Kampuni ya Crown Lapidary ya jijini Arusha inayojihusisha na biashara ya madini imekumbwa na kashfa ya kutorosha madini yenye thamani ya dola za Marekani milioni 300 (shilingi zaidi ya bilioni 700), JAMHURI limebaini.

Madini hayo aina ya Green Garnet, yanatajwa kuwa na thamani kubwa kuliko aina nyingi za madini ya vito, ikiwamo tanzanite.

Tukio hilo ingawa lina muda sasa, limeishitua serikali, hivyo kuufanya uongozi wa juu wa nchi utoe maelekezo ya kufanyika kwa uchunguzi mara moja. Endapo itathibitika kuwa utoroshaji huo wa madini umefanyika, serikali itakuwa imekosa mapato ya mabilioni ya shilingi kutokana na kodi na tozo kama za Kodi ya Ongezeko la Thamani na mrabaha (asilimia 6).

Kutokana na hali hiyo, serikali imeunda kamati maalumu kuchunguza tuhuma hizo na tayari wahusika wameanza kuhojiwa.

Kampuni ya Crown Lapidary inamilikiwa na mfanyabiashara, Rajan Verma Ashok, ambaye biashara yake kuu ni madini ya vito, hasa tanzanite.

Tuhuma dhidi ya kampuni hiyo zimekuja wakati Serikali ya Awamu ya Tano ikiweka mikakati ya kupambana na utoroshwaji wa madini ambao kwa miaka mingi umeikosesha nchi mapato.

Taarifa zilizolifikia dawati la habari la gazeti hili kutoka ndani ya Wizara ya Madini na kuthibitishwa na vyanzo vya uhakika zinaeleza kuwa kamati hiyo imeundwa na wataalamu kutoka idara nyeti za serikali na Mkoa wa Manyara, ambako ndiko madini hayo yalikotoka, ndio unaoratibu uchunguzi huo.

Siri ilivyofichuliwa

 

Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo mbalimbali, utoroshwaji wa madini hayo ulifanyika kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2010 na 2011.

Madini hayo ya Green Garnet yalizalishwa kutoka kwenye mgodi namba 145 wenye leseni 0003601 unaomilikiwa na Anthony Ngoo katika machimbo ya Mirerani, wilayani Simanjiro, Manyara. Mgodi huo ni mahususi kwa uchimbaji wa tanzanite, lakini ilikuwa bahati tu kwa mwenye mgodi huo kupata madini hayo ya thamani.

Ngoo ambaye anaisaidia serikali kwenye sakata hili, anasema baada ya kuchimba mgodi kwa miaka 21 bila kuzalisha chochote, mwaka 2010 alipata Green Garnet katika mkondo wa tanzanite.

Wastani wa uzito wa madini hayo unatajwa kuwa ni kilo zaidi ya 10, na yanaelezwa kuwa yenye rangi na kiwango cha juu.

JAMHURI limezungumza na Ngoo na kusema: “Kutokana na ugeni wa madini hayo nilipata utata kidogo kuhusu soko lake, hasa kimataifa, na baada ya utafiti nilijulishwa kuwa mfanyabiashara Rajan Verma wa Crown Lapidary alikuwa na ufahamu kuhusu soko la kimataifa, pia ni mnunuzi wa madini hayo.”

Kwa sababu hiyo, alimkabidhi sehemu ya madini hayo na yakasafirishwa kwa magendo kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

“Siku hiyo Verma alitokea Mombasa, Kenya alikokuwa kwenye likizo ya sikukuu za mwisho wa mwaka. Alitumia ndege ya kukodi kufuata madini hayo na hakukuwa na ukaguzi wowote, aliniahidi kuwa angenilipa fedha zangu baada ya kumaliza likizo yake, lakini hakufanya hivyo,” amesema Ngoo.

Anajitetea kwa kusema ukweli wa hayo anayosema unaweza kuthibitishwa na mamlaka za nchi kwa kuchunguza kamera za usalama (CCTV) za Uwanja wa KIA siku ya tukio hilo.

Amesema walikubaliana na Verma kuwa angenunua madini hayo kwa shilingi milioni 15 kwa gramu moja.

“Aliniomba nifungue akaunti Benki ya Exim ili aniwekee fedha zangu baada ya kuuza madini. Bei halali ya madini hayo kwa wakati huo ilikuwa dola nyingi sana kwa gramu moja, makubaliano yakawa kwamba angenilipa Sh bilioni 150, vielelezo ninavyo, lakini hakufanya hivyo,” amesema Ngoo.

Anasema kiasi cha fedha kilichowekwa na mtuhumiwa kwenye akaunti hiyo ni Sh milioni 18 pekee. Pia alichoambulia ni gari aina ya Land Cruiser lenye namba T 856 ARH, ambalo nalo anasema umiliki wake hadi leo bado uko chini ya Kampuni ya Crown Lapidary Limited.

