NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema, Serikali imeongeza vituo vyenye vyumba maalumu kwa ajili ya kutoa huduma kwa watoto wachanga wenye umri kati ya sifuri mpaka mitano wenye hali mahututi (Neonatal Care Unit), kutoka 18 mwaka 2017 kufikia 175 mwaka 2023.
Amesema leo Juni 28,2023 wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu Mhe. Zaytun Seif Swai katika kikao cha kumi na mbili, Bungeni Jijini Dodoma.
“Serikali kupitia wizara ya Afya imeweka mipango ya kupunguza vifo vya watoto wenye umri 0 hadi 1 kwa kuongeza vituo vyenye vyumba maalumu kwa ajili ya kutoa huduma kwa watoto wachanga wenye hali mahututi (Neonatal Care Unit), kutoka 18 mwaka 2017 kufikia 175 mwaka 2023.” Amesema
Ameendelea kusema, Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kutoa mafunzo kwa watoa huduma juu ya namna ya kutoa huduma jumuishi kwa watoto wachanga na watoto wakubwa (Intergrated Management of Childhood Illness-IMCI) ili kuokoa vifo vya watoto hao vinavyoweza kuepukika.
Amesema, Serikali imeendelea kuimarisha huduma za kukinga na kuzuia magonjwa yanayozuilika kwa Chanjo kama vile Surua, Nimonia, kuharisha, donda koo, kifaduro, pepo punda na polio kwa kuongeza utoaji wa chanjo za Watoto chini ya Mwaka mmoja kufikia kiwango cha zaidi ya asilimia 98 ya utoaji wa chanjo ya Penta 3.
Aidha, Dkt. Mollel amesema, Serikali imeongeza vituo vinavyotoa huduma kwa watoto waliozaliwa wakiwa na uzito pungufu (Kangaroo Mother Care) ambapo kwa sasa vituo 72 na Hospitali 175 zinatoa huduma hizi, huku akiweka wazi kuwa, kwa mwaka 2023/2024 Serikali imepanga kuongeza vituo 100 ili kufikia vituo 275 ifikapo mwezi Juni 2024 vitavyosaidia kuongeza huduma hizo nchini.
Sambamba na hilo Dkt. Mollel amesema Serikali imeendelea kuongeza vifaa na vifaa tiba ikiwemo CT-SCAN zimeongezeka kutoka 3 mpaka sasa zipo zaidi ya 50, MRI zilikuwa 2 lakini mpaka sasa zipo zaidi ya 19, hivyo kumtoa kuwaondoa hofu Wabunge kuwa hata vifaa vya huduma hizo vitaenda kuwekwa kwenye vituo vyote 100 vitavyojengwa nchini.
Kwa upande mwingine Dkt. Mollel amesema, ili kukabiliana na changamoto ya gharama za matibabu kwa wazee, Wizara inaendelea kuhamasisha Wabunge na viongozi wengine pamoja na wananchi kuunga mkono Bima ya afya kwa wote ili kila mwananchi aweze kunufaika na huduma bora bila gharama kuanzia ngazi ya Zahanati mpaka hospitali ya Taifa.