuhusu suala hilo.
“Hili agizo la Naibu Waziri wa Ardhi lazima litekelezwe. Nimeshaagiza na nasubiri kuona utekelezaji wake,” amesema DC Senyi.