Huwezi kuzungumzia kuhusu Hifadhi za Taifa za Gombe, pamoja na ile ya Milima ya Mahale, bila kutaja jina la Dk. Jane Goodall, ambaye ametumia miaka zaidi ya 57 katika kutafiti maisha na tabia za sokwe.
Katika kutambua jitihada zake, Serikali imempatia tuzo Dk. Jane Goodall, Waziri wa Mali Asili na Utalii, Prof Jumanne Maghembe, ametoa sababu kadhaa za kumpatia tuzo mtafiti huyo ambaye ametumia muda wake mwingi kutafiti maisha ya sokwe.
“Wakati Dk. Jane Goodall anafanya utafiti mimi nilikuwa darasa la pili, katika kipindi hicho cha utafiti wake aliweza kuithibitishia dunia kwamba sokwe mtu si tu kwamba wanakula matunda, bali wanakula nyama pamoja na kutumia zana katika maisha yao ya kila siku.
“Wakati anafanya utafiti huo dunia haikuwa inaelewa sana kuhusu sokwe mtu, kilichoshangaza zaidi ni kuona namna wakati ule binti mdogo alivyoweza kujikita katika utafiti ambao aliusimamia na leo amekuwa shujaa hapa duniani, ushujaa huo huko duniani ameupata kutokana na kutafiti kuhusu sokwe mtu, hasa hapa kwetu Tanzania.
“Haikuwa kazi nyepesi kwa Goodall kuwazoesha sokwe pamoja na kufanya utafiti wake, alikuwa alitumia ndizi kuwafanya wawe karibu naye,” amesema Prof. Maghembe.
Akizungumza kuhusu tuzo aliyopewa, Dk. Jane Goodall, amesema anaishukuru Serikali kwa namna ambavyo imethamini kazi za utafiti alioufanya, huku akisisitiza hana maneno mazuri zaidi ya kusema kuonesha furaha yake.
“Ninashukuru sana kwa tuzo hizi…sina maneno mazuri ya kushukuru. Nilizaliwa nikiwapenda wanyama, kila mmoja alinishangaa niliposema nakwenda Afrika, bara la giza…hata familia yangu haikuwa na furaha kwa sababu hawakuwa wanaelewa vizuri kuhusu Afrika. Niliwaambia nakwenda kuishi porini na kufanya utafiti,” amesema Dk. Jane Goodall.
Huku ukumbi wa Chuo cha Utalii, ukiwa umefurika wageni mahsusi, waliokuwa kimya wakimsikiliza Dk. Goodall, anakumbuka namna alivyoingia katika bara la Afrika, akitokea kwao Uingereza akitumia usafiri wa majini, kupitia Mfereji wa Suez.
“Sehemu ya kwanza kufika hapa Afrika ilikuwa ni Cape Town, nilikuwa naangalia Mlima wa Meza huko Afrika Kusini. Baadaye nikaenda Kenya nikakaa na rafiki zangu pale, pale nikakutana na Dr Louis Leakey, baba yake Richard. Akanipa kazi ya kutunza kumbukumbu. Kwangu mimi fursa zimekuwa zinakuja tu,” anakumbuka Dk. Goodall.
Historia yake katika utafiti wa sokwe mtu
Umewahi kuwaza kuhusu binti wa miaka 26, kutoka katika nchi na bara lake na kwenda bara jingine katika kile kinachoitwa kutimiza ndoto zake? Ukikutana na Dk. Jane Goodall na kumuuliza swali hilo, jibu lake ni rahisi sana, ndiyo.
Dk. Jane anaanza kwa kuzungumzia safari pamoja na ndoto yake mpaka hapo alipo leo. Anakumbuka magumu aliyoyapitia katika familia yake. Anasema alikuwa anapenda wanyama tangu akiwa mtoto mdogo. Anakumbuka kwao hapakuwa na televisheni kwa hiyo wanyama alikuwa akiwasoma kwenye vitabu tu.
“Nilikuja Tanganyika Julai 1960, nikiwa na umri wa miaka 26. Nilisafiri kutoka Uingereza mpaka hapa, eneo ambalo leo linajulikana kama nyumbani kwa sokwe mtu. Nilikuja hapa nikiwa na sehemu ya kuandikia kumbukumbu pamoja na darubini,” anasema Dk. Jane.
