Miradi ya maji lazima itekelezwe kwa wakati kama serikali ilivyopanga ili wananchi wapate huduma ya maji safi na salama, na kujishughulisha na kazi nyingine za maendeleo, ikiwamo kutumia maji hayo kuongeza thamani ya bidhaa mbalimbali na kuleta maendeleo zaidi.
Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema hayo baada ya kukagua miradi ya maji katika wilaya za Monduli, Karatu, Bagamoyo na Kisarawe hivi karibuni.
Aweso, akiwa katika miradi ya maji wilayani Monduli na Karatu alisema mkandarasi atakayepewa kandarasi katika mradi wa maji na kuzembea katika kufanikisha mradi husika au mtaalamu wa serikali kushiriki kuhujumu mradi, wote hawatakuwa na nafasi katika sekta ya maji hapa nchini na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Kukamilika kwa miradi ya maji wilayani Monduli kwa wakati ni muhimu. Takwimu zinaonyesha Wilaya ya Monduli yenye vijiji 62, kwa wastani upatikanaji wa maji ni asilimia 64. Aidha, kwa nyakati za masika upatikanaji wa maji huongezeka na kuwa asilimia 76. Uzalishaji wa maji yanayowafikia wananchi kila siku ni lita milioni 1.3.
Hata hivyo, Waziri Aweso anasema kufanya utafiti na kupata vyanzo vya maji vya uhakika ni jambo la msingi kabla ya kutekeleza mradi wa maji. Wilaya ya Monduli ni moja ya wilaya ambazo wananchi wake wanajihusisha na ufugaji. Aidha, chanzo kikuu cha maji katika wilaya hii ni mabwawa, visima virefu na chemchemi.
Pamoja na hayo, kwa mjini, mahitaji ya maji hususan katika mji wa Monduli ni lita milioni 1.6 kwa siku, na wastani wa uzalishaji ni lita milioni 1.3 kwa siku. Upotevu wa maji ni asilimia 30, hivyo kufanya asilimia 70 ya uzalishaji wa maji kuwafikia wateja, sawa na lita 935,000 kwa siku. Upatikanaji huu wa maji ni sawa na asilimia 57 kwa mji huo.
Ili kuongeza nguvu katika kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi, Naibu Waziri Aweso kwa kuwashirikisha viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli na watendaji wengine wa serikali wilayani humo, wameamua Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Monduli (MOUWSSA) kuwa chini ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA). Kwa mujibu wa Aweso, hatua hiyo itasaidia kuongeza nguvu ya utaalamu na ari zaidi katika kufanikisha huduma ya maji safi na yenye uhakika kwa wananchi.
Upatikanaji wa maji wilayani Monduli hutegemea vyanzo husika, kwa mfano, Monduli ukanda wa Bonde la Ufa, hali ya upatikanaji wa maji ni nzuri na kwa wastani, asilimia 80 ya wakazi wote hupata maji, ambayo ni sawa na watu 49,031 kati ya 61, 502.
Ukanda wa kati hali ya upatikanaji wa maji ni ya wastani na asilimia 42 ya wananchi hupata maji, sawa na watu 33,178 kati ya 80,226. Eneo jingine ni ukanda wa Monduli juu, ambako hali ya upatikanaji wa maji imekuwa ya kuridhisha. Katika ukanda huu, wananchi 12,755 kati ya 18,044 hupata maji, yaani asilimia 71 hupata maji. Ikumbukwe kuwa, lengo la serikali ni wananchi kufikiwa na huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yao.
Hata hivyo, katika hatua nyingine, ziara ya Naibu Waziri Aweso ilibaini kuwapo kwa changamoto ya gharama za mitambo ya kusukuma maji kwenda wilayani Monduli kutoka katika visima vya Ngaramtoni kwa umbali wa zaidi ya kilometa 27, na tayari viongozi wa halmashauri walikwisha kuwasilisha changamoto hiyo katika kikao husika.
Kuhusu changamoto hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Stephen Ulanga, anasema halmashauri hiyo imepanga kufanya utafiti wa maji ya ardhini ili kuwa na maji safi, salama na yenye uhakika katika maeneo ya karibu na kuepuka gharama za kuchukua maji katika vyanzo vilivyoko mbali. Maeneo yaliyoainishwa kwa kufanyiwa utafiti huo ni Loosimingori, Makuyuni na Naalarami ili kuondokana na matumizi ya maji ya mabwawa.
Changamoto nyingine inayoainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Ulanga, ni matumizi ya mitambo inayotumia mafuta ya dizeli kusukuma maji safi ili yawafikie wananchi.
Akito mfano, alisema mradi wa maji Mswakini unaozalisha lita 27,300 kwa saa na kutoa huduma kwa wananchi zaidi ya 8,000 kuwa unaendeshwa kwa nishati ya mafuta ya dizeli na hutumia takriban lita 200 kwa wiki. Gharama za uendeshaji kwa mwezi zinatajwa kuwa wastani wa shilingi milioni 11.
Ulanga aliongeza kuwa pamoja na changamoto hiyo ya gharama ya kusukuma maji, mradi huo unatoa huduma kwa wananchi wa wilaya jirani ya Babati, kikiwamo Kiwanda cha Minjingu.
Mradi mwingine unaofanana na huo katika uendeshaji ni mradi wa maji Lemioni uliojengwa mwaka 2008. Ulanga anasema kuwa mradi huo pia unatumia nishati ya dizeli, na unazalisha lita za ujazo 15,000 kwa saa. Mafuta yanayotumika ni lita 1,120 kwa mwezi na mradi unahudumia wakazi zaidi ya 70,000 wa Makuyuni.
