Serikali imeitaka jamii kuhakikisha inapinga ukatili wa aina zote ili kufikia malengo ya kuwa na kizazi chenye usawa kati ya wanawake na wanaume.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Prudence Constantine, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yatakayofanyika Machi 8, mwaka huu.

Amesema kuwa lengo la maadhimisho ya siku hiyo ni kutathmini utekelezaji wa hatua za kufikia usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake kiuchumi, kijamii na kisiasa katika kufikia maendeleo endelevu.

Maadhimisho haya pia yanatoa fursa ya kuelimisha jamii kuhusu jitihada mbalimbali zilizofanywa na jamii, serikali, asasi za kiraia, sekta binafsi na wadau wengine katika kukuza hali ya mwanamke wa Kitanzania.

Kadhalika, katika kuadhimisha siku hiyo wadau wanapata fursa ya kubainisha upungufu na mbinu za utatuzi wa changamoto zilizopo.

“Katika miaka ya 1990 wanawake walikuwa wanafanya kazi nyingi na kupata ujira mdogo chini ya mazingira ya unyanyasaji, hawakupewa kipaumbele ikilinganishwa na wafanyakazi wanaume,” anasema.

Maadhimisho ya kitaifa yalizinduliwa Februari 27, mwaka huu katika kongamano lililofanyika jijini Dodoma, mgeni rasmi akiwa Spika wa Bunge mstaafu, Anne Makinda.

Constantine amesema serikali imeendelea na jitihada za kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa kuanzisha mfuko wa uwezeshaji kiuchumi, ikiwa ni pamoja na mfuko wa maendeleo ya wanawake wenye masharti nafuu ambao umesaidia kutoa mikopo nafuu na mafunzo ya stadi za biashara kwa wajasiriamali wanawake.

“Wizara inahakikisha kutumia maadhimisho haya kwa kuandaa makongamano na majukwaa mbalimbali ili kujadili na kuibua kero zinazokwamisha maendeleo na ustawi wa wanawake na kuyatafutia ufumbuzi yakiwamo matatizo ya maji na uchumi duni,” anasema.

Ameongeza kuwa tangu mwaka 2015/16 hadi 2018/19 serikali imetoa kiasi cha Sh bilioni 28.8 ambazo zimesaidia vikundi vya wanawake 13,691 na kufanya idadi ya wanawake wajasiriamali walionufaika na fedha hizo kufikia 883,724 ukilinganisha na wanawake 12,842 kwa mwaka 2013/14.

Aidha, serikali imewezesha wanawake wajasiriamali kushiriki katika maonyesho ya biashara mbalimbali za kitaifa na kimataifa kwa mwaka 2017/18, ambapo wanawake wajasiriamali 1,183 kutoka katika mikoa yote 26 wamenufaika na fursa hiyo.

Kaulimbiu ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka 2020 ni ‘Kizazi cha Usawa kwa Maendeleo ya Tanzania ya Sasa na Baadaye.’