Amesema kutokana na jinsi alivyokuwa anapenda wanyama, alitokea kuvutiwa na sokwe mtu. Tangu kipindi hicho maisha yake yakajikita kwenye utafiti wa sokwe mtu, ambao kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi yake, wanyama hao wanafanana kwa asilimia kubwa na binadamu. Wanafanana kuanzia mfumo wa upumuaji, damu mpaka hata ubongo.
“Nilifika hapa Tanganyika (Tanzania) baada ya kuelekezwa na rafiki zangu waliokuwa Kenya. Nilielekezwa kwa Dk. Louis Leakey ambaye alikuwa akifanya tafiti zake huku… baada ya kukutana naye nilionesha kwamba ninapenda sana wanyama, alinikubalia na nilianza,” amesema Dk. Jane.
Anaongeza, “Nilikuwa na ndoto ya kuja Afrika, lakini nilikuwa nachekwa sana na rafiki zangu ambao walikuwa wanajua hali ya uchumi wa nyumbani. Sikuwa na fedha na nilikuwa naambiwa Afrika ni mbali sana…nilikaribishwa na Dk. Louis Leakey ambaye alikuwa anafanya utafiti.”
Amesema katika utafiti wake wa sokwe, anamkumbuka sokwe mtu, aliyekuwa amempa jina la David. Anasema sokwe mtu huyo ndiye aliyekuwa rafiki yake, baada ya kuanza kumfuatilia na ndiyo akasababisha Dk. Jane kuanza majaribio ya kuwazoesha sokwe mtu kuwasogelea binadamu.
“Sokwe mtu wanazo namna mbalimbali za kuwasiliana…sokwe hao hao pia wanatengeneza zana ambazo zinawasaidia kumudu mazingira wanayokutana nayo. Sokwe mtu kwa kiwango kikubwa anafanana na binadamu, lakini wana nguvu zaidi ya binadamu,” amesema Dk. Jane.
Dk. Jane amesema maisha ya sokwe mtu yanafanana kwa kiwango kikubwa na yale ya binadamu, ingawa yeye anabeba mimba kwa miezi minane na wiki mbili tu. Akizaa hulea mtoto kwa miaka minne mpaka mitano. Katika kipindi hicho sokwe jike, hawezi kuzaa mpaka atakapomwachisha kunyonya mtoto wake.
Amesema sokwe mtu akiwa na mimba anapenda kulala na hatembei umbali mrefu. Akifikia kipindi cha kujifungua hutoweka. Mtoto akifikisha siku tatu ndiyo huanza kujichanganya na sokwe wengine. Ananyonyesha kwa kipindi cha miezi sita bila kumpatia mtoto chakula cha aina yoyote.
Sokwe huzaa mapacha, ila ni aghalabu kutokea. Gombe wapo mapacha – Greter na Golden – mama yao anaitwa Gremlin. Kwa sasa sokwe hao mapacha wana miaka 23. Sokwe mwenye jina la Fifi alipata kuzaa mapacha, japokuwa walishakufa, walikufa wakiwa na zaidi ya miaka 16.
Sokwe huyo alikuwa anabeba mtoto mmoja mgongoni na mwingine tumboni, na wakati mwingine huwabeba wote mgongoni.
Watoto mapacha wa sokwe wanashirikiana, kukitokea ugomvi wanasaidiana. Mara nyingi hupenda kutembea pamoja. Hata ikifikia kipindi cha wao kuanza kuzaa urafiki huendelea na wanatambuana kama wanafamilia.
Kwa nini sokwe wanapewa majina? Dk. Jane anasema kuwapa majina sokwe mtu kulilenga kuendelea kuwachunguza tabia zao katika tafiti zake. Anasema yeye kama mtafiti imekuwa rahisi zaidi hata kuwafananisha tabia kutoka kizazi kimoja cha sokwe mtu kwenda kingine.
Ukienda katika Hifadhi ya Taifa ya Gombe, majina kama Glitter pamoja na Golden siyo mageni. Hao ni sokwe mtu pacha ambao wote pia wana watoto. Dk. Jane anasema sokwe mtu hawafanani, wako kama ambavyo binadamu tunatofautiana kwa sura, tabia na hata matendo.
“Sokwe hawafanani sura. Wana tofauti kubwa tu usoni. Unaweza kukuta sokwe mtu mmoja ni mweusi zaidi, wakati mwingine ngozi yake ni angavu, mwingine anakuwa na manyoya ya tofauti. Pia hutofautishwa kwa tabia. Utakuta huyu anapenda kucheza sana wakati mwingine hapendi. Wengine wanakuwa wachoyo na wengine siyo wachoyo,” anasema Dk. Jane.
