. Yamnyang’anya umiliki wa ardhi aliyojipatia kinyemela

. Aliitumia kuuza viwanja kwa wageni kinyume cha sheria

. Raia wa Zimbabwe alishauziwa na kujenya nyumba

Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imemnyang’anya raia wa Uswiss umiliki wa ardhi mkoani Tanga.

 

Mswiss huyo, Dk. George Hess, alidaiwa kumiliki kinyemela ardhi ya ufukwe wa Amboni uliopo Wilaya ya Muheza, mkoani Tanga.

 

Serikali imechukua hatua hiyo kwa maelezo kwamba Dk. Hess alikiuka Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999 kujipatia umiliki wa ardhi hiyo.

 

Dk. Hess anayeishi nchini Kenya, anadaiwa kumiliki ufukwe huo na kuuza viwanja kwa wageni na wazawa kinyume cha sheria za nchi.

 

Hatua hiyo ya Serikali imekuja baada ya JAMHURI kuandika habari kuhusu Dk. Hess na umiliki wa ufukwe huo, miezi mitatu iliyopita.

 

Chanzo cha habari kutoka ndani ya wizara hiyo kililiambia JAMHURI kuwa uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha watendaji wa wizara hiyo miezi miwili iliyopita, jijini Dar es Salaam.

 

“Tumekaa kikao na tumemwita Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Kaskazini, Doroth Wanzala na akatakiwa kutoa maelezo ambapo alikana kuhusika na utoaji wa kibali au hati ya umiliki wa ufukwe huo.

 

“Kikao kilikuwa ni kizito tumefanya hivyo kwa kuangalia mustakabali wa taifa kwani sheria iko wazi tulimsimamisha asifanye lolote katika eneo hilo na sasa tumeamua kumnyang’anya,” kimesema chanzo hicho.

 

Inaelezwa kuwa katika kikao hicho Wanzala alidai kupelekewa maombi ya kutaka Dk. Hess amilikishwe ufukwe huo na Ofisi Ardhi ya Halmshauri ya Walaya ya Muheza lakini alikaata kuyaidhinisha.

 

Chanzo hicho kilisema baada ya kukataliwa, Dk. Hess alianza kuuza viwanja hivyo bila idhini kwa madai kuwa yeye ni mmiliki halali wa kiwanja hicho.

 

Hata hivyo, JMHURI ilipomtafuta Msemaji wa Wizara hiyo, Abraham Nyantori,  ili kuzungumzia suala hilo ameeeleza kwamba kwa sasa hawezi kuzungumza lolote kuhusu hilo kwani watendaji wote wa wizara hiyo wanahudhuria vikao vya Bunge mjini Dodoma.

 

“Ni kweli tulikaa kikao kuhusu hilo lakini siwezi kuzungumza kwa sasa ndugu yangu, kwani makamishna wote ambao wangetoa majibu sahihi wako Dodoma, hata nikipiga simu sasa kuwauliza kuhusu hilo watanishangaa, wao wanazungumzia bajeti mie naleta mambo mengine, tutafutane kesho au baada ya bajeti nitakupa jibu kamili,” amesema Nyantori.

 

Dk. Hess, kupitia tovuti yake ya ambonibeach.com, alijitangazia ‘Jamhuri’ katika eneo hilo, kuwa ndiye mmiliki pekee Tanzania mwenye ufukwe, jambo ambalo ni kinyume cha Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999.

 

Sheria ya Mipango Miji namba 7 ya mwaka 2008 na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, inakataza mtu yeyote kumiliki ufukwe wa bahari bali fukwe zinapaswa kumilikiwa na umma. Lengo la kutungwa kwa sheria hiyo ni kuhakikisha fukwe hazihatarishi amani, ulinzi na usalama wa raia.

 

Pia sheria hizi zinalenga kupunguza uharibifu wa mazingira na kuwapa wananchi fursa ya kutumia fukwe za bahari kwa burudani, michezo na mambo mengine yenye tija nchini.

 

Mbali ya hilo, Dk. Hess pia kupitia tovuti hiyo, ametangaza kumiliki ardhi na kuiuza kinyume cha Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999 kifungu cha 20 (1), kinachokataza wageni kumilikishwa ardhi ikiwamo ya maeneo ya ufukweni.

 

“Kuepusha mkanganyiko, mtu asiye raia [wa Tanzania] hapaswi kupewa ardhi isipokuwa kama ni kwa malengo ya uwekezaji chini ya Sheria ya Uwekezaji ya Tanzania ya mwaka 1977,” kinasema kifungu hicho na kuongeza:

 

“Ardhi iliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji chini ya sehemu ndogo ya kwanza ya sheria hii inapaswa kutambuliwa, kutangazwa katika gazeti la Serikali na kukabidhiwa kwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ambacho kitatengeneza utaratibu wa haki ya mwekezaji kuitumia ardhi hiyo kuzalisha [si kuimiliki]”.

