Na Mwandishi Wetu, Kibaha

Serikali imeipongeza Benki ya NMB kwa kutenga kiasi cha Sh. Mil. 225 kwa ajili ya kuzawadia Shule Bora katika Kampeni ya Upandaji Miti Milioni 1 ‘Kuza Mti Tukutuze,’ ambapo Shule ya Sekondari ya Mwambisi Forest ya Mamlaka ya Mji wa Kibaha, mkoani Pwani imeibuka kinara na kujizolea Sh. Mil. 50.

Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohammed Mchengerwa, wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi kwa shule vinara wa kampeni hiyo iliyozinduliwa Machi, 2023 na Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Philip Isdor Mpango, jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Juma Kimori, Mwambisi Forest ilipanda michezo 2,800 na kukuza kwa asilimia 99, ikifuatiwa na Shule ya Sekondari Ibondo ya Sengerema, Mwanza, iliyopanda na kutunza asilimia 88.5 ya miti yao na kuzawadiwa Sh. Mil. 30.

Shule ya Msingi Itimbo, iliyopo Mafinga Mkoani Iringa, ilifanikiwa kupanda, kutunza na kukuza asilimia 83.2 na kujizolea Sh. Milioni 20, huku shule shiriki 19 zilizopanda miti 1,000 au zaidi na kuwa na ustawishaji wa asilimia 60 ya miti hiyo, kila shule ikizawadiwa Shilingi Milioni 2 kila moja.

Aidha, shule zingine 121 zilizoshiriki ‘Kuza Mti Tukutuze’ ya NMB, zimepewa kifuta jasho cha Shilingi 500,000 pamoja na vyeti vya shukrani kwa kila shule kwa ushiriki bora wa kampeni hiyo iliyoshirikisha Shule za Msingi na Sekondari 189 kutoka katika Halmashauri 184 Tanzania Bara na Visiwani. 

“Pongezi za Serikali ziwaendee NMB, sio tu kwa dhamira ya dhati ya utunzaji mazingira kwa kuanzisha kampeni ya upandaji miti milioni 1 kote nchini, bali kushirikisha shule 189 kutoka halmashauri zetu zote nchini kote, hii ni njia bora kabisa ya kuibua kizazi chenye mtazamo chanya juu ya mazingira.

“Tunawapongeza washindi waliofanya vizuri katika shindano la mashule, pongezi kwenu Mwambisi Forest kupanda na kuitunza asilimia 99 ya miti 2,800 mliyochukua, ubora wenu huu katika utunzaji mazingira, ukaakisi ufaulu wenu katika mitihani kwa kupata ufaului mzuri,” alisema Waziri Mchengerwa.

Alibainisha ya kwamba NMB imethibitisha kuwa sio tu vinara wa masuala ya kifedha, bali katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo endelevu ya taifa na kuutaja uamuzi wa benki hiyo kutenga Sh. Mil. 225 kwa ajili ya zawadi za motisha kwa shule zitakazostawisha miti, kuwa kielelzo cha dhamira njema ya taasisi hiyo kwa vizazi vya sasa na vijavyo

Aidha, aliipongeza NMB kwa kutenga kiasi cha Sh. Bilioni 100 za mikopo nafuu kwa wauzaji, wasamabazaji na mawakala wa Nisati Safi ya Kupikia, na kubainisha kuwa fungu hilo la mikopo nafuu linathibitisha dhamira ya dhati ya benki, inayoenda nchi nzima kusaidia jamii kuachana na Nishati Chafu.

“Katika hili, NMB mmeenda mbali kwa kusambaza elimu juu ya Nishati Safi ya Kupikia huko vijiji, kupitia Jukwaa la NMB Kijiji Day. Hongereni sana, jambo hili ni kielezo cha dhamira yenu ya kujenga jamii iliyoelimika, jambo hili linalenga kujenga jamii salama, jamii yenye afya njema, jamii rafiki na mazingira ya taifa letu

“Wito wangu kwa taasisi zingine zote nchini, ziige mfano wa NMB kwa kushirikiana na Serikali katika juhudi za kulinda, kutunza na kuhifadhi mazingira, kuboresha elimu, juhudi ambazo zinalenga kukuza uchumi na kustawisha jamii na taifa kwa ujumla,” alisisitiza Waziri Mchengerwa.

