,đź“Ś Dkt. Biteko Asema Matumizi ya Teknolojia na Nishati Safi katika Shughuli za Madini Hayaepukiki

đź“Ś Serikali Yendelea Kufanya Mapinduzi Makubwa katika Sekta ya Madini

đź“ŚMaonesho ya Madini Geita kuwa ya Kimataifa

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuboresha, kuvutia na kuwakaribisha wawekezaji katika sekta ya madini ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Pato la Taifa kwa ujumla.

Dkt. Biteko ameongeza kuwa Rais Mhe. Dkt. Samia ametenga kiasi cha shilingi bilioni 118 kwa ajili ya kupeleka umeme kwa wachimbaji madini na kwa upande wa Kanda ya Ziwa kuna maeneo zaidi ya 90 ambayo yanatarajiwa kupelekewa umeme.

Dkt. Biteko ameyasema hayo leo Oktoba 5, 2024 mkoani Geita wakati akifungua Maonesho ya Saba ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini.

“ Naomba nichukue fursa hii kuwashukuru tena Watanzania wote kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali katika jitihada zake za kuendeleza sekta mbalimbali za kiuchumi.  Wajibu wa Serikali ni kuendeleza jitihada za kujenga na kuimarisha misingi thabiti ya uchumi katika kuvutia wawekezaji kwenye sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya madini, amesema Dkt. Biteko.

Ameongeza kuwa lengo la Sera ya Madini ya Mwaka 2009 ni kuhakikisha sekta hiyo inafungamanishwa na sekta nyingine za kiuchumi ili kuleta tija na maendeleo ya haraka kwa watu hasa kupitia ajira mbalimbali zinazotokana na shughuli za utafutaji, uchimbaji, uongezaji thamani na biashara ya madini nchini.

“ Ili sekta ya madini iweze kuongeza mchango wake kwenye uchumi wa nchi ni lazima ifungamanishwe kikamilifu na sekta muhimu za uchumi. Ufungamanishaji wa sekta ya madini na sekta nyingine za uchumi ni dhahiri kuwa utaliletea Taifa maendeleo kwa haraka kwa kuwezesha upatikanaji wa ajira pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi.” Amesema Dkt. Biteko.

Aidha, ametoa rai kwa Watanzania kujituma, kubadilisha mtizamo na kuwa mstari wa mbele kulinda na kutetea jitihada za Serikali za kuinua uchumi wa nchi.

Pia, Dkt. Biteko ameipongeza Wizara ya Madini kwa jitihada zake za kuanzisha uwepo wa akiba ya dhahabu, sambamba na kuipongeza Benki Kuu ya Tanzania.

Akizungumzia kaulimbiu ya maonesho hayo ya madini kwa mwaka 2024 yenye ujumbe usemao “Matumizi ya Teknolojia Sahihi na Nishati Safi katika Sekta ya Madini kwa Maendeleo Endelevu”.

Dkt. Biteko amesema kuwa matumizi ya teknolojia na nishati safi katika shughuli mbalimbali ikiwemo shughuli za madini hususan katika utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji na uongezaji thamani madini ni muhimu na hayaepukiki.

“ Katika kufanikisha hili matumizi sahihi ya teknolojia ni muhimu sana ili kufanya shughuli za uchimbaji hasa zinazofanywa na wachimbaji wadogo zifanyike kwa kuzingatia vifaa na teknolojia ya kisasa ili kufanya uchimbaji wao uwe na tija na unaozingatia utunzaji wa mazingira.” Amesisiza Dkt. Biteko

.

Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa kwa sasa bajeti ya wizara yake ni shilingi bilioni 232 kutoka shilingi bilioni 90 iliyokuwa awali ambapo wamejiandaa kujenga maabara kubwa ya kisasa ili wachimbaji wapate fursa ya kufanya utafiti wa madini badala ya kwenda nje ya nchi

“ Haya tunayafanya chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia na ambaye ameelekeza kununua mitambo 15 ya uchimbaji madini ambayo tutaigawa nchi nzima ikiwemo kwa vikundi vya uchimbaji vya akina mama na vijana.” Amesema Mhe. Mavunde.

Ameongeza kuwa mwaka 2017 sekta hiyo ilichangia asilimia 7.1 katika Pato la Taifa na sasa inachangia kwa asilimia 9.0 huku malengo ikiwa ni asilimia 10 ifikapo 2025.