 

Tayari, Dk Hess ameuza viwanja tisa kwa watu mbalimbali kutoka nje ya nchi na wenyeji wapo waliojenga nyumba na wanaishi.

 

Mmoja wa watu waliouziwa viwanja hivyo ni raia wa Zimbabwe mwenye asili ya Kireno, Martin Perela, na tayari amejenga nyumba na anaishi katika eneo hilo.

 

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa Dk. Hess pamoja na sheria hiyo kukataza wazi, yeye anamiliki hati ya ardhi katika eneo hilo.

 

Hati ya mwanzo ya miaka 99 aliyopewa wakati wa ukoloni ameikabidhi kwa kampuni ya Amboni Plantation Limited shamba la mkonge la Kigombe.

 

Ramani ya shamba hilo hadi sasa inaonesha kuwa shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 12,000 lina hati moja na lilianzia katika Kijiji cha Kilale na kuishia Bahari ya Hindi.

 

Baada ya kuuza shamba hilo kwa kuligawa vipande viwili, alikabidhi hati kwa Amboni Plantation Limited, hivyo ambonibeach.com ikabaki bila hati.

 

Mbali ya ufukwe huo, uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa wageni wamekuwa wakimiliki fukwe nyingi katika maeneo mbalimbali ya nchi, hususan katika eneo la Kigamboni Dar es Salaam ambako wameuziwa na wenyeji.

 

Akizungumza na JAMHURI, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Galawa, alisema hana taarifa kuhusu umiliki na mgogoro wa shamba hilo.

 

Anasema hajawahi kuona au kusikia kuhusu mabadiliko ya matumizi ya shamba hilo, lakini ameahidi kufuatilia katika makabrasha ya Wilaya ya Muheza.

 

“Ninavyojua suala hili limevuka mipaka haliwezi kujadiliwa katika ngazi ya mkoa au wilaya hadi taifa, naomba uwasiliane na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, watakupa majibu,” amesema Galawa.

 

Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu, amesema hataweza kushughulikia suala hilo kwa kuwa ana majukumu mengine.

 

“Hivi nani aliyekupa hizi habari? Bwana mie sina habari na hilo kwa sasa naangalia vipaumbele vya maji, elimu na kilimo kwa kuwa wananchi hawajaleta malalamiko yao kwangu.

 

“Mie silijui wakileta nitalishughulikia na kutoa majibu lakini wasiliana na DED (Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya) atakuwa na majibu,” amesema Mgalu.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Ibrahm Mtovu, alipoulizwa alimtaka mwandishi kumpigia simu baadaye lakini muda waliokubaliana ulipofika alimpigia akapokea na kukata mawasiliano.

 

Alipopigiwa, Mtovu alipokea simu na baada ya mwandishi kujitambulisha alimtaka apige baada ya dakika tano.

 

Baada ya dakika 10 Afisa Ardhi wa Wilaya Muheza, Selemani Kanunge, alipiga simu na kuiambia JAMHURI kuwa mgogoro huo upo na ni wa muda mrefu.

 

Amesema suala hilo limefanyiwa kazi na Halmashauri ya Wilaya ya Muheza kupitia vikao vya Kamati ya Ardhi.

 

Waligundua suala hilo baada ya kusoma katika mtandao kuwa Dk. Hess anauza viwanja katika Ufukwe wa Amboni, wakamsimamisha na viongozi wa wizara wakafanya ukaguzi.

 

Amesema walimweleza utaratibu na akapeleka maombi katika Baraza la Ardhi la Wilaya na yakafanyiwa kazi kisheria.

 

Kanunge amesema walipeleka maombi yake kwa Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Kaskazini, Doroth Wanzala, naye akatoa kibali cha ardhi hiyo kupimwa.

 

Hata hivyo, amesema suala hilo bado lina mkanganyiko mkubwa kutokana na Dk. Hess kukataa kupima viwanja hivyo kwa ramani iliyoidhinishwa na wizara, badala yake anatumia yake.

 

Kanunge amesema Dk. Hess amekataa kupima viwanja hivyo kama inavyotaka ramani ya wizara, kwa kuwa haimruhusu kumikili ufukwe hivyo naye akatoa masharti kuwa atavipima mara tu akiruhusiwa kumiliki ufukwe.

 

Majibu ya viongozi wa wizara

Akizungumza na JAMHURI, Mkurugenzi wa Mipango Miji na Vijiji, Albina Burra, amesema hajui mabadiliko hayo ya ardhi.