Awali, Afisa Mkuu wa Fedha NMB, Bw. Juma Kimori aliishukuru Serikali kupitia TAMISEMI, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Wizara ya Maliasili na Utalii, Shule Shiriki 189, Magereza mbalimbali, UDART na taasisi nyingine kwa kufanikisha kampeni hiyo.

Kimori alibainisha kuwa, kama wadau vinara wa maendeleo nchini, walichagua kujivika ujasiri na uthubutu kuitokana na imani yao kuwa Kuza Mti Tukutuze ingetoa mchango mkubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kwamba walivuka lengo la kupanda miti milioni 1, ikapandwa miti 1,400,000 kote nchini.

“Kupitia mchakato uliofanywa na TAMISEMI, washindi wetu wa kwanza ni Mwambisi Forest Sekondari ya hapa Kibaha, Pwani ambao wanajipatia Sh. Mil. 50, Ibondo Sekondari ya Sengerema Mwanza ya pili Sh. Mil. 30, na Itimbo Shule ya Msingi ya Mafinga imeibuka washindi wa tatu na kuzoa Sh. Mil. 20.

“Ningependa kuzipongeza shule hizi kwa kazi kubwa waliyoifanya, hakika mmeonyesha nia na adhma kubwa katika kushiriki kwenye kutunza mazingira ya shule zenu. Fedha hizi mlizoshinda hakika zitaenda kuboresha shule zenu na zikawe kichocheo cha kuendelea kupenda kutunza mazingira.

Aidha, alimueleza Waziri Mchengerwa kuwa katika kuhakikisha dhamira ya utunzaji mazingira kupitia upandaji na utunzaji miti inaliwezesha taifa kukabiliana na mabadiliko ya taibianchi, NMB imetenga kiasi cha Sh Bilioni 100, kwa ajili ya utoaji wa mikopo maalum kwa miradi, na biashara zinazolenga kupeleka nishati safi ya kupikia kwa Watanzania.

“Mbali na mikopo hii, NMB kwa kutumia Jukwaa letu la usambazi wa huduma za Kibenki vijijini la NMB Kijiji Day, tunatumia nafasi hiyo pia kutoa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wakazi wa vijiji husika tunavyotembelea, katika kufanikisha hili, wenzetu wa Taifa Gas nao wameungana nasi katika utoaji wa elimu hiyo,” alisema.

Akimkaribisha Waziri Mchengerwa, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Aboubakar Kunenge, aliipongeza NMB kwa wazo lililozaa shindano la Kuza Mti Tukutuze, huku akisema Mwambisi Forest Sekondari imemheshimisha yeye, mkoa na watu wake kwa ujumla.

“Mkoa wa Pwani ni kati ya mikoa iliyo kwenye vita ya mabadiliko tabianchi yatokanayo na ukataji miti na kupotea kwa mapori ya asili, huu ndio mkoa unaozalisha asilimia kubwa ya mkaa unaotumika Dar es Salaa na tumefanya jitihada kubwa kutekeleza agizo la Makamu wa Rais la kupanda miti milioni 1.5 kwa kila Halmshauri.

“Mwaka jana tulipanda miti milioni 10 kwa halmshauri zetu zote, sawa na asilimia 77, na mwaka huu tayari tumeshasambaza miti milioni 10 kwa ajili ya upandaji na kwa Wilaya ya Kibaha Mji tumeshapanda miti 1,4000. Mwambisi Sekondari kuwa kinara wa shindano hili ni kielelzo cha jitihada zetu kama wilaya na mkoa,” alisema DC Nickson.