Kuhusu utawala wa sokwe mtu, Dk. Jane anasema wanao muundo wa utawala wao. Utawala huenda kwa sokwe mtu mwenye nguvu zaidi pamoja na busara, kuwaongoza wenzake. Madume wanapigana mpaka mmoja anayeshinda ndiye anayekuwa kiongozi na hatimaye kutengeneza himaya.
Anasema katika utawala wake anakuwa na sokwe wengine ambao ikitokea uvamizi wa sokwe mwingine wanamsaidia kupigana na sokwe wengine.
Dk. Jane anasema Serikali inapata mapato kutoka katika sekta ya utalii, kwa hiyo Serikali inapaswa kuwekeza katika suala la ikolojia. Inatakiwa pia kuangalia suala la miundombinu na kukifikiria kizazi kijacho, mazingira yasiharibiwe.
Akielezea kuhusu changamoto anazokutana nazo katika kuwatafiti sokwe mtu, Dk. Jane anasema mwanzo kulikuwa na msitu mnene unaounganisha Ziwa Tanganyika na sehemu za Rwanda na Uganda, lakini kwa sasa uhabifu mkubwa umefanyika na kwamba uharibifu huo umewafanya sokwe wengi kuondoka katika maeneo yao ya asili na kwenda nje ya hifadhi.
Anasema Tanzania inatakiwa kujivunia matunda makubwa ya tafiti ambazo zimekuwa zikifanywa, kwani imekuwa nchi ya kwanza kuanzisha utafiti wa sokwe mtu duniani, na tafiti hizo zimekuwa zikiendelea kufanyika.
Dk. Jane Goodall anasifia jitihada za Rais Magufuli za kupambana na rushwa. Anasema mapambano hayo dhidi ya rushwa yatakuwa na maana kubwa kwa Shirika la Hifadhi za Taifa na hifadhi zote nchini, maana fedha za kuwezesha uhifadhi zitapatikana.
Anayo matumaini kwamba jitihada zinazofanywa na Rais Magufuli zimelenga katika kuondosha matumizi mabaya ya ofisi za umma, na kitendo hicho kitaongeza ufanisi katika uhifadhi na hivyo kuongeza idadi ya watalii na pato la nchi litokanalo na sekta hiyo.
Enzi hizo, Dk. Louis Leakey, ambaye alikuwa nchini Kenya, akiendelea na tafiti zake, Dk. Jane alimpigia simu na kumwomba wakutane kujadiliana kuhusu wanyama. Dk. Leakey aliamini kwamba tafiti za kuishi kwa binadamu wa kale, alizokuwa anafanya zingeweza kuhusishwa na kuishi kwa sokwe mtu, hivyo naye alihitaji kumpata mtafiti kama Dk. Jane.
Dk. Leakey aliamua kubadili mawazo na kuamua kumfanya Dk. Jane kuwa katibu wake. Alimtuma katika Bonde la Olduvai ambako tayari alikuwa akiendelea vyema na mikakati yake ya utafiti. Mwaka 1958, Leakey alimtuma Dk. Jane, London.
Mtafiti huyo wa binadamu wa kale alitafuta fedha na Julai 4, 1960 alimtuma Dk. Jane katika Hifadhi ya Taifa ya Gombe kufanya utafiti. Dk. Jane alipokewa na Jumanne Rashid, mkazi wa Kigoma. Anakumbuka kwamba alimpokea mtafiti huyo wa sokwe mtu akiwa ameambatana na mama yake.
Jumanne Rashid, ambaye kipindi hicho alikuwa kijana mdogo, alikuwa pia Gombe. Alimsaidia Dk. Jane kutoa mizigo kwenye meli na kuandaa kambi kando ya Ziwa Tanganyika kwa ajili ya utafiti. Dk. Jane alirudi katika Chuo Kikuu cha Cambridge mwaka 1962 ambako alikwenda kusoma shahada ya uzamivu katika etholijia.
Alianza kufanya utafiti kuhusu jamii ya sokwe mtu walioshi Kasekela ndani ya Hifadhi ya Gombe. Hapo alikutana na sokwe na kuwapatia majina ya Fifi pamoja na David Greybeard ambao alikuwa akiwafuatilia kuhusu tabia zao.
Kutokana na utafiti wa Dk. Jane ulioanza mwaka 1960, leo Gombe ni hifadhi maarufu kuliko zote duniani kutokana na sifa hii ya kuwapo kwa sokwe mtu.