 

“Mie sijui lolote kuhusu eneo hilo, sijapewa taarifa au dondoo zozote – ziwe za maneno au barua – kuhusu kubadilishwa kwa matumizi ya shamba hilo.

 

“Ninachoona mie ni kama wewe. Kuna mambo yanaendelea tu, naona nyumba zinajengwa na wala hakuna mchoro wowote uliopita kwangu, ili kupata majibu hebu muone Kamishna wa Ardhi, anaweza kuwa na majibu,” amesema Burra.

 

JAMHURI iliwasiliana na Kaimu Kamishna wa Ardhi, Bramsiden Sichone, ambaye naye alisema hana taarifa kuhusu suala hilo hadi atakapofanya utafiti na kumtaka mwandishi kuwasiliana na mtu ambaye angesaidia katika suala hilo.

 

Akizungumza na JAMHURI, mtumishi huyo wa wizara ambaye hakuta jina lake litajwe gazetini, amesema mgogoro huo ni mkubwa kutoka na kila kiongozi kupata kigugumizi kuushughulikia.

 

“Hapa hakuna kigugumizi kuzungumzia suala hili.

 

“Hii ni nchi yetu lazima tuoneshe uzalendo. Hapa kuna matatizo makubwa, hakuna kilichofanyika kule katika kupanga mipango miji kuna mambo matatu ya kufanyika.

 

“Kwanza unapima eneo zima, pili kujua viwanja vinakaaje na mwisho upimaji wa viwanja vyenyewe hapa hakuna kilichoafanyika.

 

“Sijui tunapata wapi ukakasi wa kusema hayo huyo bwana kakiuka sheria ya ardhi katika umiliki wala kubadilisha matumizi ya ardhi kinyume na sheria, kama ulivyoeleza mwanzo iko wazi kabisa.

 

“[Sheria inasema] watu wasio raia hawatapewa ardhi isipokuwa kupitia TIC.

 

“Si hivyo tu, hata kampuni za kigeni hawaruhusiwi kununua ardhi kutoka kwa wanakijiji bila kupata kibali kutoka TIC bali wanatakiwa kuwasiliana na Kituo cha Uwekezaji.

 

“Hata hawa TIC ni wateja wetu kama mteja mwingine. Wanakuja hapa na kununua ardhi kutoka kwetu, wao ndiyo wanawakodishia wawekezaji kwa muda maalumu utakaopangwa. Wakishindwa wanatakiwa kurudisha TIC,” amesema.

 

Amesema sheria na sera za ardhi zinatamka wazi halmashauri ina mamlaka ya kugawa ardhi hadi ukubwa wa eneo la ekari 500 ikizidi hapo ni kazi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, chini ya Kamati ya Ardhi ya Taifa inayoongozwa na Kamishna wa Ardhi Taifa.

 

“Ninalifahamu suala hilo, ndiyo kuna makosa makubwa, ndiyo maana umeambiwa uje kwangu kwa kuwa wanajua nalifahamu,” amesema.

 

JAMHURI imewasiliana na Meneja wa Amboni Beach, Steve Kabwoya, ambaye amekiri kuuza viwanja katika eneo hilo la ufukwe.

 

“Tumesitisha kuuza viwanja kutokana na mwanasheria wetu wa mwanzo kutudanganya kuwa tuna haki ya kuuza viwanja katika eneo hilo. Baada ya kubaini hilo tukasitisha, lakini sasa tumeamua kuwekeza katika hoteli,” amesema Kabwoya.

 

Amesema jambo hilo kwa sasa limesitishwa baada ya kubaini kuwa jambo hilo ni kosa kisheria.

 

Hata hivyo, alipoulizwa ni viwanja vingapi vilivyouzwa hadi sasa katika eneo hilo, alidai kuwa swali hilo ni gumu kwa sasa na kwamba anayetakiwa kulijibu ni bosi wake Dk. Hess, aliyedai kuwa amesafiri kikazi.

 

Yaliyoandikwa kwenye mtandaoTanga ni mkoa wa pili kuwa na bandari kubwa nchini Tanzania na ndiyo makao makuu ya raia huyo wa Uswisi anayemiliki Amboni Sisal Properties Ltd (ASPL).

 

ASPL inamiliki mashamba matatu ya katani ya Kigombe, Pongwe na Magoroto ambayo yanajishughulisha na kilimo na utalii. Shamba la Kigombe huzalisha tani 2,000 za katani kwa mwaka na ni moja ya mashamba makubwa nchini Tanzania.

