Serikali imeiomba Benki ya Dunia kusaidia rasilimali fedha ili kuwezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na serikali.

Ombi hilo limetolewa hivi karibuni jijini New York nchini Marekani na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alipokutana na viongozi wa juu wa Benki ya Dunia.

Katika ombi lake, Mpango aliishauri Benki ya Dunia kuacha kufadhili miradi midogo midogo hapa nchini wakati ipo miradi mikubwa inayohitaji pesa nyingi kuitekeleza.

Ushauri huo aliutoa mjini Washington DC nchini Marekani baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa taasisi hiyo ya fedha anayesimamia Kanda ya Afrika, Hafez Ghanem.

Wakati wa mkutano huo, Dk. Mpango aliwasilisha miradi mbalimbali ambayo serikali inatekeleza na akaiomba benki hiyo msaada wa rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wake ambao utahitaji matrilioni ya shilingi.

Rais Dk. John Pombe Magufuli amekuwa akisisitiza kwamba miradi hii mikubwa na ya kimkakati lazima itekelezwe hata kama ni kwa pesa za ndani peke yake, kwani taifa lina fedha za kutosha kufanya hivyo. Utekelezaji wa miradi hiyo kwa wakati ni muhimu kufanikisha ajenda za maendeleo ya Serikali ya Awamu ya Tano, hasa ujenzi wa viwanda ili kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Miradi ambayo Dk. Mpango aliwasilisha Benki ya Dunia ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ujenzi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere katika Mto Rufiji mkoani Pwani, mradi wa ujenzi wa reli kutoka Mtwara kwenda Mbamba Bay na miradi ya Mchuchuma na Liganga mkoani Ruvuma ambako kuna rasilimali kubwa ya madini ya chuma na makaa ya mawe.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Wizara ya Fedha, Benny Mwaipaja, Dk. Mpango alimwambia Ghanem kuwa kwa sasa Tanzania inatekeleza miradi mikubwa na inayohitaji fedha nyingi kuikamilisha, hivyo ni vema Benki ya Dunia ikajielekeza katika kusaidia utekelezaji wa miradi hiyo. 

“Nisingependa kuona taasisi kubwa ya kifedha kama Benki ya Dunia inakimbilia kufadhili utekelezaji wa vimiradi vidogo vya kujenga hosteli au hoteli za nyota tano. Kwa sasa nchi yetu inahitaji kujikita zaidi katika miradi mikubwa ambayo itawaletea maendeleo ya haraka wananchi wetu,’’ taarifa hiyo iliyoko kwenye tovuti ya Wizara ya Fedha inamnukuu Mpango akisema.

Tangu uhuru, Benki ya Dunia imekuwa miongoni mwa wafadhili wakubwa wa maendeleo nchini na ni kati ya taasisi za fedha duniani ambazo zimekuwa zikiisaidia Tanzania kwa namna tofauti katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na ujenzi wa taifa.

Kwa upande wa mikopo, ambayo mingi huwa ni nafuu, takwimu za benki hiyo zinaonyesha kuwa mwaka 2015 Tanzania ilikopeshwa dola za Marekani milioni 865 ambazo kwa sasa ni karibu Sh trilioni 1.99. Mwaka uliofuata kiasi hicho kilipungua kwa karibu asilimia nne na kufika dola milioni 827 kabla ya kuongezeka maradufu mpaka dola milioni 1,206 mwaka 2017.

Mwaka 2018, mikopo yenye riba ndogo ya Benki ya Dunia kwa Tanzania ilipungua kwa asilimia 58 hadi dola milioni 505 ambayo ni sawa na Sh trilioni 1.16.

Kwa takwimu zilizopo kwenye tovuti ya ofisi za Benki ya Dunia nchini, kwa mwaka huu mikopo iliyokuwa imetolewa kwa Tanzania ilikuwa na thamani ya dola milioni 9, ambazo ni sawa na Sh bilioni 20.7 tu. 

Walipoulizwa kuhusu hali hii, viongozi wa benki hiyo hapa nchini walisema kwamba sera ya upatikanaji wa taarifa ya benki hiyo huwa hairuhusu kila kitu kuwekwa wazi.

Jijini Washington, Dk. Mpango alimshukuru Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika, Ghanem kwa kukubali maombi mengi kutoka Tanzania ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo. 

Pia waziri huyo ameiomba taasisi hiyo iwatume wataalamu wake nchini kuainisha miradi mikubwa ya kimkakati inayotakiwa kutekelezwa kati ya sekta binafsi na umma chini ya utaratibu wa PPP (public-private partnership) badala ya taasisi hiyo ya fedha duniani kutaka serikali itekeleze miradi midogo isiyo na tija kubwa kwa taifa.

“Nimewahimiza kwamba kama kweli tunataka kutekeleza kwa ufanisi mpango wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) ni lazima tutekeleze miradi mikubwa, na kwa kuanzia, wangekuja kuanza kutekeleza ule mradi wa kujenga reli ya kutoka Mtwara kwenda Mbamba-Bay, Mchuchuma hadi Liganga,” amesema Mpango. 

Ameongeza kuwa ukamilishaji wa ujenzi wa reli hiyo utasaidia kuchochea kwa kasi maendeleo ya nchi kutokana na rasilimali zilizopo katika maeneo inapopita reli hiyo. 

Ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati hautetereki, serikali imekuwa ikiitengea fedha kutoka kwenye bajeti zake za ndani kila mwaka na tayari Dk. Mpango ametabainisha kwamba hilo litafanyika pia kwenye mwaka wa fedha ujao.

Akilihutubia Bunge wiki iliyopita, Dk. Mpango alisema utekelezaji wa miradi hiyo ni miongoni mwa vipaumbele katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2020/21 na Bajeti ya Serikali kipindi hicho ambapo serikali inatarajia kutumia takriban Sh trilioni 12.69 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Hilo ni ongezeko la asilimia 3.68 kulinganisha na kiasi cha takriban Sh trilioni 12.45 ambacho ni kwa ajili ya shughuli za maendeleo katika bajeti ya serikali ya mwaka huu. Katika bajeti ijayo, serikali imepanga kukusanya na kutumia kiasi cha Sh trilioni 34.36 ukilinganisha na Sh trilioni 33.11 mwaka wa fedha wa 2019/20 ambao nusu yake inaisha mwezi ujao.