Tarehe 16 Aprili 2025, Wizara ilipokea taarifa za uwepo wa tangazo katika mfumo wa picha mjongeo (Video Clip) lililosambaa kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii hapa nchini lenye maudhui yenye kuhamasisha matumizi ya dawa aina ya Semaglutide (Ozempic) kupunguza unene uliopitiliza.

Dawa hiyo ambayo ni maalumu kwa ajili ya matibabu ya ugonjwa wa kisukari ilidaiwa kupatikana kwenye kituo cha tiba kiitwacho Sky Heart Pharmacy Clinic kilichopo Manispaa ya Kinondoni, mkoa wa Dar es Salaam.

Wizara inapenda kuujulisha umma kuwa, dawa hiyo haijasajiliwa hapa nchini kwa ajili ya matumizi hayo.

Vilevile, maudhui ndani ya tangazo hilo hayakuwa na nia njema ya kuelimisha bali yalilenga kupotosha umma dhidi ya matumizi sahihi ya dawa ambapo ni kinyume na kifungu cha 96 cha Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba Sura, 219 pamoja na Mwongozo wa matangazo wa mwaka 2024 (Advertising, Health Communications and Medical Camps for Health Care Facilities and Services in Tanzania Mainland Guideline 2024) uliotolewa na Bodi ya Usajili wa Vituo Binafsi vya kutolea huduma za afya nchini.

Kufuatia hali hiyo na mapungufu yaliyobainika baada ya kufanyiwa ukaguzi, Waziri mwenye dhamana ya Afya ameelekeza Bodi na Mamlaka husika kuchukua hatua dhidi ya ukiukwaji huo ikiwemo kukifungia kituo hicho hadi hapo kitakaporekebisha mapungufu yake na kulipa faini kwa kukiuka Sheria na miongozo ya nchi.

Wizara inatoa rai kwa wamiliki wote wa vituo mbalimbali vya tiba hapa nchini kuacha mara moja vitendo hivyo na kuhakikisha kuwa wanazingatia matakwa ya Sheria kama yalivyoainishwa kwenye leseni na vibali vyao vya utoaji huduma.

Wizara haitasita kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya kituo chochote kitakachobainika kukiuka taratibu hizo.

Vilevile, Wizara inatoa wito kwa Wananchi wote kutoa taarifa Wizarani au kupitia taasisi za udhibiti kama Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Baraza la Famasi na Bodi ya Usajili Vituo Binafsi endapo watabaini uwepo wa matangazo ya dawa au huduma za afya yenye viashiria vya upotoshaji.