Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Isdor Mpango ametoa maelekezo kwa Taasisi ya Watumishi Housing Investments(WHI) kuzingatia ubora na viwango stahiki wakati wa kujenga Nyumba za makazi ya Watumishi ili kuendana na thamani ya fedha na kuwaepushia wanunuzi wa nyumba hizo gharama za marekebisho na maboresho zaidi.
Dkt.Mpango ameeleza hayo leo December 11,2024 Jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Mpango wa makazi kwa watumishi wa Umma Njedengwa unaolenga kuboresha hali ya makazi kwa wafanyakazi wa serikali na kutoa fursa kwa watumishi hao kuishi katika mazingira bora yatakayoleta tija katika maeneo ya kazi.
“Ili mpango huu uweze kufikia malengo yake na kuwa na manufaa kwa watumishi, ni muhimu vigezo na masharti ya upatikanaji wa nyumba kwa watumishi wa umma viheshimiwe na kuzingatiwa,upokeaji, uchambuzi wa maombi na uthamini wa nyumba hizo vifanyike kwa haki na kuzingatia uhalisia,nasisitiza juhudi za makusudi zifanyike ili watumishi wa ngazi za chini na kati wapewe kipaumbele katika upatikanaji wa nyumba hizo, “amesisitiza.
Dkt. Mpango pia ametumia nafasi hiyo kuziagiza Halmashauri zote nchini kutoa maeneo ya ujenzi wa Nyumba za wafanyakazi jirani na wanapofanyia kazi ili kurahisisha katika utendaji kazi wao.
” Ninatambua changamoto kubwa ya upatikanaji wa viwanja vya kutosha katika maeneo mengi, hususan maeneo ya mijini,ili kuufanya Mpango huu kuwa endelevu, ninashauri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi na Halmashauri husika kufanyia kazi suala hili ili kuhakikisha upatikanaji wa maeneo ya ujenzi wa nyumba za watumishi yaliyo karibu zaidi na sehemu za kazi, na yanayozingatia mahitaji ya msingi ya watumishi na familia zao, hivi sasa na kwa wakati ujao, “amesema
Amesema kuwa uzinduzi wa nyumba za watumishi ni ishara ya Serikali kujali na kuheshimu mchango wa watumishi wa umma, na ni hatua muhimu katika kukuza ustawi wao na familia zao hivyo kuchangia maendeleo ya taifa na hivyo kuwataka watumishi na wananchi ambao watapata nafasi ya kununua nyumba hizo kuzitunza ili zibaki katika hali ya ubora kadri inavyowezekana.
“Matunzo ya nyumba hizi yajumuishe miundombinu na mazingira yanayozunguka eneo la nyumba,nawasihi kupanda miti na maua ili kuleta mandhari nzuri na pia kuhakikisha usafi muda wote,angalieni pia uwezekano wa kushirikisha taasisi au watu binafsi wenye utaalam wa kupendezesha makazi (landscaping),”amesisitiza Dkt.Mpango.
Aidha ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha Watumishi Housing Investments kupanda miti katika maeneo yote inakotekelezwa miradi ya ujenzi wa nyumba za makazi kwa watumishi wa umma ili kuhifadhi na kutunza mazingira na kuweka angalizo kuhusu ujenzi wa nyumba za makazi ya watumishi kuzingatia uwepo wa viwanja vya michezo, maeneo ya kupumzikia na huduma nyingine za jamii kama elimu, afya na huduma za mahitaji kama maduka na maeneo ya ukusanyaji wa taka.
Sambamba na hayo ameiagiza WHI kitoa kipaumbele kwa watumishi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa ambayo iko jirani na Njedengwa wakati wa uuzaji wa Nyumba zitakazoendelea kujengwa hapa Dodoma kutokana na uhaba mkubwa wa nyumba za makazi kwa ajili ya madaktari na wauguzi hali itakayowawezesha kutoa huduma kwa Watanzania kwa wakati.
Mbali na hayo amesema, “kwa kuwa mahitaji ya nyumba nchini bado ni makubwa, ninawaachia Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na Watumishi Housing Investments changamoto ya kutafuta vyanzo vingine ya fedha kwa ajili ya upanuzi wa mradi huu,mbali ya fedha kutoka Serikalini, angalieni uwezekano wa kupanua vyanzo vya upatikanaji wa fedha kupitia Hatifungani, Makampuni ya Bima, Wadau wa Maendeleo, Taasisi za kifedha na Uwekezaji kutoka Taasisi nyingine na hata mtu mmoja mmoja, “amesema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Investments (WHI) Dkt.Fred Msemwa ameeleza kuwa taasisi hiyo ya Serikali iliyoanzishwa mwaka 2014 kwa mujibu wa sheria ya Makampuni (Cap 212) na inalenga kutekeleza Mpango wa Makazi kwa Watumishi wa Umma pamoja na wanachama wa mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Ameeleza kuwa Taasisi hii inachukua hatua muhimu katika kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa kama yalivyoainishwa katika Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Makazi (2000), Dira ya Maendeleo ya 2025, na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya mwaka 2030.
Amesisitiza kuwa mpango huo
utasaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa makazi kwa watumishi na kutoa motisha kwa wataalamu mbalimbali kuendelea kutoa huduma bora katika sekta za afya, elimu, na usalama.
Ameeleza kuwa uwekezaji huo unafanyika kupitia Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja katika Milki, maarufu kama WHI Real Estate Investment Trust Fund (WHI-REIT) unaotoa fursa kwa watu mbalimbali, hasa mifuko ya hifadhi ya jamii, kushiriki katika uwekezaji wa sekta ya makazi na kumwezesha mteja kupata nyumba bora.