Dk Jane anaelezea namna alivyoanza kuwazoesha sokwe ili kurahisisha kazi yake ya utafiti, anasema alianza kuwazoesha sokwe kwa kutumia matunda, hasa ndizi. Anasema sokwe mtu wanapenda sana ndizi, hivyo katika kuhakikisha anafanikiwa alihitaji kuwatafutia chakula wanachopenda.
“Nilianza kuwazoesha sokwe mtu kwa kutumia ndizi, hiyo ilikuwa ni hatua muhimu sana katika utafiti wangu. Haikuwa kazi rahisi kuwazoesha maana sokwe mtu kwa asili wanakuwa na haya, hivyo ilinichukua muda mrefu kidogo,” anasema Dk Jane.
Anasisitiza kwamba kitendo cha kuwazoesha sokwe mtu, kimeweza kurahisisha sasa wanaweza kusogelewa na watalii na kuwatazama kwa umbali wa mita tano mpaka kumi. Anasema kitendo hicho kimechukua muda mrefu kidogo.
Anasema katika kuwazoesha sokwe mtu, huchaguliwa familia moja ambayo hupewa majina na kuwafuatilia makazi yao, tangu wanapoamka asubuhi na pindi wanapokwenda kulala, jioni. Sokwe mtu wanaandaa sehemu ya malazi kama ilivyo kwa binadamu.
Dk Jane anasema sokwe mtu, hulala na kuamka mapema, huku wakiitana na kuthibitisha kama wote ni wazima. Baada ya kukamilisha zoezi hilo, huanza maisha yao ya kawaida kwa kwenda kutafuta chakula pamoja na shughuli nyingine.
Alipoulizwa kama angeanza kufanya kazi ya kuwazoesha sokwe mtu leo angetumia mbinu zilezile za kuwapatia ndizi, Dk Jane anasema kwamba, asingeweza kufanya hivyo tena, maana wanyama hao kwa asili hujitafutia chakula wenyewe na anahisi alifanya makosa kwa aina ya ushawishi aliyoitumia kwa sokwe mtu.
“Kama ningeanza leo kufanya hii kazi ambayo sasa nimekuwa nikiifanya kwa zaidi ya miaka 50, nisingefanya kama nilivyofanya kipindi kile wakati ninaanza. Leo ningewazoesha sokwe mtu kwa mazingira yao ya kawaida kabisa,” anasema Dk Jane.
Mtafiti huyo anasema katika miongo zaidi ya mitano ya utafiti wa sokwe mtu, amejifunza namna ya kuwasiliana nao kwa karibu hasa kupitia sauti maalumu. Anasema amekuwa akiwaita sokwe mtu pindi anapowahitaji na wamekuwa wakimuitikia.
“Nimekuwa nikiwaita sokwe mtu pindi ninapowahitaji, wamekuwa wanakuja na kunikumbatia vizuri kabisa. Ninawapenda sana, nao wamekuwa wakionesha upendo mkubwa sana kwangu,” anasimulia Dk Jane.
Wakati akiendelea na mahojiano maalumu anaanza kuwaita sokwe mtu kwa sauti ya kuwaelezea kwamba yuko maeneo jirani, katika muda mfupi walimuitikia, na Dk Jane anasema walikuwa wakimueleza sehemu walipo.
Hakika ilikuwa inavutia kuona anaweza kuwasiliana na sokwe mtu, na wao baada ya muda mfupi wanaonesha kuielewa lugha iliyotumiwa na Dk Jane. Anasema katika sokwe mtu ambao amekuwa akiwatafiti, daima David atabaki katika kumbukumbu zake, maana alitokea kuwa rafiki yake mkubwa.
Dk Jane anasema aliweza kuutumia ushawishi wa sokwe mtu David, ili kuweza kuingia kwenye makundi ya sokwe mtu wengine. Anasema David alikuwa ni kiongozi mzuri na ndiye alikuwa akileta makundi mengine kwake, na ikawezesha kuwazoesha kwa urahisi.
“Nakumbuka sokwe mtu David, akiwa rafiki yangu sana, alipokuwa akiniona alikuja mbio na kunilaki…alikuwa anafanya kama wafanyavyo binadamu, alikuwa ananikumbatia nami ninampapasa kichwani kuonesha kwamba ninamheshimu sana,” anasema Dk Jane
Na Mkinga Mkinga