Akizungumzia changamoto hizo, Aweso anasema nia ya serikali ni kufikisha maji safi na salama ya uhakika kwa wananchi, kwa hiyo serikali imezipokea changamoto hizo na kwamba kinachofanyika ni serikali kuhakikisha umeme unafika katika vyanzo hivyo ili kupunguza gharama za kusukuma maji, pia kuwafikishia wananchi huduma ya maji safi, salama na yenye kutosheleza kwa gharama ndogo zaidi.
Akiwa wilayani Monduli, Naibu Waziri Aweso alibaini kasoro za kitaalamu katika utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Lendikinya ambao ni moja kati ya miradi ya vijiji 10 wilayani Monduli unaotekelezwa kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP) ulioanza tangu mwaka 2017.
Katika mradi huo, licha ya kasoro kadhaa za kitaalamu zilizobainishwa na mradi husika ukiwa haujakamilika kwa wakati, Naibu Waziri Aweso alimtaka mkandarasi na wataalamu kusimamia mradi huo kwa karibu na kuainisha maeneo yote yenye upungufu na kuzitatua kabla hajarudi wakati mwingine kukagua utekelezaji wa mradi huo. Aidha, alisisitiza wananchi kushirikishwa kwa sababu mradi huo ni kwa ajili ya wananchi.
Mradi wa Lendikinya utapokamilika utatoa huduma ya maji safi kwa wananchi 6,000 wa Kijiji cha Lendikinya. Aidha, mifugo nayo itapata maji.
Kila halmashauri ya wilaya ilipangiwa kutekeleza miradi ya maji katika vijiji 10. Miradi hiyo ilianza kutekelezwa Septemba, 2013 na hadi sasa inaendelea. Miradi hii inatekelezwa kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia na Serikali ya Tanzania. Wilayani Monduli miradi ikikamilika itahudumia vijiji 16 vya Kipok, Kloriti, Moita Bwawani, Naalarami, Lolkisale, Nyoriti, Emairete, Eluwai, Lepurko, Mbuyuni, Selela, Mbaash, Engaruka Juu, Engaruka Chini, Irerendeni na Oldonyo Lengai. Mradi wa Lendikinya Monduli ndio bado haujakamilika, thamani yake ikiwa ni shilingi bilioni moja.
Wakati huohuo, wilayani Karatu changamoto iliyobainika ni miradi ya maji kutokuwa na kiwango cha ufanisi cha kama ilivyotarajiwa, sababu kubwa ya hali hiyo ikitajwa kuwa ni upungufu wa kiusanifu kwa miradi iliyokamilika na isiyokamilika. Miradi hiyo ilipoanza kutekelezwa mwaka 2012/2013 haikufanyiwa mapitio ya usanifu upya na ilitekelezwa kwa hali ile ile ilivyosanifiwa awali na mtaalamu mshauri Kampuni ya Tanplanet Njegimi Express ambayo hata hivyo iliachishwa kazi kwa kushindwa kukidhi viwango.
Wilayani Karatu wastani wa upatikanaji wa maji safi na salama vijijini ni asilimia 61.39, ambayo ni sawa na idadi ya wakazi 126,726 kati ya wakazi wote 206,426 wa vijijini. Kwa upande wa mjini, wastani wa upatikanaji wa maji ni asilimia 33 sawa na wakazi 17,707 kati ya watu 51,749.
Lakini katika hali ya kujiridhisha kuhusu utekelezaji wa miradi ya maji Karatu, Naibu Waziri Aweso alimtaka mkuu wa wilaya hiyo kuwakutanisha wote waliohusika na miradi hiyo ili kuweka mambo sawa.
Pamoja na hilo, changamoto nyingine inayoainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Theresia Mahongo ni Vyombo vya Watumiaji wa Maji (COWSO) kushindwa kukusanya mapato kikamilifu ili kuendesha miradi ya maji.
Pamoja na changamoto hizo, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Karatu (KARUWASA), Kanael Palangyo, anasema Karatu mji imejipanga kufika asilimia 95 ya utoaji huduma ya maji kwa wananchi kwa kujipanga kuendeleza visima vitatu; viwili vya Ayabale na kimoja cha Bwawani. Visima hivyo vina uwezo wa kuzalisha mita za ujazo 59 kwa saa, sawa na mita za ujazo 1,416 kwa siku.
Serikali kupitia Wizara ya Maji inatekeleza Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP II). Utekelezaji wa programu hii, pamoja na mengine, unahusisha programu nyingine mbalimbali za usimamizi na uendelezaji wa rasilimali maji nchini. Nia hasa ni kufikisha maji safi, salama na yenye kutosheleza kwa asilimia 85 kwa wananchi vijijini na asilimia 95 mijini ifakapo mwaka 2020.
Kwa ujumla, juhudi za serikali katika kuboresha huduma za maji vijijini zimekuwa zikifanyika kupitia Programu ya WSDP II inayohusisha ujenzi, upanuzi na ukarabati wa miundombinu ya miradi ya maji vijijini ikiwa ni pamoja na kujenga miradi ya visima virefu na vifupi, kujenga mabwawa katika maeneo yenye ukame na ujenzi wa miradi mikubwa na miradi ya kitaifa ambayo vyanzo vyake ni maziwa na mito.
Mwandishi wa makala hii ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Maji.