Mtendaji Mkuu huyo wa WHI, amesema kuwa nyumba si tu bidhaa bali ni huduma muhimu inayoweza kuboresha maisha ya watumishi na kueleza kuwa lengo kuu la WHI ni kuhakikisha kuwa watumishi wa umma wanapata makazi bora.
“Nyumba ni huduma, si bidhaa,tunapojenga nyumba kwa ajili ya watumishi wa umma, hatuendi tu kwa mtindo wa kuuza bidhaa, bali tunatoa huduma ambayo inawafaa watumishi, kuwapunguzia changamoto za makazi na kuboresha ustawi wao,hii ni sehemu ya mfumo wa uwekezaji wa fedha, ambapo watumishi wanapata nyumba bora na pia wanapata fursa ya kuwekeza mali zao kupitia programu zetu,”amesema
Amefafanua kuwa ili kuhakikisha utekelezaji wa mipango ya ujenzi wa nyumba unakuwa wa tija, WHI imejizatiti kudhibiti mnyororo wa ujenzi wa nyumba.
“Tumeboresha mifumo yetu ya utekelezaji na kudhibiti mnyororo wa ujenzi,hii inahakikisha kuwa nyumba zinazojengwa zinalingana na viwango vya ubora zinazoendana na wakati na pia zinapatikana kwa bei rafiki kwa watumishi wote,” amesema.
Ameongeza kuwa usimamizi bora wa ujenzi wa nyumba ni muhimu ili kuepuka ucheleweshaji na kupunguza gharama za ujenzi, jambo ambalo linasaidia watumishi wa umma kumiliki nyumba zao kwa urahisi na kwa wakati.
“Kwa kudhibiti mnyororo wa ujenzi, tunahakikisha kwamba gharama za ujenzi zinakuwa chini, na hivyo kutoa fursa kwa watumishi wetu kupata nyumba nzuri kwa bei nafuu, mpango wa Watumishi Housing umejizatiti kutoa suluhisho la muda mrefu kwa watumishi wa umma, na pia ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya kuboresha makazi ya wafanyakazi, “amesisitiza na kuongeza;
“Kwa kupitia Watumishi Housing, tunatoa suluhisho la makazi kwa watumishi wa umma, na tunahakikisha kuwa nyumba zinazojengwa zinaendana na mahitaji ya watumishi wetu. Hii itasaidia kupunguza changamoto za makazi na kuongeza tija katika sekta mbalimbali za huduma za jamii,” amesema.
Amesisitiza kuwa Watumishi Housing Investments itaendelea kutoa mchango mkubwa katika kuboresha makazi ya watumishi wa umma na kusaidia kufikia malengo ya Serikali ya kuimarisha ustawi wa jamii.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi ,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora George Simbachawene amesema WHI ni taasisi ya Serikali iliyoanzishwa mwaka 2014 chini ya sheria ya Makampuni (Cap 212) kwa ajili ya kutekeleza Mpango wa Makazi kwa Watumishi wa Umma na wanachama wa mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambayo ni matarajio katika malengo ya kitaifa na kimataifa kama yalivyoainishwa katika Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Makazi (2000), Dira ya Maendeleo ya 2025, na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030.
Amesema Uwekezaji unafanyika kupita Mfuko wa uwekezaji wa pamoja katika milki(WHI Real Estate Investment Trust Fund au WHI-REIT) ambapo Wawekezaji wa awali katika WHI-REIT ni mifuko ya hifadhi ya jamii ikiwemo Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), NHC, na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Ameeleza kuwa mfuko huo umetekekeza ujenzi wa zaidi ya Nyumba 1000 kwa mikoa 18
na kwamba mpango wa WHI unahusisha uwekezaji katika sekta ya makazi kwa ajili ya watumishi wa umma, ambapo unalenga kutoa fursa kwa wafanyakazi wa serikali kuishi katika makazi bora kwa kuweka taratibu rafiki zinazowawezesha wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii, kumudu kununua nyumba kwa kutumia mishahara yao.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule ameeleza kuwa kukamilika kwa makazi hayo kutaenda sambamba na juhudi za kuboresha mazingira ya mji wa Dodoma kwa kupanda miti katika maeneo mbalimbali ya makazi hivyo kuufanya mji kuwa wa kijani, safi na wenye mandhari bora.
“Uzinduzi wa nyumba hizi ni ishara ya kujali na kuthamini mchango wa watumishi wa Serikali,hatuwezi kujivunia nyumba nzuri pekee bila kuboresha mazingira ya nyumba hizi,hapa Dodoma, tunaendelea na juhudi za kupanda miti kwa wingi ili kuboresha mandhari ya mji wetu na kuwa na mazingira rafiki kwa familia za watumishi na wananchi kwa ujumla,” amesema
Mkuu huyo wa Mkoa ameeleza kuwa upandaji miti katika maeneo ya makazi ya watumishi ni sehemu ya mikakati ya mkoa kuhakikisha kuwa Dodoma inakuwa mji wa kijani, ambapo miti itasaidia kupunguza mabadiliko ya tabianchi, kuboresha hewa, na kuleta mandhari ya kuvutia.
“Tunapozindua nyumba za watumishi, tunafanya kazi kubwa ya kuboresha mazingira yetu,tumejipanga kupanda miti katika maeneo ya shule, hospitali, barabara na maeneo ya makazi ili kuboresha mazingira na kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi,” anafafanua Mkuu huyo wa Mkoa wa Dodoma
Mwisho