Wizara ya Nishati imekabidhi kibali cha ujenzi  wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki kwa kampuni ya EACOP Tanzania ambapo itaanza utekelezaji wa ujenzi wa kipande cha kutoka Mtukula hadi  Chongoleani Mkoani Tanga.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi Kibali hicho Waziri Wa Nishati Januari Makamba amesema kwamba mchakato wa kukabidhi kibali hicho umeanza muda mrefu kwani ulipaswa kuzingatia masuala ya utunzaji wa mazingira pamoja na haki za binadamu

Amesema kwamba tayari mradi umeanza kutekelezwa kwa kulipa fidia kwa makazi wa maeneo ambayo yamepitiwa na mradi huo katika mikoa minane ambapo kaya 9898 wameshalipwa fidia huku kati yake watu  390 ardhi yao itachukuliwa nakwamba wamekubali kujengewa nyumba za kisasa.

“Tumelipa fidia shilingi bilioni 29,mradi huu katika baadhi ya maeneo umeanza kutekelezwa mfano kununua vifaa,kuanza ujenzi wa vituo vya kuhifadhia mafuta mkoani Tanga,kwahiyo tunatarajia mradi huu ulete ajira nyingi za mojakwa moja lakini pia ajira za kutoa huduma kama vile hoteli, hivyo Watanzania wachangamkie fursa hiyo” amesema Waziri Makamba

Bi. Wendy Brown Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya EACOP Tanzania alipokuwa akizungumza mara baada ya kumpuni hiyo kupewa Kibali cha Ujenzi wa Bomba la mafuta Ghafi February 21, 2023.

Aidha ameitaka Malaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ( EWURA) ambayo imepewa asilimia 15 ya usimamizi wa mradi huo kwenye kampuni ya EACOP kuhakikisha inatangaza fursa zilizopo pamoja na kusimamia ipasavyo sheria ya Local Content ambayo inatoa fursa kwa wazawa kushiriki katika ujenzi wa bomba hilo la mafuta ghafi la Afrika Mashariki.

Awali akizungumza Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Dkt. James Andilile kampuni ya EACOP imepewa zabuni hiyo kutokana na kukidhi masharti ya kimkataba ikiwemo kuzingatia masuala ya utunzaji wa mazingira,Athari za kiubinadamu,uwezo wa kitaalamu na kifedha kwa ajili ya kutekeleza mradi.

“Ujenzi huu wa kipande cha kutoka Mtukula hadi Chongoleani Mkoani Tanga una urefu wa kilomita 1147 , sisi kama EWURA tuna matumaini kwamba kampuni ya EACOP itaendelea kuzingatia yote tuliyokubaliana kabla na baada ya ujenzi wa Bomba hili”amesema Dkt Andilile.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omary Mgumba akizungumza kwa niaba ya wakuu wa mikoa wenzake ambapo Mradi huo umepita amesema kwamba watahakikisha wamesimamia vizuri miundombinu ya mradi huo kwa kutumia Jeshi la Akiba huku wakiiomba serikali kujenga vituo vya polisi katika vituo vya kuhifadhia mafuta ghafi ili kuhakikisha ulinzi na usalama.

Nae Naibu Mkurugenzi wa Kampuni ya EACOP Tanzania ambayo imekabidhiwa Kibali cha ujenzi wa  mradi huo amesema kwamba kampuni hiyo itahakikisha inazingatia makubaliano ya mkataba nakuhakikisha ujenzi huo una kamilika kwa wakati.

Mikoa  nane ambayo bomba hilo litapita ni pamoja na Tanga,Manyara,Dodoma,Singida,Tabora,Shinyanga,Geita,Kagera,ambapo katika maeneo hayo fursa za ajira kwa wananchi  zitapatikana kwa wingi.