Serikali imetangaza kuondoa ukomo wa matumizi ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) vilivyomalizika muda wake kufuatia mabadiliko ya Kanuni za Usajili na Utambuzi wa Watu za mwaka 2014.

Hayo yamesemwa leo Februari 21, 2023 na Waziri, Mambo ya Ndani ya Nchi Eng. Hamad Masauni alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari juu ya Marekebisho ya Kanuni za Usajili na Utambuzi wa Watu za mwaka 2014 na kueleza kuwa Vitambulisho vya Taifa kwa raia, Vitaendelea kutumika bila kujali Muda wa Ukomo wa matumizi uliopo kwenye vitambulisho hivyo isipokuwa kwa wageni wakaazi na Wakimbizi.

Eng. Hamad Masauni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi

Mchakato wa Marekebisho ya Kanuni umekamilika na tayari kanuni hizo zimeanza kutumika baada ya kutangazwa rasmi kwa tangazo la serikali (GN) Na 96 la tarehe 17 Februari 2023.

Serikali imetoa rai kwa watoa huduma wote nchini wanaotumia utambulisho wa Taifa kutoa huduma kwa wananchi hususan Taasisi za fedha, Benki na Kampuni za simu kuendelea kuvitambua na kuvitumia Vitambulisho vya Taifa ambavyo vina tarehe ya muda wa ukomo wa matumizi.