WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amesema serikali imekamilisha upembuzi yakinifu wa awali kwa ajili ya upanuzi wa Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria wa Tinde-Shelui kwenda zaidi ya vijiji 30 vya wilaya za Shinyanga na Iramba.

Alisema utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2025/2026 na utafanyika kwa kipindi cha miezi 12.

Aweso alitoa ufafanuzi huo wakati akijibu Swali la Msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Christina Mnzava (CCM) alitaka kufahamu lini serikali itapeleka maji ya Ziwa Victoria katika Kata ya Usanda, Halmashauri ya Shinyanga.

Aweso alisema, “Mradi huo utatekelezwa kwa utaratibu wa kusanifu na kujenga yaani ‘design and build”’.

Alisema mradi huo unatarajia kunufaisha wananchi 138,839 waishio kwenye kata 12 za wilaya za Iramba na Shinyanga, ikiwemo Kata ya Usanda.

Katika swali la nyongeza, Dk Mnzava alisema awamu ya kwanza ishaanza kutekelezwa na tangi la maji lipo kubwa lakini linahudumia kijiji kimoja tu, hivyo lini kutaanza kusambazwa maji katika vijijini vingine.

Aweso alisema: “Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kuleta maji Shinyanga kutoka Ziwa Victoria na sasa tupo hatua za mwisho kumpata mkandarasi kusambaza maji katika vijiji vyote”.