Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia,Songea
Waendesha bodaboda na vyombo vingine vya moto wameomba Serikali ione umuhimu wa kuchukuwa hatua za haraka kuwadhibiti baadhi ya wafanyabiashara wa vituo vya mafuta katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea ambao baada ya kusikia Serikali imevifungua baadhi ya vituo vya mafuta kwa madai ya kuficha mafuta ya Petrol kwa lengo la kutaka kuongeza bei .
Hayo yamesemwa kwa nyakati tofauti na waendesha boda boda waliokuwa wakiongea na waandishi wa habari kwenye maeneo ya vituo vya kuuzia mafuta vilivyopo jirani na kituo cha mabasi ya daladala cha kata ya mfaranyaki mjini hapa.
Walisema hali kwa sasa bado sio nzuri ya upatikanaji wa mafuta kwani mafuta yameadimika kwa zaidi ya wiki hadi sasa jambo ambalo limekuwa ni kero kubwa kwa wakazi wa Manispaa ya Songea wakiwemo abiria ambao wamedai kuwa hata nauli zimepanda kutokana na uhaba wa mafuta uliopo.
Sebastian Nchimbi mkazi wa Lizaboni Manispaa ya Songea alisema kuwa mafuta yamekuwa na changamoto tangu wiki iliyopita na kituo kinachotoa mafuta ni cha Kisumapai tu napo ukienda wa bodaboda unapewa lita zisizozidi mbili za mafuta hawaelewi tatizo ni nini.
” Ndugu waandishi suala la mafuta limekuwa changamoto kubwa kwetu sisi waendesha bodaboda tunapoenda na madumu ya mafuta wanatukatalia kuchukuwa mafuta wakati wengine wanaendesha bodaboda inakuzimikia mbali na kituo cha mafuta ambapo hulazimika kuchukuwa madumu kwenda kutafuta mafuta.” alisema Nchimbi.
Jackson Matembo mkazi wa mfaranyaki anasema kuwa kuna baadhi ya watu wengine wanashindwa kufanya kazi kabisa kutokana na uhaba wa mafuta hivyo wanaiomba Serikali iangalie kwa umakini kwa baadhi ya wafanya biashara wanaoficha mafuta na kuwachukulia hatua za kinidhamu dhidi yao ikiwemo kuwafungia vituo vya mafuta kama walivyofanya kwa mikoa mingine.
Pius Magagula mwendesha boda boda anasema kuwa serikali inawafuga wafanyabiashara wa mafuta kwa sababu wafanyabiashara wanauza mafuta wanavyojisikia wao wanasema mafuta hamna wakati serikali inasema hakuna shida ya mafuta lengo wanataka bei ya mafuta ikipanda ndo waanze kuuza kwa kuwa sisi ni wavunilivu hatuwezi kuandamana ila tunaomba serikali itusaidie kumaliza tatizo lililopo la uhaba wa mafuta.
Kwa upande wake msimamizi wa kituo cha mafuta cha Refueling Solution Abdul Aziz Abbas amekiri kuwepo kwa uhaba wa mafuta aina ya petrol kwenye kituo chake tangu September 1 mwaka huu na kwamba kwa hivi Sasa kituo kinatoa huduma ya kuuza mafuta aina ya dizel tu na si vinginevyo licha ya kuwa mafuta yanaweza kuingia muda wowote kuanzia sasa.
Nae mmiliki wa kituo cha mafuta cha Kisumapai Dastan Ngonyani alipofuatwa kuhojiwa na waandishi wa habari juu ya malalamiko ya waendesha boda boda pamoja na baadhi ya wamiliki wengine wa vyombo vya moto kwamba wanauza mafuta kwa masharti alisema kuwa kwa sasa hivi hawezi kuongea kitu chochote kwa kuwa yupo mbali na kituo.