 

Linauza nusu ya mkonge safi ya daraja la 3L na 3S katika maeneo 20 tofauti duniani.Katika wavuti wa kampuni hiyo, anajinadi kuwa anamiliki kiwanja cha ekari 360 za uwanja wa gofu wa kwanza Tanzania kwa uzuri na wenye makazi. Eneo hilo linafikika kirahisi kwa gari kutoka Tanga kwani muda wa dakika 40 kufika Pangani.

 

Anaendelea kujinadi kuwa barabara za Tanzania Bara kwenda Kenya ni nzuri na unaweza kuendesha gari kwa saa 10 kutoka Pangani hadi Nairobi na Mombasa hadi Pangani ni saa tatu.

 

Anasema kutoka Moshi hadi Pangani hutumia saa 4 na Pangani kwenda Arusha saa 5 na kutoka Dar es Salaam hadi Pangani ni saa tano na kujinadi kupitia mtandao huo kuwa ni karibu mno kutoka katika uwanja wa ndege wa Tanga, Kilimanjaro na Dar es Salaam.

 

Anasema katika eneo hilo atajenga uwanja wa ndege kwa kiwango cha moramu na utaruhusu ndege ndogo kutua.Kusini mwa shamba la Kigombe kutaendelezwa wastani wa mashimo 71, na viwanja 18 vya kuchezea gofu ambavyo vyote vitabuniwa na Tommy Fjastad.

 

Uwanja wa gofu ndiyo utakaokuwa pekee wenye nyumba zilizojengwa katika viwanja vya nusu au ekari moja zitakazokuwa zinatazamana na Bahari ya Hindi.

 

Katika tovuti hiyo, Dk. Hess amsema kutakuwa na huduma za hoteli, uwanja wa ndege binafsi, viwanja vya tenisi, maduka makubwa, klabu za usiku, bwawa la kuogelea na mengineyo.

 

“Nchi imebarikiwa kuwa na wanyamapori wengi, ina jiolojia ya ajabu, kreta, volcano,” anajinadi.

 

Maswali kwa ajili ya kuuza viwanjaKatika mtandao wake ameweka maswali na majibu ya kuvutia wateja wafike kununua viwanja kama ifuatavyo:-

 

Swali: Wapi viwanja vilipo?

Jibu: Kilomita 35 Kusini mwa Tanga kwenda pwani ya Barabara ya Pangani.

Swali: Ni jinsi gani unaweza kufika resort?

Jibu: Kwa kutumia gari kutoka Tanga dakika 40, Mombasa (saa 3), Kilimanjaro (saa 5), Dar es Salaam (saa 5).

Swali: Viwanja vilivyoendelezwa ni vipi?

Jibu: Ekari 360 kwa ajili eneo la gofu na ekari 200 vilivyopo ufukweni mwa bahari, ambavyo ni kwa ajili ya makazi ndani ya ekari 12,000 za zao la mkonge na za kilomita 8 ufukwe binafsi.

Swali: Ni viwanja vingapi vinapatikana katika eneo la makazi?

Jibu: Kunakadiriwa kuwa na viwanja 30 katika eneo la uwanja wa gofu na viwanja vikubwa kwa ajili ya makazi 50 ambayo yanakuwa kati ya ekari 3-5 mbele ya ufukwe wa bahari.

Swali: Kama nataka kujenga nyumba ni kiasi gani cha fedha kitakachotumika?

Jibu: Gharama za ujenzi wa nyumba, Tanzania ni dola za Marekani 40 kwa mraba wa futi moja.

Swali: Kama nitanunua kiwanja na kujenga nyumba naruhusiwa kupangisha?

Jibu: Ndiyo. Timu ya manejimenti itakusaidia kupangisha au kutoa mkataba wa kupangisha kwa watalii au watu binafsi.

Swali: Nani atakayejenga nyumba yangu?

Jibu: Unayo nafasi ya kununua ramani ya nyumba ya kuanzia vyumba vitatu au vinne kutoka kwa mkandarasi wetu au kuijenga mwenyewe.

Swali: Kama nina mkandarasi wa kujenga nyumba yangu mwenyewe ni gharama kiasi gani nitatumia hadi kukamilisha nyumba?

Jibu: Gharama za ujenzi Tanzania ni dola za Marekani 40 kwa mraba wa futi moja.

Swali: Je, kuna zuio la kuunda mchoro wa ramani ya nyumba niitakayo?

Jibu: Ndiyo. Nyumba lazima iwe aina ya ‘bungalow’ ikiwa na mapambo ya asili.

Swali: Je, naweza kununua nyumba bila kuhusisha uwanja wa gofu?

Jibu: Ndiyo unaweza kununua uwanja wa ufukwe kwa haki utakayo.