πŸ“Œ Anadi soko la mazao jamii ya mikunde India

πŸ“Œ Mnada mazao ya kunde mtandaoni waboresha biashara ya kimataifa

πŸ“Œ Biashara kati ya Tanzania na India kufikia dola bilioni 7.9

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Serikali ya Tanzania imejidhatiti kuboresha na kuimarisha sekta ya kilimo kwa kuja na mipango kadhaa yenye lengo la kuongeza fursa kwa wakulima nchini.

Dkt. Biteko amesema hayo jijini New Delhi, India wakati akishiriki mkutano kuhusu masuala ya mazao jamii ya mikunde.

β€œTunaongeza uwekezaji katika utafiti na kuboresha upatikanaji wa teknolojia za kisasa za kilimo ambapo kila afisa wa ugani nchini amepewa vifaa vyote muhimu ikiwemo pikipiki na kompyuta ili kutoa huduma nzuri na kwa wakati kwa wakulima wetu.” Amesema Dkt. Biteko.

Amesema Serikali pia imeboresha shughuli za usafirishaji wa bidhaa ikiwa ni pamoja na kurahisisha michakato ya uuzaji mazao “Tanzania inaendeleza ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ambayo itaimarisha usafirishaji wa bidhaa yenye urefu wa takribani kilomita 500 kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi Dodoma ambayo imekamilika na na inatumika.

Vilevile, amesema kupitia mradi wa BBT (Building a Better Tomorrow) Serikali imewezesha vijana kwa kuwapa ardhi, fedha na upatikanaji wa masoko sambamba na kuongeza huduma za kifedha za kidijitali.

Aidha, Dkt. Biteko amesema β€œIndia ni soko muhimu kwa mazao jamii ya kunde kutoka Tanzania na tunaweza kupata mafanikio makubwa zaidi. Leo nawaalika wawekezaji kutoka India na nchi nyingine duniani kuja kuwekeza katika sekta ya kilimo ya Tanzania kuanzia uzalishaji wa kisasa wa soya hadi uwekezaji katika mifumo ya usimamizi wa mavuno,”

Akizungumzia maendeleo ya sekta mazao jamii ya mikunde, amesema kuwa mwaka 2023, Tanzania ilizalisha takriban tani 250,000 za mbaazi, ikiwa ni ongezeko la asilimia 56 ikilinganishwa na mwaka 2018.

Inakadiriwa ifikapo mwaka 2030 Tanzania itakuwa na ukuaji mkubwa katika Pato la Taifa kupitia Kilimo, ambapo mauzo ya maharage mekundu, mbaazi na choroko yanatarajiwa kufikia dola bilioni 1.47, dola milioni 84 na dola milioni 115. Aidha, ili kufikia uwezo huo, Tanzania imeweka mikakati ya kukuza sekta ya mazao jamii ya kunde kupitia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani kwa wakulima kusajiliwa, kuboresha mbinu za kilimo na teknolojia, kuhakikisha ubora na viwango vya mazao kulingana na mahitaji ya soko.

Pamoja na hayo Dkt. Biteko amesema β€œMazao jamii ya kunde nchini Tanzania yanauzwa kupitia mnada wa mtandaoni ambao unatoa fursa kwa wafanyabiashara kupata taarifa kuhusu mizigo iliyohifadhiwa katika ghala lililosajiliwa,”

Amesisitiza β€œMfumo huu unahakikisha uwazi, ufuatiliaji na ufanisi katika biashara ya kimataifa. Mwaka 2024 pekee kupitia mfumo huu, wakulima wa Tanzania walipata zaidi ya dola milioni 91.31 kutoka katika biashara ya mbaazi, dengu na maharagwe ya soya, ubunifu huu si tu unaimarisha ushindani wetu bali pia unafungua fursa mpya za ushirikiano,”

Kufuatia hali hiyo,kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili kimeongezeka na kufikia dola bilioni 7.9 kwa mwaka wa fedha 2023/2024. Pia, mwaka 2023 mauzo ya mbaazi kutoka Tanzania kwenda India yalifikia tani 186,447 yenye thamani ya dola milioni 139.1.