“Baada ya hapo akaanza fitina na danadana nyingi hadi nikapoteza kila kitu…nimeonewa sana,” amesema.

Hata hivyo, JAMHURI limeambiwa kuwa kwenye rekodi za Wizara ya Madini hakuna wakati wowote ambao Ngoo aliweza kulipa mrabaha au kodi nyingine, ingawa mwenyewe anadai kuwa kwa miaka zaidi ya 20 alichimba bila kuambulia kitu.

Ngoo amesema walipothamanisha madini aliyompa Verma kwenye soko la dunia kwa wakati huo, gramu moja iliuzwa dola 30 za Marekani, ambazo kwa sasa ni karibu Sh 70,000.

Amesema kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2013 hadi mwaka jana kwa kuwatumia watendaji wa vyombo vya dola wamemfungulia kesi mbalimbali, zikiwamo za uraia yeye na familia yake.

“Huyu bwana alianzisha vita kali dhidi yangu na kwa familia yangu, lengo likiwa nisiendelee kumdai. Nikazushiwa tuhuma kwamba mimi si raia wa Tanzania na kwa sababu hiyo sikustahili kuchimba madini kwa kutumia leseni kama raia.

“Nikanyang’anywa hati ya kusafiria na mwanangu (Davis) naye alinyang’anywa hati na kitambulisho cha taifa. Nikafunguliwa kesi ya madai ya Sh bilioni 2.5  katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha. Nikashindwa, lakini nikakata rufaa na kushinda katika Mahakama ya Rufani. Mahakama ikaamuru nilipwe na mtu aliyenifungulia kesi kiasi cha Sh milioni 258 lakini sikulipwa,” amesema.

Ngoo anadai kuwa kesi zote zilizofunguliwa dhidi yake zililenga kumdhoofisha ili asiendelee kudai mabilioni kutoka kwa Verma.

Ngoo anadai kuwa yeye ni Mtanzania aliyeishi nchini Kenya kwa muda mrefu, na huko alioa na kuzaa watoto kadhaa. Mmoja wa watoto wake, Davis, aliukana uraia wa Kenya na kuchukua uraia wa Tanzania. JAMHURI limeona nakala ya vyeti hivyo vya uraia.

Hata hivyo, taarifa za ndani kutoka Wizara ya Madini zinasema Ngoo si raia, japo yeye mwenyewe anatoa ushahidi wa kimaandishi na wa kinasaba wa kuthibitisha kuwa ni mzaliwa wa Tanzania, lakini aliishi Kenya kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa Sheria ya Madini, mtu ambaye si raia wa Tanzania haruhusiwi kumiliki leseni ya uchimbaji madini ya vito.

Akizungumza na JAMHURI, Waziri wa Madini, Doto Biteko, ameulizwa kuhusu sakata hilo na kujibu kwa ufupi: “Tuliache kwanza, naamini mamlaka husika zinalishughulikia. Kwa sasa tuache kazi ifanywe.”

Mkoani Manyara, ofisa kutoka Idara ya Madini aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa gazetini kwa kuwa si msemaji, amesema ni kweli Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti, ametuma kikosi kazi kufuatilia tuhuma dhidi ya Kampuni ya Crown Lapidary Limited.

Verma ametafutwa mara kadhaa kuzungumzia tuhuma hizi lakini kila alipopatikana alijibu kuwa hawezi kuzungumza kwa kuwa yuko kwenye vikao.

Taarifa zilizopatikana jijini hapa zinasema wamiliki na wafanyakazi wa kampuni hiyo walianza kuhojiwa wiki iliyopita.

Hii si mara ya kwanza kwa Kampuni ya Crown Lapidary kuhusishwa na utoroshwaji wa madini.

Desemba, 2015 raia wa India, Anurag Jain, alikamatwa katika Uwanja wa KIA akitorosha tanzanite yenye thamani ya dola 310,137 za Marekani. Madini hayo yalikuwa yakisafirishwa kwenda Hong Kong.

Jain alifunguliwa kesi ya jinai Na. 28/2015 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Moshi na kuhukumiwa Desemba 31, mwaka huo.

Katika utetezi wake mbele ya Hakimu Tiganga, Jain alikiri kutorosha madini hayo ambayo aliyapata kutoka Kampuni ya Crown Lapidary ya jijini Arusha.

Aliiambia mahakama kuwa Verma alimwahidi kuwa angemsaidia kupita vizuizi vyote katika Uwanja wa KIA bila kuyalipia tozo na kodi za serikali.

Siku ya tukio hilo Verma alimwagiza mmoja wa wafanyakazi wake aliyefahamika kwa jina la Luca kumsindikiza Jain kwenda KIA na kuhakikisha madini hayo yanavushwa kwa kuwatumia baadhi ya watumishi walioko kwenye mtandao wake wa kutorosha madini.

Mshitakiwa Jain alitiwa hatiani kwa makosa mawili na kuhukumiwa kulipa faini ya Sh milioni 5 kwa kila kosa.