Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia
Serikali imeeleza kuendelea na mchakato wa mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari na hatua inayofuata ni kufanya mapitio ya mwisho ya mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari ya 2016.
Akizungumza katika kikao cha pili cha Wadau wa Kupata Habari (CoRI), kilichofanyika jijini Dar es Salaam Novemba 21,2022 ,Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema kuwa Serikali imepokea mapendekezo hayo na sasa wanayafanyiakazi.
“Serikali inaendelea na mchakato wa mabadiliko ya sheria na sasa tunayafanyia mapitio ya mwisho ya mapendelezo ya marekebisho ya sheria,” amesema.
Nape amesema kuwa hatua inayofuata baada ya kikao hicho, ni uandishi wa mapendekezo hayo na kisha kupelekwa kwa watunga sheria.
” Niwahakikishie kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, inayo nia ya dhati katika jambo hili.
“Nimekuja mwenyewe kuwasilikiliza na imani yangu ni kuona sekta inaendelea kukua” alisema.
“…tupo kwa ajili ya kufanya mapitio ya mwisho ya mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari ya 2016,” amesema.
Hata hivyo baada ya kikao hicho, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile ambaye alisema kuna muelekeo mzuri kuelekea mabadiliko ya sheria ya habari.
‘‘Kikao kilikuwa kizuri, serikali imeendelea kuonesha dhamira yake ambayo ilikuwa nayo tangu mwanzo. Tumemaliza na serikali inaendelea na hatua zake kabla ya kupelekwa bungeni.
‘‘Suala la mabadiliko ya vipengele vya sheria lina mchakato wake, cha msingi Serikali imetoa fursa, na si kutoa peke yake, inaendelea kuchukua hatua,’’ alisema Balile.
Miongoni mwa mapendekezo ya CoRI kwa Serikali ni pamoja na mamlaka haya ya Mkurugenzi wa Habari (MAELEZO) yafutwe na kiundwe chombo ambacho pamoja na mambo mengine, kitashughulikia masuala ya usuluhishi yanapotolewa malalamiko dhidi ya chombo cha habari, badala ya kazi hiyo kufanywa na mtu mmoja.
Wadau wanataka marekebisho dhidi ya kifungu cha 6 (e) kinachoelekeza magazeti kupatiwa leseni badala ya usajili wa moja kwa moja.
Pia wadau hao wanapendekeza magazeti yasiendeshwe kwa kupewa leseni, badala yake yapewe usajili wa kudumu au wa muda mrefu, ili kudhibiti changamoto ya ufutwaji holela wa leseni na kuvutia wawekezaji.
Mapendekezo mengine kuhusu sheria hiyo, ni marekebisho dhidi ya kifungu chake cha 7 (2)(b)(lV), kinachoelekeza vyombo vya habari kutangaza au kuchapisha habari na masuala yenye umuhimu kwa taifa, kadiri itakavyelekezwa na serikali, wadai wakieleza kipengele hiki kinaingilia uhuru wa uhariri.
Sheria nyingine zinazolalamikiwa ni Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Huduma za Posta (EPOCA, 2010), Sheria ya Makosa Mtandaoni (2015), Sheria ya Haki ya Kupata Habari (2016) na Kanuni za Maudhui Mtandao (2018) kama zilivyorekebishwa mara kadhaa.