Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha

Serikali imeombwa kuondoa kodi ya maziwa yanayosafirishwa kutoka nje ya nchi ili bei ya maziwa iwe shindani na kuweza kupanua soko la maziwa zaidi.

Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Afisa mauzo kutoka kampuni ya kuagiza na kusambaza bidhaa za matumizi ya nyumbani ya Nead Distributors Ltd,Zullu Sadiq wakati akizungumza mbele ya Mkuu wa wilaya ya Babati ,Lazaro Twange alipotembelea banda lao katika viwanja vya nanenane vilivyopo Themi Njiro.

Mkuu wa wilaya ya Babati, Lazaro Twange akipata maelezo kutoka kwa Afisa mauzo wa kampuni ya Nead Distributors Ltd,Zullu Sadiq  baada ya kutembelea banda hilo. 

Zullu amesema kuwa, kwa kila kilo moja ya maziwa inayoingizwa nchini ina kodi kubwa sana ikilinganishwa na maziwa yanayotengenezwa hapa nchini Tanzania,jambo ambalo limekuwa ni changamoto kubwa kwao.

Ameiomba serikali kutoa kodi hiyo kwenye maziwa kwani ni chakula cha watoto na huwezi weka kodi kubwa hivyo kwenye chakula kwani maziwa hayo yanasaidia kuboresha afya ya watoto.

“Tunaomba serikali itufikirie katika hilo na kama ikishindikana kabisa tunaomba itoze kodi ndogo ya shs mia tatu kwa kila Lita moja ya maziwa yanayoingia nchini kama wanavyofanya wenzetu wa Tanzania visiwani Zanzibar ili bei ya maziwa iweze kuwa shindani”amesema Zullu.

Aidha amesema kuwa, kuliko kuweka Kodi kwenye chakula kama maziwa badala yake ielekeze Kodi nyingi katika bidhaa kama pombe badala ya kuweka kwenye maziwa ambayo ni chakula cha watoto.

“Sisi tunaamini serikali yetu ni sikivu sana na tuna imani na Rais Samia Suluhu Hassan ,hivyo ni matarajio yetu kuwa kilio chetu kitasikika kwani imekuwa ni changamoto kubwa ambayo inasababisha tushindwe kufanya biashara kwa uhuru zaidi”amesema Zullu.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Babati, Lazaro Twange amesema kuwa amesikia changamoto hiyo na ataipeleka sehemu husika ili iweze kufanyiwa kazi huku akiwataka kujipanua zaidi na kujitangaza ili bidhaa zao ziweze kufahamika kila mahali.