Amefafanua “ Naamini ikifika mwakani tutafikia lengo kwa kuwa vipo viashiria vinavyoonesha jambo hili linawezekana na malengo yetu kwa mwaka huu wa fedha tutachangia shilingi trilioni 1 katika Mfuko Mkuu wa Serikali.”

Halikadhalika, Mhe. Mavunde amebainisha kuwa Serikali inafanya jitihada mbalimbali za kutatua changamoto katika sekta ya madini na kuwataka wachimbaji kuepuka migogoro kwa kuzingatia Sheria ya Madini.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martine Shigella amesema kuwa maonesho hayo yameshirikisha washiriki zaidi 800 na kuwa Mkoa wake utaendelea kuboresha maonesho hayo kuwa ya kitaifa.

Mhe. Shigella ameendelea kusema kuwa maonesho hayo yameleta maendeleo na mabadiliko makubwa na kuwa ambapo kipindi cha uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia alifuta leseni ambazo hazikuwa zinaendelezwa lakini kwa sasa Mkoa huo umetoa leseni kwa wachimbaji wadogo zaidi ya 3,106.

Akitaja mafanikio ya sekta ya madini mkoani humo Mhe. Shigella amesema “ Tumewezesha wanawake kumiliki leseni 30 kwa vikundi zaidi ya 20 vyenye wanachama zaidi ya 1000. Geita inazalisha dhahabu angalau kilo 5000 kila mwaka na tayari shilingi trilioni 2.2 zimeingia kwenye mzunguko wa fedha. Aidha, zaidi ya bilioni 65 zimetolewa Serikalini kupitia madini katika mkoa wetu,”

Kuhusu uwepo wa nishati ya umeme katika maeneo ya wachimbaji wadogo mkoani humo, Mhe. Shigella amesema tayari mkoa umepokea shilingi bilioni 7 na tayari miradi 52 inaendelea kutekelezwa ili kufikisha nishati ya umeme kwa wachimbaji.

Naye, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Kilumbe Ng’enda amesema kuwa Kamati inaridhishwa na kazi inayofanywa na sekta ya madini ikiwemo namna inavyochangia Pato la Taifa pamoja na wachimbaji wadogo kuchangia asilimia 40 katika pato hilo.

“ Tunapongeza utulivu uliokuwepo katika sekta ya madini na wachimbaji, sasa tunaipongeza Serikali na Waziri na tunaomba muendelee kusimamia utulivu huu.” Amesema Mhe. Ng’enda.

Vilevile, Rais wa Shirikisho la Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA), Bw. John Bina ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha sekta ya madini nchini na kusema kuwa wachimbaji wa madini wote wameazimia kuendelea kuiuzia Benki Kuu dhahabu kwa asilimia 20.

Makamu wa Rais wa Kambuni ya Uchimbaji Madini ya Dhahabu ya Geita (GGM), Simon Shayo amesema kuwa matumizi ya teknolojia sahihi kwa ajili ya uchimbaji madini na nishati safi ni masuala yanaoungwa mkono na Kampuni yake ambayo itaendelea kushirikiana na Serikali katika kukuza sekta ya madini nchini.

“ Tunafarijika kwa kuendelea kuwa wachangiaji kinara wa mapato katika sekta ya madini na mafuta nchini Tanzania na tutaendelea kuwa mbia wa maendeleo.” Amesema Bw. Shayo.

Manufaa ya Maonesho hayo yanatajwa kuwa ni kuwakutanisha wadau na mifuko ya hifadhi ya jamii, kuongeza kipato katika mkoa, kuvutia watembeleaji hadi kufikia 25,000, kukutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya madini wakiwemo wafanyabiashara, wawekezaji, Vyama vya Wachimbaji Madini, Mashirika ya Kimataifa na Asasi za Kiraia na washirikimbalimbali kutoka nje ya nchi.

Awali akiwa Mkoani Geita, Dkt. Biteko amezindua nyumba sita za Maafisa wa Jeshi la Polisi zilizojengwa kwa ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Dhahabu ya Geita (GGM) mkoani kwa lengo la kuboresha makazi ya Maafisa wa Jeshi la Polisi pamoja na kuimarisha ulinzi wa raia na mali zao.

Please follow and like us:
Pin Share