Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodo.a
Wataalamu wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi nchini wameagizwa kuhakikisha miradi yote mikubwa yenye mvuto wa kibiashara nchini inatekelezwa kwa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) ili kuipunguzia Serikali mzigo wa kugharamia miradi hiyo.
Agizo hilo limetolewa jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Omolo, kwa niaba ya Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Elmaamry Mwamba, wakati akifungua Kikao Cha Kuimarisha Ushirikiano kati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Tanzania Bara kuhusu masuala ya ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).
Alisema utekelezaji wa miradi kupitia PPP ni sehemu ya kujenga uchumi imara na ni suala ambalo linatekelezwa na nchi nyingi ulimwenguni.
“Msiogope, hata nchi zilizoendelea zinateleza miradi yao kupitia PPP, ukiangalia madaraja na majengo mbalimbali wameyatekeleza kupitia PPP, Sekta Binafsi wakipewa nafasi wanafanya vizuri”, alibainisha Bi. Omolo.
Aliwaagiza wataalamu hao kukuza uelewa wa dhana ya PPP kwa wadau mbalimbali kwa kuwa bado kuna changamoto ya uelewa wa dhana hiyo pamoja na faida zake.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Zanzibar, Bw. Rashid Ali Salim, aliwaagiza wataalam hao kuhakikisha wanayafanyia kazi yale yote waliyokubaliana katika kikao hicho hususani suala la kuwa na mkakati wa pamoja wa kuuza fursa na kuibua miradi ya pamoja ya PPP ili kuimarisha sekta ya PPP nchini.
Naye, Kaimu Kamishna wa Kitengo cha Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), Wizara ya Fedha, Bw. Bashiru Taratibu, alisema katika kikao hicho kuna masuala mbalimbali wameazimia kuyatekeleza ikwemo maboresho ya Sheria ili kurahisisha shughuli za PPP nchini hususani katika kutekeleza miradi ya pamoja katika ya Zanzibar na Tanzania Bara.
“Tumejadili kuhusu miradi ya pamoja ambayo Sekta Binafsi inaweza kutekeleza kama mradi wa Daraja la Dar es Salaam hadi Zanzibar, lakini kila sehemu wana Sheria yao ya PPP, kwa hiyo tumekaa kuona namna bora ya kutekeleza suala hilo iwapo mwekezaji atajitokeza”, aliongeza Bw. Taratibu.
Alisema Tanzania inahitaji kuwa na Sera au Sheria ya PPP inayoelezea utekelezaji wa miradi ya pamoja kati ya Zanzibar na Tanzania Bara kwa kuwa suala kama hilo limeshajitokeza katika nchi za Afrika Mashariki ambapo kuna miradi ambayo inaunganisha nchi moja na nyengine na kwasasa tayari kumeshaandaliwa Sera ya PPP ya Afrika Mashariki.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), David Kafulila alisema katika kikao hicho wamejadiliana mambo mbalimbali ya kurahisisha suala la ubia nchini ili kuipunguzia mzigo Serikali wa kugharamia miradi ya maendeleo ambayo inaweza kugharamiwa kupitia PPP.
Alisema Tanzania kwa sasa inafanya vizuri katika eneo la PPP ambapo kwa Tanzania Bara kuna takribani miradi 74 ambayo ipo katika hatua za mwisho kuanza kutekelezwa na Zanzibar kuna zaidi ya miradi 13.
“Tumekubaliana mambo mengi kuhakikisha kwamba katika eneo hili la ubia tunafanya mkubwa zaidi na tunakubaliana kitumia sekta binafsi kufanya miradi ambayo serikali ingeweza kufanya kwa kutumia kodi, mikopo, ushuru, tozo pamoja misaada,” amesema Kafulila.
Amesisitiza kwamba kuna umuhimu wa kuzidi kuongeza nguvu ya kutumia eneo hili la ubia kufanikisha miradi mingi ambayo ingeweza kuhitaji kutumia kodi,” amesema.
Kafulila ameongeza kuwa Tanzania inafanya vizuri kwenye mikopo kwa kuwa ripoti zinaonyesha uwiano wa deni na uchumi wa Tanzania ni asilimia 47, kiwango ambacho kiko chini ukilinganisha na mataifa mengine ya Afrika Mashariki.